Baadhi ya Wakuu wa Mashtaka kutoka Mikoa na Wilaya zote Tanzania bara wakiendelea kufuatilia hotuba ya ufungaji wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya namna ya kukabiliana na kesi za ukatili ambao umekuwa changamoto kubwa kwa sasa nchini.
Wa Kwanza Kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Joseph Pande, katikati ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatib Kazungu akifuatiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini DPP Bw.Sylvester Mwakitalu wakiwa katika picha ya Pamoja.
Ukatili wa Kijinsia umetajwa kuwa mojawapo ya chanzo kikubwa kinachoathiri Afya, Utu, Usalama na Uhuru wa binadam, ambapo muathirika huwa sehemu ya kunyanyasika kisaikolojia, kimwili, kiafya, na kiakili.
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini DPP Bw.Sylvester Mwakitalu akizungumza na washiriki wa mafunzo ya namna ya kukabiliana na kesi za ukatili wa kijinsia nchini.
Ukatili huo hutokana na vitendo anavyokutana navyo ikiwemo kupata matatizo ya afya ya uzazi, mimba zisizotarajiwa, utoaji wa mimba ambao sio salama, magonjwa ya zinaa, UKIMWI na hata kifo.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu akizungumza na Waendesha Mashtaka wa Mikoa, Wilaya, Wapelelezi na Waendesha Mashtaka Viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu amebainisha hayo wakati akifungua Mafunzo maalum kwa Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa, Wilaya na Waendesha Mashtaka Viongozi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yanayofanyika mjini Morogoro tarehe 29 Machi, 2023.
Dkt. Kazungu amesema kuwa kuna baadhi ya mila na desturi za kitanzania ambazo zimefumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na kubaki kufanya bila kuchukua hatua kali za kisheria hali inayochangia uvunjaji wa haki za msingi za kibinadamu.
" Tafiti zinaonyesha ongezeko kubwa la matukio ya ukatili wa kijinsia, ubakaji dhidi ya makundi mbalimbali katika jamii yetu. Hata hivyo bado wahalifu wanaosababisha makosa haya hawajaweza kuwajibishwa ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mapungufu katika Upelelezi, mapungufu katika uendeshaji wa Mashauri hayo mahakamani hivyo kupelekea watuhumiwa wengi kuachiwa huru."Amesema Naibu Katibu Mkuu.
Washiriki wa mafunzo wakiendelea kufuatilia mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani Morogoro.
Dkt. Kazungu ameipongezi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo katika eneo hilo, kwa kuwa kundi hilo ni muhimu katika kufikia malengo ya uendeshaji wa kesi za ukatili hivyo mafunzo hayo yatasaidia katika kushughulikia makosa hayo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashtaka hapa nchini.
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Joseph Pande, akizungumza na washiriki wa mafunzo Mkoani Morogoro.
Dkt. Kazungu ameongeza kwa kusema kuwa kazi kubwa inayofanywa na Waendesha Mashtaka nchini ni kuhakikisha waathirika wanapata haki na stahiki zao huku watuhumiwa wakipewa adhabu kali zinazowapa fundisho watu wengine.
Katika hatua nyingine Dkt. Kazungu ameitaka jamii kukemea vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa changamoto kubwa sana ikiwemo ubakaji, ulawiti na matendo mengine maovu ambayo ni kinyume cha mila na desturi za Mtanzania.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu kwa niaba ya Wizara ya Katiba na Sheria alitoa pongezi kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo katika eneo hilo, sio tu kwa Waendesha Mashtaka lakini pia kwa Wapelelezi kwani mafunzo hayo yatasaidia kuongeza tija katika kushughulikia makosa kwa Wapelelezi na Waendesha Mashtaka katika masuala mazima ya haki jinai.

















