Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu
ametembelea Gereza Kuu la Isanga Jijini Dodoma kwa lengo la kusikiliza changamoto
zinazowakabili Maafisa wa Magereza katika kuwatunza wafungwa pamoja na
kusikiliza changamoto zinazowakabili mahabusu.
Akizungumza baada ya kutembelea Gereza Kuu la Isanga,
Mkurugenzi wa Mashtaka amesema kuwa lengo la kutembele wafungwa na mahabusu ni
kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo kwa misingi ya sharia na kanuni zake.
“kufanya haya yote ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo
lakini tukipata hizi changamoto na kusikiliza tunaenda kuzifanyia kazi na
kuzishughulikia. Changamoto tulizozipokea ambazo hazipo chini ya Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka tunazichukua na kuzipeleka ofisi ambazo zinahusika lengo
ikiwa ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo.”
“Mahabusu wengi ambao nimewasikiliza wamesema kesi zao
zimechelewa upelelezi lakini hali halisi ni kwamba kesi zao hazijachelewa
upelelezi kwa kuwa tayari umekamilika na kinachosubiriwa ni utaratibu wa
kesheria ambao utawezesha kesi hizo kusikilizwa na Mahakama Kuu.”











