• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

WAWILI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMDANGANYA DPP KUWA NI MAOFISA USALAMA WA TAIFA

Mwonekano wa Mbele wa Jengo la Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam 

Na Rebeca Kwandu Dar es Salaam.

 Mfanyabiashara, Joshua Jelemia (37) na Yahaya Abdallah (31) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam  kujibu mashtaka mawili ya kujifanya Maofisa Usalama wa Taifa (TISS) katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) na naibu mkurugenzi wa mashtaka.

 Washtakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama hiyo Juni 18, 2021 na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,  Godfrey Isaya. 

Wakiwasomewa Mashtaka na  wakili wa Serikali Mwandamizi,  Wankyo Simon amedai  kuwa watuhumiwa hao walitenda  makosa hayo Juni 12, 2021  katika ofisi za DPP zilizopo jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

 Inadaiwa siku hiyo wawili hao walifika Ofisini kwa (DPP) Slyvester Mwakitalu  na naibu wake (DDPP), Joseph Pande na kujitambulisha   kuwa wao ni maofisa kutoka TISS.

 Baada ya kusomewa Mashitaka hayo, upande wa Mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na hivyo wapangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya  kuwasomea washtakiwa hoja za awali. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 22, 2021 na washtakiwa kurudishwa rumande baada ya kukosa dhamana.
Share:

DPP MWAKITALU ASEMA ATAPELEKA MAHAKAMANI MASHAURI YENYE USHAHIDI KAMILI.

 Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu akipokea Maelezo kutoka kwa Mkuu wa Gereza la Mahabusu Segerea Mrakibu Mwandamizi wa Magereza(SSP)Daniel Mwakyoma wakati  alipotembelea Gereza hilo Juni 13,2021.

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu amehitimisha ziara yake ya kutembelea  na kukagua hali ya Magereza ya Mkoa wa  Dar es Salaam baada ya kutembelea na kuzungumza na Mahabusu pamoja na wafungwa walioko katika magereza yote matatu ya mkoa huo.

Akizungumza mara baada ya kujionea hali ilivyo katika Magereza hayo, baada ya kuhitimisha ziara kwa kutembelea Gereza la Mahabusu Segerea  DPP Mwakitalu  amesema Changamoto alizoziona ndani ya magereza hayo zitamsadia katika kufanya maamuzi na kuboreha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

DPP Mwakitalu alisema changamoto zilizowasilishwa na baadhi ya mahabusu walioko gereza la Segerea ambazo  hazipo ndani ya uwezo wa Ofisi ya Mashtaka atakahikikisha anazifikisha kwa wahusika ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi ambapo amesema maeneo yanayohitaji suluhisho la pamoja atahakikisha anakaa na wadau ili kutafuta suluhisho la pamoja.

“Kwa changamoto ambazo ziko chini ya ofisi yangu, nitazifanyia kazi kwa  haraka kadri iwezekanavyo ili haki  iweze kutendeka,haya mengine  ambayo yako nje ya Ofisi yangu nitawashirikisha wadau wakiwemo mahakama, wapelelezi na wachunguzi ili tuwe na suluhu ya pamoja”Alisema DPP Mwakitalu

Aidha, DPP Mwakitalu akizugumzia chagamoto ya kuchelewa kwa upelelezi wa mashauri mbalimbali alisema kuwa wapelelezi wanaoshugulikia kesi ni wadau wake wa karibu  kwani bila uwepo wao yeye hawezi kufanya kazi hivyo ameahidi kukaa kwa pamoja  ili kesi zilizoko mahakamani ambazo upelelezi wake haujakamalika uweze kufika mwisho.

Alisema  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kutekeleza majukumu yake itaendelea kufanya kazi zake kwa kutenda haki.

Mwakitalu alisema kuwa kwa sasa Ofisi yake kwa pamoja na watendaji wataanza kazi ya kupitia upya majalada ya kesi ili kubaini kama yana ushahidi wa kutosha kesi ziendelee na kama ushahidi wake ni hafifu  atayafanyia maamuzi.

“Naomba  niwaeleze changamoto hizi na ushauri wenu nimeupokea kwa sasa hatua  tulizonazo ni kupitia upya majalada ya kesi ili kuona lipi linafaa kuendlea a lipi linafaa kufanyiwa maamuzi upya”alisema DPP Mwakitalu

Katika hatua nyingine DPP alisema kuwa Ofisi yake kwa sasa  itahikikisha inapeleka kesi mahakamani zenye ushahidi kamili na zile ambazo bado hazijapata Ushaihidi kamili hazitafikishwa Mahakamani ili  kuondoa changamoto ya Msongamano Magerezani .

Kuhusiana na suala la utoaji wa vibali vya kesi DPP Mwakitalu alisema kuwa atahakikisha vibali vya Kesi(Concert)  ambazo zimekwama kutokana na kukosa kibali hicho atahakikisha  vibali hivyo vinatolewa ili kesi ziweze kuendelea.

Aidha, DPP Mwakitalu ametembelea magareza ya Keko,Segerea na Gereza Kuu Ukonga ambapo alisema kuwa huo ni Mwendelezo wa ziara zake za kutembelea na kukagua hali ya magereza hapa nchini, kusikiliza  kero na changamoto za wafungwa na mahabusu ili Ofisi yake iweze kuzitafutia Suluhu

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu akiwasili katika gereza la Mahabusu Segerea na kupokelewa na mkuu wa gereza hilo Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Daniel Mwakyoma Mapema juni 13,2021.Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu(Kushoto)akisalimiana na Mkuu wa Gereza la Mahabusu wanawake Segerea Mrakibu wa Magereza Iyunge Saganda (wa pili kutoka kushoto) wakati wa ziara ya kutembelea na kusikiliza changamoto za Mahabusu .

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu akisalimiana na baadhi ya maafisa wa magereza katika gereza la Mahabusu Segerea Mkoani Dar es salaam wakati wa ziara yake.Mkuu wa Gereza la Mahabusu Segerea Mrakibu Mwandamizi wa Magereza(SSP)Daniel Mwakyoma  akiwaongoza Viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)Sylvester Mwakitalu kuelekea Gereza la  Mahabusu wanaume.

  

Share:

DPP MWAKITALU ATEMBELEA NA KUKAGUA HALI YA MAGEREZA UKONGA NA KEKO JIJINI DAR ES SALAAM, AAHIDI KUZITAFUTIA UFUMBUZI CHANGAMOTO

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw.Sylvester Mwakitalu (mwenye suti nyeusi) akiwa ameongozana na Mkuu wa Gereza la Ukonga SSP Hamis Lissu (kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Magereza na kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakitembelea Maeneo mbalimbali ya gereza la Ukonga kujionea hali halisi ya gereza hilo.

Na Rebeca Kwandu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amefanya ziara ya ukaguzi  katika Magereza ya Keko na Gereza Kuu Ukonga ya jijini Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya magereza hayo, kuzugumza na mahabusu pamoja na wafungwa na kuahidi kushirikiana na vyombo vingine kutatua changamoto zinapelekea kuwepo kwa msongamano  ndani ya magereza hayo.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo aliyoongozana na baadhi ya  watendaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na Mkoa wa Dar es Salaam , Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Mwakitalu amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea hali halisi ya magereza, kuwasikiliza mahabusu  na wafungwa ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili  mahabusu na wafungwa kufuatia kesi mbalimbali zilizoko mahakamani.

“Ujio wangu hapa ni kwa ajili ya kujionea hali halisi ya msongamano  pamoja na kusikiliza kero za mahabasu, wafungwa na magereza kwa ujumla ili niweze kufanyia kazi maeneo yale yanayohusu ofisi yangu  “Alisema DPP Mwakitalu.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema Magereza mengi nchini yanakabiliwa na msongamano mkubwa wa  wafungwa na mahabusu kutokana na sababu mbalimbali  ikiwemo kuongezeka kwa hali ya  uhalifu nchini.

Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu amewataka watanzania kuacha kujihusisha na uhalifu hali ambayo inachangia kuongezeka kwa msongamano magerezani huku akiahidi kufanya kazi kwa nguvu na bidii ili mashauri yaweze kusikilizwa kwa haraka na wakati.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Mashtaka ametembelea na kujionea uzalishaji mkubwa wa Bidhaa (Fanicha) zinazotengenezwa na wafungwa katika gereza kuu Ukonga

Ziara hiyo ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini  imelenga katika  kusikiliza, kupokea malalamiko na changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya mashtaka ili ofisi yake iweze kuyatafutia ufumbuzi ili kupunguza changamoto na  msongamano magerezani.

Katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka ameambatana na  Mkurugenzi wa Divisheni ya Utenganishaji wa  Shughuli za Mashtaka  na Upelelezi  Bw. Oswald Tibabyekomya, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam  Bi. Mkunde Mshanga na Wakuu wa Mashtaka Wilaya zote za  Dar es Salaam. 

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu akiwa ameambatana na Viongozi wengine wakati wa zoezi la kutembelea magereza ya Ukonga na Keko Jijini Dar es Salaam mapema leo Juni 12,2021.


Mkuu wa Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es salaam SSP Hamis Lissu akimuongoza Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu pamoja na timu yake wakati walipotembelea Gerezani hapo Mapema leo Juni 12,2021
Mkuu wa Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es salaam SSP Hamis Lissu akimueleza jambo  Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester juu ya hali ilivyo katika gereza hilo.

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu akipokea maelezo ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali unaofanywa na Jeshi la Magereza Ukonga kutoka kwa Mkuu wa kiwanda SP Edger Kaiza leo Juni 12,2021.




Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester akiwa katika picha ya Pamoja na Mkuu wa Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es salaam SSP Hamis Lissu mara ya Kutembelea na Kukagua Magereza hiyo. 

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu  akiwaaga Maafisa wa Jeshi la Magereza Nchini katika Gereza Kuu Ukonga Jijini Dar es salaam mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika gereza hilo. 

Share:

DPP MWAKITALU ATETA NA WATENDAJI WA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU AAHIDI USHIRIKIANO ILI KUMALIZA MRUNDIKANO WA MASHAURI.

Na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka --DSM.

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amekutana na kufanya mazungumzo na Watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam, mapema leo ikiwa ni sehemu ya kukuza Uhusiano na Ushirikiano katika utendaji, ili kuwezesha kumalizika kwa mrundikano wa Mashauri yaliyoko katika Mahakama hiyo.

Akizungumza na Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mkurugenzi wa Mashataka Bw. Mwakitalu amesema kuwa ili kesi ziweze kwenda kwa kasi na usikilizwaji ufanyike kwa haraka, ni lazima Taasisi hizo zishirikiane kwa ukaribu hali itakayosaidia kuondoa kero na changamoto zinazosababisha kuchelewa kesi.

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Mwakitalu amesema kuwa changamoto ya Maridhiano(Pre Bargaining) ambayo imeonekana kuwa tatizo amehaidi ndani ya wiki moja itashughulikiwa na kufanyiwa kazi ili ufanisi wa kazi uweze kuendelea,ambapo timu ya maalumu ya Serikali ya mauala ya Kisheria itakutana na kuona  namna ya kuboresha Sheria ya Maridhiano katika Kesi mbalimbali hususani za Uhujumu Uchumi .

Kuhusiana na suala la Mashauri ambayo awali yalikuwa yana Mkurugenzi, kutoa kibali cha kuendesha kesi, ili hali anaweza kuwakasimisha Utoaji wa vibali hivyo Waendehsa Mashtaka wa Mikoa, Bw. Mwakitalu amesema kuwa yapo Mashauri  ambayo kwa mujibu wa Sheria anaweza kuwaelekeza Waendesha Mashtaka wa Mikoa kuyashughulia, lakini yapo mengine ambayo yanahitaji  kibali chake.

“Kwa sasa Mashauri yote yatakayofikishwa Mahakamani ni yale tu ambayo upelelezi wake umekamilika ikiwa ni mkakaki wa Mahakama ya Tanzania kupitia kwa Jiji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Ibrahim Juma wa kutakwa Mashauri yasizidishe Mwaka yakiwa hayajasikiizwa”Alisema Bw.Mwakitalu

Aidha Bw. Mwakitalu amesema kuwa kwa sasa atahakikisha anasaini Kesi zote zinazo hitaji kibali chake ili zianze kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kuondoa mrundikano wa Mashauri hayo Mahakamani.

Bw. Mwakitalu Ameongeza kwa kusema  kuwa Kesi inapochukua muda mrefu upelekea Mashahidi wengi kupotea na wengine kutoonekana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Kuhama au Vifo, ambapo amewahakikishia watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ushirikiano mkubwa ili kuwezesha ufanikishaji wa Kesi na kupunguza Mlundikano wake Katika Mahakama hiyo.

“Mfano mpaka sasa jumla ya Kesi 369 zimekwisha pitisha muda wake hali inayochangia uwepo wa  Malalamiko ya Wananchi, hivyo basi mimi niwahakikishie Ofisi yangu na Watendeji wangu hawatakuwa kikwazo kwa hili nikiwa DPP wakati wangu” Alisema Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Mwakitalu.

Awali akisoma Risala kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Gedfrey Isaya amesema kuwa mkoa wa Dar es salaam unazo Mahakama za Hakimu Mkazi Nne ambazo ni Hakimu Mkazi Kisutu,Mahakama ya Watoto,Hakimu Mkazi Kivukoni/Kinondoni na Mahakama ya Jiji/Sokoine.

Hakimu Mkazi Isaya amesema kuwa kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Juni 10,2021 Mashauri mbalimbali yameshughulikiwa ambapo Kesi 579 zilibaki kwa Mwaka 2020 huku Kesi 132 zikipokelewa hadi Mei, Kesi 167 zikisikiliszwa

Aidha Hakimu Isaya amesema kuwa zipo jumla ya Kesi 8 ambazo zimechukua muda mrefu kutokana na Mashahidi kuwa changamoto katika upatikanaji wake hali ambayo inapelekea Kesi hizo kuchukua muda mrefu pasipo kusikilizwa.

Hakimu Mkazi Isaya ameongeza kwa kusema kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa moja ni Upelelezi wa Mashauri kuchukua muda mrefu hata kwa Mashauri ya bhangi na kuchangia Mlundikano wa Kesi, pili Mashauri mengi kuwa ya muda mrefu hii ikisababishwa na kutopatikana kwa  Mashahidi,  Mashauri mengi kusubiri Kibali cha Mkurugenzi wa Mashataka na hivyo mengi yanachelewa hata kabla ya kibali kutolewa.

Hakimu Mkazi Isaya maehitimisha kwa kusema kuwa Mashauri mengi ya Nyara za Serikali,Madawa ya kulevya na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)huchukua muda mrefu sana  katika upelelezi wake.

Kikao hicho kilichofanyika leo Juni 11, ni Mwendelezo wa kikao cha awali ambacho kilifanyika mwezi Mei Tarehe 21, mwaka huu kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Watendaji na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  kikiwa na lengo la kutatua changamoto  na malalamiko ya Mlundikano wa Kesi katika Mahakama hiyo.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Mashtaka ametembelea gereza la Keko jijini Dar es Salaam kujionea hali halisi ya gereza hilo na kuzungumza na wafungwa pamoja na mahabusu wa gereza hilo.

 Akizungumza  katika gereza hilo Mkurugenzi wa Mashtaka alisema hali ya mrundikano wa mahabusu na wafungwa katika gereza hilo inampa hamasa ya kufanya kazi kwa nguvu, bidii na maarifa ili kutatua changamoto za Msongamano magereza

Bw. Sylvester amesema kuwa changamoto ya kuchelewa kwa upelelezi iliyowasilishwa kupitia risala iliyotolewa na mahabusu na wafungwa wa gereza hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka alisema atakaa na wapelelezi ili kutatua changamoto hiyo na kufanya maamuzi yatakayosaidia kuondoa changamoto hiyo.

Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka aliahidi kwenda kuangalia upya hati za dhamana zilizotolewa ili kuona kama sababu zilizopelekea kutolewa kwa dhamana hizo zipo au hazipo na endapo zitakuwa hazipo kwa sasa ataziondoa. Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu akizungumza na Wafanyakazi na Watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam(hawapo Pichani)  ikiwa ni mojawapo ya Mkakati wa Ofisi yake kuhakikisha Mashauri yanaendeshwa kwa weledi na kwa wakati.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Bw. Godfrey Isaya Akieleza baadhi ya Changamoto wanazokumbana nazo katika usikilizwaji wa Kesi mbalimbali ikiwemo Upelelezi wa Mashauri kuchukua Muda Mrefu katika Ukumbi wa  Mahakama hiyo Jijini Dar es salaam Juni 11,2021. 

Mkurugenzi wa Mashtaka wa Mashtaka Bw. Sylivester Mwakitalu (kushoto) akiteta jambo na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe. Godgrey Isaya mara baada ya kuzungumza na Watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylivester Mwakitalu akizungumza na watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam kujadili namna Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam wanavyoweza kushirikiana kuondoa mashauri yaliyochukua muda mrefu yaliyokaa kwa muda mrefu katika mahakama hiyo. Jumla ya mashauri 369 bado hayajafanyiwa kazi ambapo kufuatia kikao hicho maamuzi ya kumaliza changamoto hiyo yamefikiwa Kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mhe. Godfrey Isaya.
Watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam wakifuatilia maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylivester Mwakitalu na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam Mhe. Godfrey Isaya wakati wa kikao cha kuzungumzia namna Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama zitakavyoshirikiana kumaliza changamoto ya mrundikano wa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande (kushoto) akifuatilia maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylivester Mwakitalu ( hayupo pichani) wakati akizungumza na Watendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam. Kulia kwa Bw. Pande ni Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Mkunde Mshanga Mwendesha Mashtaka Mkuu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam Wankyo Simon( Katikati)akiwa ameketi pamoja na Mahakimu wa Mahakama hiyo wakati wakimskiliza Mkurugenzi wa Mashtaka Sylvester Mwakitalu Juni 11,2021 katika ukumbi wa Mahakama hiyo.
Mahakimu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiwa katika ukumbi wa Mikutano wa Mahakama hiyo wakimsikiliza Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ambaye hayupo katika Bw. Sylvester Mwakitalu wakati akizungumza na Watumishi na Watendaji wa Mahakama hiyo Juni 11, 2021 Jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Dar es salaam Bi Mkunde Mshanga, akiteta jambo na Mkurugenzi anayesimamia divisheni ya Uendeshaji wa Mashtaka Nchini Bw. Osward Tibabyekomya. 






 

Share:

Labels

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .