• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

WAZIRI KABUDI AHIMIZA USHIRIKIANO KWA TAASISI ZINAZOSIMAMIA HAKI JINAI

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi amezitaka Taasisi zinazounda haki jinai kujenga utamaduni wa kuwa pamoja, kufanya kazi pamoja, kusaidiana  na kuwezeshana ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Waziri Kabudi amebainisha hayo wakati akifungua Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu pamoja na Wakuu wa Mashtaka Mikoa, Wakuu wa Upelelezi Mikoa na Wakuu wa TAKUKURU Mikoa kinachofanyika tarehe 9 na 10 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.

Prof. Kabudi amesema kuwa Taasisi zinazosimamia Haki Jinai nchini zinatakiwa kuendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata Haki zao kwa wakati ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia misingi ya haki ili kuhakikisha amani, utulivu na umoja vinatamalaki kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema umoja huo wa Utatu uliundwa kwa lengo la kurahisisha utendaji wao wa kazi na pia kutatua changamoto wanazokumbana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ambazo kwa namna moja ama nyingine zinachelewesha ama kukwamisha haki za watu.

"Tuliamua kila mwaka tuwe tunakutana Menejimenti ya Utatu na Viongozi wa ngazi za mikoa ili kujadiliana na kutathmini yale ambayo tumeyafanya pamoja na kuweka mikakati ya mwaka mwingine unaokuja, na tumekuwa na mijadala mizuri, mawasiliano na mada mbalimbali na kuongeza ufanisi katika majukumu yetu". Amefafanua hayo Mkurugenzi DPP

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kamishna Ramadhani Kingai amesema ushirikiano wao umeleta manufaa makubwa kwao katika utekelezaji wa utoaji haki  katika jukwaa la haki jinai. 

"Ni rai yangu kuendeleza na kuimarisha ushirikiano huu hususani katika kushughulikia makosa yanayovuka mipaka hivyo ni muhimu kukuza ushirikiano huu sio tu kwa Taasisi zetu bali kuwa na mashirikiano kutoka katika taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi." Amebainisha hayo DCI Kingai.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Bw. Crispin Chalamila ameeleza kuwa kupitia mashirikiano waliyonayo ya Utatu, ameshuhudia ongezeko la idadi za kesi zilizofunguliwa mahakamani baada ya kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka, aidha wamekuwa na vikao vya viongozi na watendaji katika ngazi za mikoa vinavyofanyika mara kwa mara na hivyo kusaidia kuharakisha maamuzi mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU amebainisha kuwa kupitia mashirikiano hayo Waendesha Mashtaka watatu wa TAKUKURU wamepata vibali vya kuendesha kesi katika Mahakama Kuu na pia kuahidiwa vibali hivyo kuongezwa. Pia kumekuwa na ongezeko la idadi ya kesi zinazofunguliwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kutokana na vikao vya pamoja vya kupitia majalada.

"Ni matarajio yetu kwamba kupitia kikao hiki tutaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano huu ambao 

kimsingi unasaidia kuondoa malalamiko ya ucheweleweshwaji wa haki jinai" Amefafanua hayo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU

Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Bw. Mgeni Jailan Jecha ametoa pongezi na shukrani kwa Menejimenti ya Bara kwa mwaliko wa ushiriki katika kikao hicho cha Utatu kwani kutasaidia  kuimairisha zaidi mashirikiano ya sekta za Jinai baina ya Bara na Zanzibar, pia kujifunza na kupata uzoefu wa utendaji kazi kupitia kikao hicho cha Utatu.


Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo akitoa neno la ukaribisho na utambulisho wakati wa Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu pamoja na Wakuu wa Mashtaka Mikoa, Wakuu wa Upelelezi Mikoa na Wakuu wa TAKUKURU Mikoa kinachofanyika tarehe 9 na 10 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.

Waziri Kabudi akisalimiana na viongozi wa Utatu mara baada ya kuwasili kufungua Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu pamoja na Wakuu wa Mashtaka Mikoa, Wakuu wa Upelelezi Mikoa na Wakuu wa TAKUKURU Mikoa kinachofanyika tarehe 9 na 10 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.


Washiriki wa Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu pamoja na Wakuu wa Mashtaka Mikoa, Wakuu wa Upelelezi Mikoa na Wakuu wa TAKUKURU Mikoa wakifuatilia kwa umakini mada mbalimbali zinazowasilishwa kwenye kikao hicho.

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi kufungua Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu pamoja na Wakuu wa Mashtaka Mikoa, Wakuu wa Upelelezi Mikoa na Wakuu wa TAKUKURU Mikoa kinachofanyika tarehe 9 na 10 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.



Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu pamoja na Wakuu wa Mashtaka Mikoa, Wakuu wa Upelelezi Mikoa na Wakuu wa TAKUKURU Mikoa kinachofanyika tarehe 9 na 10 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.

Share:

"Rushwa isipodhibitiwa uchumi utayumba"- DPP

 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema rushwa isipodhibitiwa kikamilifu itasababisha  uchumi  wa nchi kuyumba  hali itakayochangia wananchi kutopata huduma muhimu za kijamii ikiwemo  afya, maji, barabara na maendeleo ya jamiii.

Mkurugenzi wa Mashtaka ameeleza hayo wakati  wa Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu ( Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) kilichofanyika tarehe 8 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.

Kikao hicho cha Menejimenti kinalenga kufanya tathmini ya kazi na kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya taasisi hizo katika kufanya kazi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wote na wananchi wanapata huduma bora.

Mkurugenzi Mwakitalu ameitaka Menejimenti kufanya kazi kwa weledi, umakini na pia kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria.

"Kazi zetu zinagusa haki za watu, zinagusa maisha ya  watu, maamuzi tunayoyafanya yote yanagusa haki za watu,  tumeaminiwa na kupewa dhamana hii." Amefafanua hayo DPP 

Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka amewasihi Menejimenti kushiriki kikamilifu kikao hicho kwani michango yao ya thamani inahitajika sana ili kuweza kutoka na maazimio ambayo yatasaidia kuboresha utendaji kazi wao kwa mwaka huu mpya.



Share:

DCI AHIMIZA KUUNGANISHA NGUVU NA WADAU WENGINE

 Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Bw. Ramadhani Kingai amesema ni muhimu kikao cha Taasisi zinazounda Utatu kuwafikiria na kuwaunganisha wadau wengine kwa kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanafanya jambo ambalo linawasaidia wananchi na kurahisisha maisha yao hususani kwenye masuala ya ufuatiliaji wa haki za msingi kwa mujibu wa sheria zilizopo.

"Kuwa pamoja kunasaidia kurahisisha mawasiliano na kuwezesha mambo mengine kuendelea sawasawa." 

DCI Kingai amebainisha hayo wakati akifungua Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu ( Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) kilichofanyika tarehe 8 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Ramadhani amesema kikao hicho kitajadili masuala mbalimbali yanayohusu utoaji wa haki nchini ambayo yaliibuliwa wakati wa ukaguzi wa pamoja uliofanyika mwaka huu 2024 kwa lengo la kuhakikisha wanaboresha utendaji kazi wao lakini pia utoaji wa haki kwa ajili ya Watanzania.

"Tutapitia utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita ambayo yatatupa mwanya wa kujitathmini utendaji wetu wa kazi kwa mwaka mzima. Baada ya kupitia maazimio hayo wajumbe wote wa kikao tutakuwa na fursa ya kuona nini kilifanyika na nini hakikufanyika ili kuweka mpango kazi kuhakikisha  tunaleta mafanikio chanya." Amefafanua hayo DCI Kingai 

Aidha Mkurugenzi huyo ameitaka Menejimenti kuwa na umoja katika kazi ili kujenga vyema jukwaa la haki jinai ambapo Taasisi hizo tatu ni muhimili katika kutekeleza jukumu la kuwahudumia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Ni matumaini yangu kuwa kikao hiki cha Menejimenti kitatoka na maazimio mahususi ambayo yataenda kuwasilishwa kwa watendaji wetu na kutumika kama dira katika kuboresha utendaji kwa mwaka mwingine." Ameyasema hayo DCI Kingai.

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Crispin Chalamila ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali na kuyasimamia yale yote ambayo watakubaliana kama Utatu kwani umoja huo ni muhimu sana katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao waliyopewa dhamana ya kuyasimamia.



Picha ya pamoja ikijumuisha Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu (katikati), Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Bw. Ramadhani Kingai, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Bw. Crispin Chalamila wakiwa na washiriki wa Kikao cha Menejimenti ya Taasisi zinazounda Utatu ( Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) kilichofanyika tarehe 8 Oktoba, 2024 Jijini Dodoma.



Share:

MASHTAKA SPORTS CLUB YAONDOKA NA KOMBE PAMOJA NA MEDALI SHIMIWI

 Katika hafla ya kuhitimisha Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI)  yaliyofanyika mkoani Morogoro, Mashtaka Sports Club imeibuka na ushindi wa kupata zawadi ya kombe moja na medali mbili kutoka katika mbio za baiskeli kilometa 50 na riadha mita 200.

Mashindano hayo ya SHIMIWI yamehitimishwa tarehe 5 Oktoba, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene.

Mshindi wa mbio za baiskeli kilometa 50 kutoka Mashtaka Sports Club iliwakilishwa na Bw. John Mgave ambaye aliibuka kuwa mshindi wa tatu na kukabidhiwa kombe moja na medali moja, na kwa upande wa riadha mita 200 iliwakilishwa na Judith  Malata ambaye pia aliibuka na kuwa mshindi wa tatu na kukabidhiwa medali moja.

Katika hatua nyingine, Mashtaka Sports Club imepokea zawadi mbili za medali ambazo zimetolewa na Uongozi wa SHIMIWI ikiwa ni ishara ya kuutambua mchango wao katika kushiriki kwenye Mashindano hayo. Zawadi hizo zimekadhiwa kwa viongozi wa Mashtaka Sports Club ambao ni Mwenyekiti na Katibu wa Mashtaka Sports Club.

Akizungumza baada ya mashindano, Mwenyekiti wa Mashtaka Sports Club Bw. Juma Mahona amesema Kwa ujumla mashindano yameisha kwa mafanikio kwa kuwa timu ya kamba ya wanawake ilifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali huku timu ya kamba wanaume ikiishia hatua ya robo fainali. Na timu ya Mpira   miguu ilitolewa katika hatua ya kumi na sita bora. 

“Haya ni mafanikio Kwa Mashtaka Sports club Kwa kuwa ni mara ya pili kushiriki katika mashindano haya". Amebainisha hayo Mwenyekiti Mahona

Mshiriki wa Mashindano ya SHIMIWI kutoka Mashtaka Sports Club Bi. Judith Malata akipokea zawadi ya medali kutoka kwa viongozi walioshiriki SHIMIWI ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi zake katika mashindano hayo



 Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akimkabidhi zawadi ya kombe la ushindi kwa mshindi wa tatu (3) wa mbio za baiskeli kilomita 50 ambae ni  Bw. John Mgave kutoka Mashtaka Sports Club  ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi zake katika mashindano hayo.


Mwenyekiti wa Mashtaka Sports Club Bw Juma Mahona akiwa na Katibu wa Mashtaka Sports Club Bi. Severina Mnyaga  wakipokea zawadi ya medali pamoja na cheti kutoka kwa uongozi wa SHIMIWI ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wao wa kushiriki kwenye mashindano hayo.



Share:

Labels

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .