• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA SERIKALI UJENZI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA TEMEKE

 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi wa Ofisi za Mashtaka za Mikoa na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kusogeza huduma kwa wananchi  pamoja na kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma za mashtaka ya jinai nchini jambo litakalosaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi na kulinda amani na Usalama ambayo ni dhamira ya Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kukagua maendeleo ya  Miradi ya ujenzi wa Ofisi za Mashtaka za Mikoa ya Kimashtaka Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam, tarehe 12 Machi, 2025 Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Mhe. Dkt. Joseph Mhagama alieleza kuwa Kamati hiyo imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hizo za Mikoa ya  Kimashtaka Temeke na Kinondoni ambapo miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, 2025

Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo, Waziri wa Katiba na  Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, aliipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa maono na utashi wa kutekeleza miradi hiyo ya kimkakati na kueleza imetokana na uongozi bora wa viongozi waliopo.

“Mimi ni Wakili hadi sasa, nimefanya kazi ya Uwakili kwa miaka zaidi ya 30 na nimefanya kazi na Wakurugenzi wa Mashtaka wengi, lakini nikupongeze Mkurugenzi wa Mashtaka Mwakitalu kwa mageuzi haya makubwa ambayo yanahitaji utashi mkubwa, uadilifu na kujitoa."

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alimshukuru Mhe. Rais, Kamati ya Bunge na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya mageuzi haya muhimu na kueleza kwamba miradi inayoendelea kutekeleza ni matunda ya Kamati hiyo.

Aidha, aliongeza kuwa miradi hii ni sehemu ya Miradi inayoendelea kutekelezwa katika mikoa mingine ambayo ipo katika hatua mbalimbali na kwamba kuanzia mwaka huu Ofisi ya Taifa  ya Mashtaka imeanza pia kutekeleza miradi ya Ujenzi ya Ofisi za Mashtaka za Wilaya ambapo tayari imeanza katika Wilaya 24 ikiwa ni jitihada za kusogeza huduma kwa wananchi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa pongezi kwa kutekelezwa kwa miradi katika Wilaya hizo na kuongeza kwamba itakua na tija kwa Wananchi.

" Tuna imani kuwa mradi huu ukikamilika kwa wakati utaweza kusaidia sana Watanzania, ambao wanausubiri kwa hamu kubwa sana." Amefafanua Mkuu wa Wilaya.

Aidha, Mhe. Mhagama alisema Kamati  inaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo itachochea upatikanaji wa haki kwa wananchi na kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa usimamizi mzuri wa taasisi zake katika utekekelezaji wa miradi  inayofadhiliwa na Serikali.

Sambamba na hilo alitoa rai kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kusimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa asilimia 100 kwa ufanisi ndani ya muda uliopangwa kulingana na mkataba uliopo.




Share:

MIAKA 20 JELA, VIBOKO 12 KWA KUKUTWA NA FISI HAI BARIADI

 Mahakama ya Wilaya Bariadi mkoani Simiyu imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kuchapwa viboko 12 Emmanuel John (31), maarufu kama Chief wa Kilulu, kwa kosa la kukutwa na Nyara za Serikali aina ya fisi akiwa hai na akiishi naye nyumbani kwake.

Mshtakiwa huyo, ambaye ni mganga wa kienyeji, mkazi wa kijiji cha Kilulu kilichopo kata ya Bunhamala, wilayani Bariadi, alipewa adhabu hiyo katika kesi namba 2458/2025 iliyokuwa ikimkabili kwenye mahakama hiyo.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Caroline Kiliwa, mara baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Awali, akisoma kosa la mshtakiwa, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Lupiana Mahenge, aliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa na nyara ya serikali, fisi akiwa hai, akimfuga nyumbani kwake ikiwa ni kinyume cha sheria.

Alisema kuwa mnamo tarehe 1 Januari, 2025 katika eneo la kijiji cha Kilulu, mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema ambao waliripoti kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai ndani ya nyumba yake.

Alieleza kuwa mtuhumiwa aliishi na fisi huyo kama mnyama wa kufuga kinyume na kifungu cha 86 (1) na kifungu kidogo cha (2)(C)(III) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori sura ya 283, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Alifafanua kifungu hicho kinasomeka pamoja na kifungu cha 14, jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1), na kifungu cha 60 (2) cha Sheria ya Kupambana na Uhujumu Uchumi sura ya 200, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Upande wa mashtaka, katika kuthibitisha kosa hilo, ulipeleka mashahidi sita ambao waliithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka.

Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama imsamehe kwa kuwa anategemewa na familia ya watoto wanne wakiwemo mapacha, ndipo hakimu akatoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na viboko 12 ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine.


Share:

DPP AWAELEKEZA WANAWAKE WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUTUNZA RASILIMALI ZA SERIKALI

 

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwa mstari wa mbele kutunza rasilimali walizopewa na serikali ili kuendelea kuwasaidia katika majukumu yao ya kila siku.

“Muwe ni watu wa kujali na mtunze rasilimali kidogo ambazo tumezipata kwani Serikali imewekeza fedha na rasilimali zingine na tunatarajia wanawake mtakuwa kinara katika kutuvusha kwenye hili hivyo tunataka kuona matokea ya uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.’’ 

Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo wakati aliposhiriki  chakula cha jioni pamoja na  watumishi wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka Makao Makuu Jijini Dodoma, Arusha, Mkoa wa Kilimanjaro na Manyara mara baada ya kushiriki kwenye kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 8 Machi, 2025.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ina watumishi wengi wa kike ambao ni zaidi ya asilimia 65 hivyo wanapaswa kujiamini ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kujituma.

“Utendaji kazi wetu lazima uonyeshe kwamba taasisi yetu ina wanawake wengi kwasababu nyie ni watu wa kujali. Tunataka watu waone Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inafanya vizuri kwasababu ya wanawake.’’ Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu

Pia Mkurugenzi Mwakitalu ametoa pongezi kwa wanawake hao kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kipindi chote cha  Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wakati walipotembelea banda la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Jijini Arusha.  

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewataka wanawake wa ofisi hiyo kuutumia uwezo mkubwa waliopewa na  Mwenyezi Mungu wa Ualimu,Ulezi  kuipendezesha na kuzidi kuiinua  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kazi zao kwa kuzingatia kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo inasema "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.

‘Kama Kauli mbiu ya Mwaka huu 2025 inavyosema,Tuutumie uwezo mkubwa kabisa ambao Mungu ameweka ndani yetu ili kuhakikisha taasisi yetu inaongoza  kutenda haki ndani ya nchi hii hata watakapotafuta siri ya mafanikio ya Ofisi yetu watambue kwamba ni  sababu ya mchango mkubwa pia wa wanawake  waliopo ndani ya ofisi hiyo.” Amesema Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka

Aidha, amewataka wanawake hao kuhakikisha kuwa  wanapoondoka mahali hapo waondoke wakiwa na  chachu ya kufanya kazi kwa bidii,kuwafundisha na kulea wengine na kuahidi kutokuiangusha taasisi yao.

‘’ Ipo nguvu kubwa ndani ya mwanamke ya kuratibu mambo,kufundisha na kulea.

 Ninaomba iyo nguvu pia tuiweke kwenye taasisi yetu kuwafundisha  watumishi walio chinj yetu, ili tuweze kuleta matunda na kufikia maono makubwa ya taasisi yetu.’’ Amefafanua Naibu DPP


Watumishi wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma, Arusha, Mkoa wa Manyara na Kilimanjaro wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kushiriki kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 8 Machi, 2025



Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo akipokea zawadi ya tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa wanawake Bi. Atugonza Kawamala kwa niaba ya wanawake wote wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika taasisi.


Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo akikata keki kuashiria upendo na umoja kwa watumishi wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka




Share:

ALIYEUA MWIZI AHUKUMIWA KUNYONGWA MPAKA KUFA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Iringa imemuhukumu Elia Martine Ngaile @ Rasta (54) kunyongwa mpaka kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la Mauaji ya Luca Pascal Mang’wata.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 7 Machi 2025 na Mhe. Jaji Angaza Mwipopo baada ya kusikiliza mashahidi wanne (4) wa upande wa jamhuri pamoja na vielelezo viwili (2) na kujiridhisha kwamba kesi upande wa Jamhuri imethibitishwa pasipo kuacha shaka.

Katika kesi hiyo ya Kikao cha Jinai Na. 26195 ya mwaka 2024, Bw. Elia ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ndiwili, wilaya ya Kilolo mkoa wa Iringa alikuwa anakabiliwa na shtaka la Mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.) 

Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe  21 Mei, 2024 katika kijiji cha Lundamatwe, kitongoji cha Kibati, Wilaya ya Kilolo ambapo inadaiwa mshtakiwa alikuwa akitafuta mwizi wa ng’ombe wanne (4) na alifanikiwa kumkamata marehemu na kumfungia katika kilabu cha pombe na marehemu alipotaka kukimbia alimkamata na kumkata na panga kichwani, mkononi na miguuni. Kitendo hicho kilisababisha marehemu kuvunjika miguu yote miwili na fuvu la kichwa kuwa wazi pamoja na ubongo kuonekana. Majeruhi alipelekwa hospitali kwa matibabu hatimae alifikwa na umauti akiwa anapatiwa matibabu hospitali ya Rufaa Iringa.

Kesi hii imeendeshwa na Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambao ni Muzzna Mfinanga akisaidiana akisaidiana na Majid Matitu.

Share:

AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA.

Mahakama ya Wilaya ya Momba imemuhukumu Bw. Laurent Emmanuel Sigula (18) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia kusafirisha dawa za kulevya aina bhangi yenye ujazo wa gramu 240.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 6 Machi, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu Raymond Kaswaga baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa mashtaka. 

Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 24 Aprili, 2024 katika  eneo la Migombani, Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba alipokutwa na Mtendaji wa Mtaa akimiliki misokoto 122 ya bhangi yenye gramu 240 kisha kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi na alipohojiwa alikiri bhangi hiyo kukutwa nyumbani kwake.

 Kesi hii iliendeshwa na Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka akiongozwa na Wakili Shadrack  Meli akisaidiana na Sadam Kitembe.

Share:

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 2 JELA KWA KUMUUA BABA YAKE BILA KUKUSUDIA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Sumbawanga imemuhukumu Kiumbe John Kantanga (28)  kifungo cha miaka 2 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kumuua baba yake mzazi bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 5 Machi 2025 na Hakimu Mwandamizi na mwenye Mamlaka ya Ziada Luambano baada ya kuridhika na kiri ya mshtakiwa na maelezo ya shauri.

Katika kesi hiyo ya Kikao cha Jinai Na. 16279 ya mwaka 2024,Bw. Kiumbe ambaye ni mkazi wa kijiji cha Bumanda, wilaya ya Nkasi mkoa wa Rukwa alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuua bila ya kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.

Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe  25 Mei, 2024 katika kijiji cha Bumanda, wilaya ya Nkasi ambapo inadaiwa mshtakiwa alimpiga shoka baba yake baada ya kutamkiwa maneno yaliyomfanya kujawa na jazba.

Kesi hii imeendeshwa na japo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Ladislaus Akaro akisaidiana na Mwanaisha Liwawa.

Share:

AHUKUMIWA KUNYOGWA MPAKA KUFA KWA KUUA.

 

Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga yenye Mamlaka ya ziada imemhukumu  Sanyiwa Nyorobi  maarufu kwa jina la Ntemasho na kumpa adhabu ya kunyogwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la Mauaji ya mkazi wa Sumbawanga Tiga Washa.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 4 Machi, 2025 na  Hakimu Mkazi mwenye Mamlaka ya ziada Mhe. Joseph Luambano baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri.

Katika kikao cha Jinai namba 14637 cha mwaka 2024, Bw. Sanyiwa ni mkazi wa Kijiji cha Kilangawana kilichopo ndani ya Wilaya ya Sumbawanga , Mkoa Rukwa alikuwa anakabiliwa na shtaka la Mauaji  kinyume na kifungu cha 196 and 197 cha Sheria ya kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 18 Desemba,2023 katika Kijiji cha Kilangawana kilichopo ndani ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoa Rukwa ambapo inaidaiwa siku ya tukio mshtakiwa alivamia nyumbani kwa Tiga Washa ( Marehemu) na kumjeruhi kwa kumkatakata mapanga katika mwili na kupelekea kifo.

Kesi hiyo imeendeshwa na  Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Neema Erasto Nyagawa akisaidiana na Mathias Yatti Joseph.

Share:

AKUHUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA MITATU JELA KWA KOSA LA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA

 

Mahakama ya Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam imemhukumu Amosi Janus Nyitara 

 (23) kifungo cha miaka 03 jela baada ya kupatikana na dawa za  kulevya aina ya bhangi kiasi cha gramu 49.2.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 28 Februari, 2025 na  Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Vicky Mwaikambo  baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 2685/2024, Bw. Amos  ambaye ni mkazi wa Mbagala Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la kukutwa na dawa za  kulevya aina ya bhangi gramu 49.2 kinyume na kifungu cha 17(1) (b) cha Sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya , (Sura ya 95 Rejeo la mwaka 2019)

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 14 August, 2023 katika eneo la Kibonde Maji B Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam, alikutwa na madawa hayo isivyo halali.

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Sabina Ndunguru Bundala akisaidiana na Nicas Kihemba.

Share:

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 20 JELA KWA SHAMBULIO LA AIBU DHIDI YA BINTI MWENYE UMRI WA MIAKA 13


 Mahakama ya Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es salaam imemhukumu  Hilary Benard Matia (37) kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la shambulio la aibu dhidi ya  binti mwenye umri wa miaka kumi na tatu (13).

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 28 Februari, 2025 na  Hakimu wa Mahakama hiyo Mhe. Vicky Mwaikambo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 2969/2024 ya Bw. Benard  ambaye ni mkazi wa Toangoma  Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la Shambulio la aibu  (grave sexual abuse) kinyume na kifungu cha 138C(1) (a) and (2) (b) cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 01 December, 2023 katika eneo la Kongowe Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam ambapo inaidaiwa siku ya tukio mshtakiwa kwa tamaa za kimwili  alimnyonya mdomo mhanga ambaye ni mwanafunzi wake.

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Sabina Ndunguru akisaidiana na Nicas Kihemba.

Share:

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 30 JELA KWA KOSA LA KUZINI NA MAHARIM


 Mahakama ya Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam imemhukumu Bw. Silvester Michael Chihongwe (42) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka miwili

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 28 Februari, 2025 na  Mhe. Catherine Madili baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 9568/2024, Bw. Silvester ambaye ni mkazi wa Kurasini, Shimo la Udongo Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuzini na Maharimu (incest) kinyume na kifungu cha 158(1) cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 22 Machi, 2024 katika eneo la Kurasin, Shimo la Udongo Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam ambapo inadaiwa mama wa mtoto huyo alikwenda kuchota maji aliporudi alikuta tayari mtoto huyo amefanyiwa kitendo hicho na baba yake mzazi.

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Abdon Andrew Bundala akisaidiana na Shabani Twahil Shaban.

Share:

 

Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam imemhukumu Bw. Arafath Laurence Thadei kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya kiasi cha shilingi milioni moja pamoja na kuchapwa viboko sita wakati wa kuingia gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka Manusura mwenye umri wa miaka 15.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 27 Februari, 2025 na Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam Mhe. Janeth Mtega baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 22093/2024 Bw. Thadei ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la ubakaji kwa Manusura kinyume na kifungu cha 130(1),(2) (a) na 131 cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo katika tarehe zisizojulikana kati ya mwezi wa 12 mwaka 2023 na tarehe 4 Machi 2024 katika eneo la Tungi,Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam ambapo inaidaiwa alimuingilia kimwili binti wa miaka kumi na tano(15).

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Bw. Sayi Gugah akisaidiana na Epiphania Mushi.

Share:

Labels

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .