Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kushirikiana na wadau wengine mbalimbali wakiwepo Magereza, Polisi, TAKUKURU na Taasisi za Kifedha kwa kuzindua Mwongozo wa Ushirikiano wa Wadau katika Upelelezi wa Utakatishaji Fedha Haramu, Ugaidi na Ufadhili wa Ugaidi ambao wanapambana katika kuzuia makosa hayo makubwa ambayo yanapangwa na kuvuka mipaka.
Katika uzinduzi huo uliofanyika tarehe 24 Mei, 2023 Jijini Dodoma Waziri Ndumbaro ameeleza kuwa Mwongozo huo ni muhimu sana kwani unachangia katika kuwaleta wadau mbalimbali pamoja ili juhudi zao za kudhibiti makosa hayo makubwa matatu ambayo ni Utakatishaji Fedha, Ufadhili wa Ugaidi na Ugaidi wenyewe viweze kufanyika kwa pamoja kwa kuwa makosa hayo ni makosa ambayo ni hatari sana, makubwa na ni makosa ambayo yanapangwa.
Aidha, Mhe. Ndumbaro amemesema kuwa umuhimu wa Mwongozo huo pia utasaidia kupata namna bora ya kushirikiana na nchi nyingine mbalimbali duniani zikiwepo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sadic, Afrika na Duniani kote.
"Mtu yeyote anaweza akafanya uhalifu wowote na kujipatia fedha zinazotokana na uhalifu huo na anaweza kuzitumia fedha hizo na kuziweka katika nchi nyingine. Hivyo kwa kuweka ushirikiano huo tunaweza kumkamata mhalifu huyo na kupata ushahidi wake katika nchi husika alikowekeza fedha hizo na kuchukua jukumu la kutaifisha mali zake na kuwa mali za Serikali. Ni jambo ambalo litasaidia kuondosha uhalifu wa namna hiyo katika jamii yetu." Amefafanua hayo Waziri Ndumbaro.
Mwongozo huu pia unalenga katika kukuza ushirikiano pamoja na kuwajengea uwezo wadau wote hususani kwa jamii kwani ndio wadau namba moja ili waweze kufahamu juu ya jambo husika linaloendelea katika jamii husika.











