• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

WAZIRI PINDI CHANA AFANYA ZIARA KATIKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefanya ziara ya kutembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa lengo la kujadililiana mambo mbalimbali yahusuyo utendaji kazi wao, Muono wa mbele, mafanikio na changamoto wanazokutana nazo.

Ziara hiyo imefanyika tarehe 2 Novemba, 2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo Waziri Pindi Chana ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa majukumu wanayoyafanya katika kushughulikia mashauri mbalimbali ya Jinai kwani kesi nyingi zimefanikiwa kuendeshwa vizuri Mahakamani.

"Dhamana tuliyopewa ni kuhakikisha Haki, Amani na Usalama vinapatikana katika nchi yetu." Ameyasema hayo Mhe. Waziri. 

 Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja Ofisi hiyo ilipata mafanikio katika kuendesha Mashtaka ambayo ni kuokoa fedha zilizopatikana kwa njia ya Uhalifu na kutaifisha mali zilizotumika kwenye Uhalifu huo ili kuhakikisha wahalifu hawanufaiki chochote na Uhalifu.

"Hivyo basi katika kipindi hicho tumeweza kuokoa fedha, magari, nyumba, viwanja na madini kutoka kwa wahalifu ikiwa ni lengo kuwakatisha tamaa wahalifu ili watambue kuwa uhalifu haulipi." Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu. 

Aidha, katika taarifa hiyo Mkurugenzi Mwakitalu amesema kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefanikiwa kupunguza mlundikano wa mahabusu na wafungwa katika magereza zilizopo nchini kwani katika miezi michache iliyopita mahabusu walikuwa ni wengi kuliko wafungwa. Kwa taarifa za magereza kwa mwezi Oktoba mahabusu waliopo ni jumla ya 9,000 na wafungwa waliopo ni jumla ya 18,000. Na hii ni moja ya sababu ya uimarishaji wa ofisi za Mashtaka Mikoa pamoja na kusogeza huduma katika ofisi za Mashtaka Wilaya kwani imewezesha mashauri mengi kusikilizwa kwa wakati na kwa haraka na hivyo kupelekea haki za washtakiwa kupatikana kwa haraka.

Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Mashtaka ameeleza baadhi ya changamoto zinazoikabili Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni pamoja na Ufinyu wa Bajeti, uhaba wa watumishi, upungufu wa vitendea kazi, ongezeko la aina mpya ya Uhalifu kwasababu makosa mengi yanafanyika kwa njia ya mitandao hivyo basi ili kuweza kudhibiti uhalifu huo  Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wapelelezi na wadau wengine wa haki jinai wanapaswa kujengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ili kuweza kukabiliana na changamoto hiyo.

Nae pia Mkurugenzi wa Divisheni ya Utaifishaji Mali, Makosa yanayovuka Mipaka na Uhalifu Mahususi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Faraja Nchimbi alitoa shukrani kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana kwa niaba ya Menejimenti na Watumishi wote wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kuahidi kuwa maelekezo ambayo yametolewa hususani katika  kuzingatia kwamba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iwekeze katika kufanya kazi kwa ukaribu na wadau kutoka ndani na nje ya nchi. Kuwekeza katika mikakati ya upatikanaji wa viwanja kwa maeneo ya makazi kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, kuongeza nguvu katika eneo la usimamiaji wa Utaifishaji na Urejeshaji Mali  zinazotokana na Uhalifu pamoja na maeneo mengine yanayopaswa kuboreshwa.

"Tunashukuru kwa pongezi ambazo umetoa na hii inaashiria namna ambavyo unatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni moja ya Taasisi zinazounda jumla ya Wizara ya Katiba na Sheria, na sisi tunaahidi kuyatekeleza na kuongeza ufanisi na utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kwamba kero zinazowakabili wananchi katika sehemu ya usimamizi wa Haki jinai zinaondoshwa." Amebainisha hayo Mkurugenzi Nchimbi.



Share:

"Mapambano dhidi ya Uhalifu tumeyapa kipaumbele" - DPP

 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu ametoa onyo kwa Watanzania ambao wanajihusisha na vitendo vya kiuhalifu na kuahidi kuongeza mikakati mipya ili kuhakikisha kwamba wanakabiliana na Uhalifu kwa nguvu zote ili wahalifu watambue kwamba uhalifu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haulipi.

Mkurugenzi Mwakitalu ameyasema hayo wakati akifungua Kikao cha Menejimenti, Wakuu wa Mashtaka, Wakuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mikoa na Wakuu wa Upelelezi Mikoa kinachofanyika tarehe 29 Septemba hadi 01 Octoba, 2023 Makao Makuu Jijini Dodoma.

Pia Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja kulingana na Maazimio waliyoyaweka na kuangalia ni kwa kiasi gani Maazimio hayo yametekelezeka, changamoto walizokutana nazo na sababu ya changamoto hizo, pamoja na kujadili kuweka malengo ya mwaka mwingine unaokuja.

Sambamba na hayo Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa Makosa ya Rushwa, Uhujumu Uchumi na Ufisadi yana athari kubwa sana katika jamii kwani yanaongeza gharama za maisha na pia yanasababisha wananchi kukosa baadhi ya huduma ambazo wangeweza kuzipata. 

"Kusipokuwa na amani, kusipokuwa na utulivu hakuna mtu ambae atakwenda kufanya shughuli za maendeleo". Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu ameendelea kueleza kuwa endapo Madawa ya Kulevya yataendelea kutumika pasipo kudhibitiwa basi nguvu kazi ya taifa itapotea.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema kuwa moja ya jukumu walilonalo ni kuhakikisha wanaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa kwa pamoja kama timu  ili kusogeza huduma kwa wananchi hususani katika kuharakisha masuala ya uchunguzi wa uendeshaji wa mashtaka.

"Katika utekelezaji wa majukumu yetu tunagusa moja kwa moja haki za wananchi." Ameyasema hayo Mkurugenzi Mkuu Salum Hamduni.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini  Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai ameeleza kuwa ushirikiano ni jambo muhimu sana katika kuwatendea haki wananchi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



Share:

WAZIRI CHANA AZINDUA MIONGOZO MITATU (3) KUTOKA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefanya Uzinduzi wa Miongozo Mitatu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambayo ni Kuwajali na kuwalinda Mashahidi, Urejeshaji na Utaifishaji Mali zinazotokana na Uhalifu pamoja na Ushirikiano wa Kisheria katika Masuala ya Jinai. 



Uzinduzi huo umefanyika tarehe 27 Septemba, 2023 Jijini Dar es salaam ikiwa na lengo la kusaidia kuleta ufanisi na kuwezesha kujenga mfumo imara wa Kisheria katika upatikanaji wa Haki Jinai utakaowawezesha Wananchi kufanya shughuli zao kwa amani, utulivu na usawa.

Waziri Chana amesema kuwa Miongozo hii inatija kubwa kwa mashahidi ambao ndio nguzo muhimu katika upatikanaji wa Haki Jinai nchini kwani ili kuleta amani katika nchi na kutenda haki panahitajika kuwa na mashahidi.



Pia Dkt. Pindi Chana alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini kwani uamuzi huo unalenga kuhakikisha kuwa mapendekezo yaliyotolewa yatasaidia kuboresha mfumo wa Haki Jinai kwa kusaidia wananchi wengi kupata haki zao ikiwemo ulinzi wa mashahidi.



Aidha Waziri Chana ametoa wito kwa wananchi kuwa mabalozi wa amani kwa kutoa ushirikiano wa kutosha pale ambapo wanaona kuna uhalifu umefanyika au unafanyika wasiache kutoa taarifa katika vyombo husika.



"Ikiwa kama kuna eneo mtu kwa namna moja ama nyingine au kikundi cha watu watakuwa wanatenda uhalifu, sisi kama Wizara tutakuwa tayari kuwapokea kama wateja wetu halali. Tunahitaji Tanzania iwe ni mfano wa kuigwa na Mataifa mbalimbali kwani Tanzania sio sehemu salama ya Makosa ya Jinai." Ameyasema hayo Waziri Chana.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema kuwa wana imani Miongozo hiyo itaenda kuwaongezea tija katika utendaji wao wa kazi za kila siku.



Pia Mkurugenzi Mwakitalu alitoa shukrani kwa Wadau mbalimbali, Wasimamizi wa Sheria na Vyombo vya Uchunguzi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kuandaa nyaraka za Miongozo hiyo.



"Kwa kushirikiana na Taasisi hizi tumeweza kuelewa maeneo ambayo yana mapungufu katika utendaji kazi wetu kwa kufahamu changamoto pamoja na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuweka katika Miongozo yetu." Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.



Sambamba na hilo Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa kupitia miongozo hiyo itasaidia kuwa na usimamizi unaofanana katika kushughulikia Mashauri ya Jinai kutoka sehemu mbalimbali na pia itasaidia kuhakikisha wahalifu hawanufaiki na mali wanazopata kwa njia ya uhalifu, au mali zinazotumika katika kutenda uhalifu.



Share:

Menejimenti na Watendaji wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wakutana Kuweka Mikakati ya Kazi

 Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amefungua Kikao kazi baina ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Menejimenti, Wakuu wa Mashtaka wa Mkoa, Wilaya, Waendesha Mashtaka Viongozi (PAI), Wahasibu/ Watendaji wanaofanya kazi za kihasibu katika Mikoa na Wanachama hai wa Mashtaka SACCOS kinachofanyika tarehe 28 hadi 29 Agosti, 2023 Jijini Dodoma.

Akifungua kikao kazi hicho Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa lengo la  kikao hicho ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali yanayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kupima utendaji bora wa kazi.

Sambamba na hayo, Mkurugenzi Mwakitalu amesema kuwa katika kikao kazi hicho watajadiliana na kukumbushana masuala mbalimbali zikiwemo changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao  ili kutoa mapendekezo ya kuzitatua kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa Taasisi.

Pia Mkurugenzi Mwakitalu amewataka Viongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha watumishi wengine waliopo chini yao ambao bado hawajajiunga na Mashtaka SACCOS ili waweze kujiunga na Chama hicho.

"Tujiunge na tukope kwenye SACCOS yetu kwa riba nafuu, masharti nafuu ili tuweze kupunguza changamoto za kifedha tunazokutana nazo." Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

 


Share:

WAZIRI SIMBACHAWENE ASISITIZA JUU YA MATUMIZI SAHIHI YA TEHAMA KATIKA TAASISI ZA UMMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amezitaka Taasisi zote za  Serikali kujikita katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kuboresha utendaji kazi wa Taasisi unaosaidia kutatua changamoto za kiutendaji.

Waziri Simbachawene amezungumza hayo wakati akihutubia kwenye Hafla ya Makabidhiano ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya, Kuchakata na Kutunza Kumbukumbu za Kesi za Jinai (Case Management Information System) na Tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iliyofanyika tarehe 23 Agosti, 2023 Makao Makuu Jijini Dodoma.

Mhe. Waziri ameeleza kuwa Mfumo huo ambao umejengwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka utakuwa ni mwarobaini katika kuhakikisha kwamba usimamizi wa mtiririko wa kesi unakwenda vizuri na haki ya mtu inapatikana kwa wakati.

"Nimejulishwa kuwa hadi sasa zaidi ya kesi 17,411 zimesajiliwa katika mfumo huu ambapo kati ya kesi hizo kesi 7,361 zimeshafikia mwisho na kutolewa hukumu. Na baadhi ya kesi 10,050 zipo katika hatua mbalimbali za maamuzi. Hakika hayo ni mafanikio na maendeleo makubwa katika nchi yetu ambayo yamelenga kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na pia ni mfano wa kuigwa kwa Taasisi nyingine zinazohusika na utoaji wa huduma kwa umma." Ameyasema hayo Mhe. Waziri.

Waziri Simbachawene ameendelea kueleza kuwa lengo kuu la Mfumo huo ni kurahisisha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kushughulikia usimamizi na uendeshaji wa kesi za jinai. Na kwa ujumla mfumo huo utakuwa wazi na kupunguza malalamiko kwa wananchi juu ya maamuzi mbalimbali yanayotolewa na mahakama.

Sambamba na hilo Mhe. Simbachawene amesema kuwa Tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imejengwa kwa lengo la kusaidia utoaji wa taarifa sahihi kwa wananchi na wadau zinazohusiana na shughuli mbalimbali za Ofisi ya Taifa ya Mashtaka

Pia Waziri Simbachawene alitoa wito kwa Taasisi nyingine za umma katika kuhakikisha kwamba hazisuisui na zinafanya jitihada kuongeza matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yao kama jinsi sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 inavyoeleza.

"Hii itaongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na pia kutimiza azma kwa Serikali ya awamu ya sita ya  Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akisisitiza sana kwa nia ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema wao kama Serikali dhamira yao ni kuona haki zote zinatolewa kwa wakati, hivyo ana imani mfumo huo utakuwa chachu ya kufanikisha hilo.

"Haki ni suala muhimu sana na inapaswa itolewe kwa wakati na hivyo kupitia mifumo ya TEHAMA tunataka kuhakikisha haki zinatolewa kwa wakati". amesema Waziri Gekul.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema kuwa Mfumo huo ni nyenzo muhimu sana ambayo itasaidia katika kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwani kupitia Mfumo huo utasaidia kutunza Kumbukumbu za majalada yote wanayopokea kutoka Vyombo vya Uchunguzi hadi yanapohitimishwa Mahakamani.

"Kupitia Mfumo huu haki za mashtaka zitapandishwa, hukumu zitapatikana humu, na pia hata mtiririko wa mgawanyo wa majalada utaonekana katika mfumo huu."  Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.



Share:

WATUMISHI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA KWA KUTENDA HAKI.

 Wa Kwanza Kulia ni Mkurugenzi wa Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Tumaini Kweka akiwa pamoja na viongozi wengine katika hafla fupi ya kuwaaga watumishi waliohama vituo vya kazi na kuwakaribisha waliofika Mkoani Shinyanga July 22,2023.

Na Ofisi ya Mashtaka-Kahama Shinyanga.

Mkurugenzi wa Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Tumaini Kweka amewataka  Watumishi wapya kuwa makini kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kuwa Shinyanga ni mojawapo ya Mikoa yenye vishawishi vingi hivyo wafanye kazi kwa weledi kwa kuongozwa na uadilifu, hofu ya Mungu, kwa kuwa ni jukumu lao  huku akiwataka kuongozwa na weledi na ufanisi ili kutenda haki iliyo na usawa kwa wananchi.

Bw. Kweka ameeleza hayo wakati akifungua halfa fupi ya kuwaaga waliokuwa Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Shinyanga na kuwakaribisha Watumishi wapya wakiwemo waliojariwa na waliohamia Mkoani Shinyanga wa ofisi hiyo pamoja na kupata chakula cha jioni kiliyoandaliwa na Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Shinyanga.

Mkurugenzi Kweka amesema kuwa kuajiriwa ni sehemu ya kuaminiwa kuwatumia wananchi hivyo jukumu lao ni kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhudumia  wananchi kwa kuzingatia weledi wa kazi yao na taaluma yao

Aidha Mkurugenzi Kweka ameeleza kuwa kazi hiyo ngumu na inavishawishi vingi hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kuzingatia miiko ya utumishi wa umma kwa kujiepusha na rushwa pamoja na kupindisha haki hali ambayo itasababisha kudhohofika kwa utendaji.

Bw. Kweka pia ameishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoani Shinyanga kwa kufanya kazi zake kwa kujituma na kuleta ufanisi katika kushughulikia mashauri ya kesi  mbalimbali ambapo wamefanya kazi kubwa na yenye kutukuka.

 “Miongoni mwa watumishi waliokuwepo hapa Shinyanga na Kahama ambao ni wanawake wameweza kufanya kazi zao kwa uweledi na umakini mkubwa na kuleta tija kwa jamii pamoja na wao wenyewe ambapo wapo waliopanda na kuwa Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa na Wilaya  kwenye maeneo mbalimbali hivyo watumishi wapya wanapaswa kuiga mfano wa wengine.” Amesema Mkurugenzi Kweka”

Bw. Kweka amesema kuwa Ofisi ya  Mkoa wa Shinyanga imekuwa mfano katika utendaji kazi wake na kuamsha hali katika maeneo mengine ambapo amewataka waajiriwa wapya kuwa mabalozi wazuri wa kazi za Ofisi hiyo.

Akizungumza kwa niaba Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kahama Bw. Robert Kwela amewataka watumishi hao kuishi katika misingi ya ajira kwa kuwa ni wengi wanaotafuta, sambamba na kuwakata Vijana waliongia kazini katika ajira mpya kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na kutenda haki.

Naye Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Shinyanga Bi. Ajuaye Zegheli  amewahakikisha ushirikiano na  watumishi wapya sambamba na kuwataka wanaposhughulika na mashtaka kutanguliza maslahi mapana ya umma na si kutanguliza mahitaji yao binasfi.

Aidha watumishi hao pia wametoa azwadi mbalimbali ikiwemo tunzo za heshima kwa watumishi wenzao ikiwa nis ehemu ya kutambua mchango wako katika utumishi  wakati wakiwa Mkoani  Shinyanga.ambapo pia Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) Sylvester Mwakitalu amepewa tunzo ya heshima kwa mchango wake katika usimamizi na usikilizaji wa changamoto za watumishi hao.

Tazama Picha mbalimabali katika matukio yaliyofanyika






















 

 

 

 

 

Share:

Labels

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .