Mkurugenzi wa Mashtaka Bw.Biswalo Mganga amewataka Makatibu Sheria nchini kuhakikisha wanatumia vizuri mfumo mpya wa Ukusanyaji,
Uchakataji, Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za
Makosa ya Rushwa kwa njia ya Kidijitali hali itakayowezesha utoaji wa
Takwimu sahihi kwa maendeleo ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga wakati akifunga Mafunzo ya siku 6 ya Makatibu
Sheria kutoka Mikoa yote ya Tanzania bara mafunzo yaliyofanyika Manispaa ya
Singida yakiwa na lengo la kuwajengea
uwezo makatibu hao katika Ukusanyaji, Uchakataji,
Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya
Rushwa kwa mfumo wa Kidijitali.
Ameeleza kuwa jukumu la watumishi wa Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka ni kuwajibika kwa umma na
serikali hivyo Makatibu Sheria wanalo
jukumu kubwa la kuhakakikisha huduma bora za mashtaka zinawafikia wananchi na
kuiona ofisi kuwa yao.
“Naomba niseme jukumu kubwa tulilonalo ni kuwajibika kwa Umma,
Taasisi na Serikali kwa kuhakikisha tunatoa huduma bora na za kuvutia kwa wananchi, nisingependa kusikia lugha mbaya toka kwenu
zikiwahusu watu wanaokuja kwenu kutafuta msaada badala yake tumieni lugha nzuri
kwani majalada yote yanapitia kwenu”amesema Bw.Biswalo
Biswalo amesema Makatibu Sheria ndiyo mlango wa Kupokea
majalada hivyo wasiwe chanzo cha kujihusisha na vitendo vya rushwa kwani
kufanya hivyo kunadhoofisha maendeleo ya Nchi na Taifa kwa ujuma
“Sitaki kusikia ninyi Makatibu
Sheria mnakuwa vyanzo vya kujihusisha na vitendo vya Rushwa ndani ya
taasisi kwa sababu tu watu wote wanaanzia kwenu na wala msidanganyike kwani mkifanya hivyo
mtaishia pabaya, siko tayari kumvumilia
mtu anayekula Rushwa”Bw.Biswalo
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Biswalo amewaasa watumishi
hao kutoharibu taaluma yao ya Ukatibu Sheria kwa kujihusisha na uvujishaji wa siri za
Nyaraka za Ofisi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha maadili pia hali ambayo
inahatarisha usalama wa nchi.
“Niwaombe ninyi Makatibu Sheria mnayo nafasi kubwa ya
kutupatia na kusaidia taarifa za siri
juu ya watu wanaofutilia majalada yetu hususani makanjanja ili tumfahamu mtu anayefuatilia
ana lengo gani na tujue tunaanzia wapi kumchukulia hatua”Bw.Biswalo
Aidha, Biswalo akizugumzia suala la Mfumo mpya wa Ukusanyaji,Uchakataji,
Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya
Rushwa kwa mfumo wa Kidijitali amewataka
kuhakikisha taarifa zinaingizwa kwenye mfumo kwa uhakika na umakini huku akiwaonya
Makatibu hao kwenda kufanya kazi zao kwenye internet Café ambako nyaraka za
serikali husalia na kuhataraisha usalama
wa ofisi na nchi kwani watu wabaya wanaweza kuzitumia kwa maslahai yao binafsi.
“Ni marufuku kutumia barua pepe za Ofisi kwenye Kompyuta za internet café utumike ndani ya ofisi na Kompyuta za
ofisi tu kwani kutumia huko taarifa zinabaki
na watu wanaanza kudukua hivyo kwa hili atakayebainika sitamwonea huruma
lazima hatua kali zichukulie dhidi yake”Bw.Biswalo
Biswalo ameongeza kuwa utumiaji wa mfumo huo mpya wa
Uchakati na utumaji wa taarifa isiwe
sababu ya kuachana na mfumo wa zamani wa regista ambapo amesisitiza mifumo yote kwenda samabmba
hadi pale mfumo wa kidijitali utakapokuwa umeimarika na kusimama vizuri
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa
Kesi na Uratibu wa Upelelezi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambaye anashughulikia Usimamizi wa Kesi Bw. Tumaini Kweka amesema kuwa Makatibu Sheria ni watu muhimu sana hivyo
mafunzo hayo yamejikita kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa
viwango vinavyotarajiwa pamoja na kuwawezesha kukabiliana na changamoto
wanazokutana nazo
“Naomba kukutaarifu
kuwa mafunzo haya yameshirikisha washiriki 30 kutoka Mikoa yote 26 ya Tanzania
Bara hivyo tuna imani kuwa kile walichojifunza
hapa kinaenda kuwa chachu kubwa kwa wengine waliosalia kwenye maeneo yao”amesema Bw. Kweka
Kweka ameongeza kuwa katika mafunzo hayo jumla ya Mada nane
zimewailishwa kutoka kwa watalaamu wa ndani na nje ya taasisi hiyo
waliowasilisha mada kwa kina na washiriki kupata nafasi ya kuuliza maswali na
kujibiwa”
Naye mwakilishi wa washiriki wa Mafunzo hayo ya Ukusanyaji,Uchakataji,
Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya
Rushwa kwa njia ya Kidijitali Bi Faraja amesema kuwa mafunzo hayo
kwao ni chachu kubwa ya kuboresha utendaji kazi wao hususani kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Idara ya Usimamizi
wa Kesi na uratibu wa upelelezi na
Programu ya BSAAT kupitia Divisheni ya Makosa ya Udanganyifu, Utakatishaji
fedha na Rushwa Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka.
Idrisa
Heri Swalehe Afisa Tehama, kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka(NPS) Mkoani
Mwanza akitoa elimu ya Ukusanyaji,Uchakataji,
Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya
Rushwa kwa mfumo wa Kidijitali
Washiriki wakiendelea kujifunza kwa vitendo wakati wa mafunzo ya Ukusanyaji, Uchakataji, Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai, na Kumbukumbu za Makosa ya Rushwa kwa njia ya Kidijitali kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga akitazama
namna zoezi la elimu kwa vitendo
linavyofanyika baada ya Makatibu Sheria
kupata Mafunzo ya Ukusanyaji, Uchakataji,
Utumaji na Utunzaji wa Takwimu za Kesi za Jinai na Kumbukumbu za Makosa ya
Rushwa kwa mfumo wa Kidijitali.
Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka ambaye anashughulikia usimamizi
wa Kesi Tumaini Kweka akifuatilia kwa ukaribu mafunzo.
Mkurugenzi
wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga akiwa ameketi kwa pamoja na Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka ambaye anashughulikia usimamizi
wa Kesi Tumaini Kweka wakiendelea kufuatilia mafunzo.