• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

NAIBU DPP AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAAJIRIWA WAPYA

 Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bi. Bibiana  Kileo,amekutana na kuzungumza na Waajiriwa Wapya 60 wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka kada mbalimbali (Mawakili, Madereva na Mkutubi) kwa lengo la kuwakaribisha na kufahamiana.

Waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wamewasili  Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 19 Septemba, 2024 kwa lengo la kupatiwa barua zao za ajira ili kwenda kuanza kazi rasmi katika vituo vyao  vya kazi walivyopangiwa.

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amewaasa Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uadilifu,bidii, na uzalendo  mara wafikapo katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa ili kuleta chachu katika utendaji kwa ofisi na jamii yote  kwa ujumla.



Mkurugenzi wa  Utawala na Rasilimali  Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi akizungumza na Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kuwataka  kwenda kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia misingi ya haki pamoja na kufuata sheria na kanuni zote za utumishi wa umma.


Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bi. Bibiana Kileo akiwa katika picha ya pamoja na Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mara baada ya kuwasili Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 19 Septemba, 2024 kwa lengo la kupatiwa barua zao za ajira ili kwenda kuanza kazi rasmi




Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakisikiliza kwa umakini hotuba ya Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bi. Bibiana Kileo wakati akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika tarehe 19 Septemba, 2024 Jijini Dodoma
Share:

TLS NA OTM WAKUTANA KUJADILI NAMNA BORA YA KUSHIRIKIANA KATIKA UTENDAJI KAZI.

 Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) limefanya ziara ya kutembelea na kukutana na wajumbe wa Menejimenti wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali ya kiutendaji  ili kuimarisha ushirikiano na kurahisisha upatikanaji haki kwa jamii.

Katika kikao hicho Baraza hilo lenye wajumbe wapatao kumi na moja wakiongozwa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Wakili Boniface Mwabukusi walipata nafasi ya kuwasilisha masuala mbalimbali yenye changamoto za upatikanaji haki.

Baada ya kusikiliza hoja za Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  walitoa ufafanuzi na kueleza changamoto za kiutendaji  zilizopo katika utekelezaji wa majukumu ya Mawakili binafsi  ambapo walikubaliana kwa pamoja kuangalia namna bora ya kushirikiana ili kuwezesha upatikanaji wa haki.

 Akizungumza katika kikao hicho Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Wakili Bonifasi Mwabukusi aliishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ukaribisho ambapo alitumia nafasi hiyo kutoa mapendekezo mbalimbali ya  namna  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na TLS wanavyoweza kushirikiana. 

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alisema kikao  kilichofanyika kimekuwa na manufaa makubwa na akaeleza kuwa maoni na mapendekezo yaliyotolewa kwa upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yamepokelwa na yatayafanyia kazi. Pia alisihi kila mmoja kuwa makini sana wanaposhughulikia masuala ya upatikanaji wa haki kwa jamii kwa kuwa Mawakili  nao ni sehemu ya jamii.

“Maoni na mapendekezo mliyowasilisha kwa upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tumeyapokea na tutayafanyia kazi, yale yaliyowasilishwa lakini yanawahusu wadau wetu tutayafikisha, yale ambayo yanatekelezwa kwa ushirikiano na taasisi nyingine za haki jinai tutayafikisha na kwa pamoja kuangalia namna bora ya kuyafanyia kazi." Alisema Mkurugenzi wa Mashtaka 

Akichangia maoni katika kikao hicho, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo aliwataka Mawakili wanaposhughulikia masuala ya Haki Jinai au kutetea wateja wao  kuzingatia  ukweli na kuwa na dhamira ya dhati ya kuisaidia Mahakama kuamua kwa haki na sio kujali suala la mteja kushinda kesi pekee  ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka na mara zote kukumbuka kwamba nao ni sehemu ya jamii.

Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika  Bi. Laetitia Ntagazwa  aliipongeza  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kazi nzuri inazozifanya katika utekelezaji wa majukumu yake.

Akitoa maoni katika kikao hicho Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Bi.  Mariam Othman aliishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ushirikiano inaoutoa kwa kuwaruhusu Mawakili wa Serikali kushikiriki katika kazi za TLS hususani Mkutano Mkuu wa TLS na pia alitumia nafasi hiyo kuiomba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwawezesha Mawakili wa Serikali kushiriki katika mafunzo maalum yanayoandaliwa na TLS ili kuwajengea Mawakili weledi na kuboresha ubora wa utendaji kazi.



Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika na Wajumbe wa Menejimenti wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakimsikiliza Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu wakati akizungumza katika kikao kilichohusisha wajumbe hao  kilichofanyika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 19 Septemba 2024.


Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Wakili Boniface Mwabukusi akizungumza katika kikao kati ya Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika na  Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa utendaji kazi iliyofanyika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 19 Septemba 2024.


Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bi. Bibiana Kileo akizungumza wakati wa kikao kati ya Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika na Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakati wa ziara  ya Baraza hilo kutembelea  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa lengo la kuboresha ushirikiano iliyofanyika Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Jijini Dodoma tarehe 19 Septemba, 2024.


Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Wakili Boniface Mwabukusi (katikati), Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu ( wa pili kushoto)na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bi. Bibiana Kileo (wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika  baada ya kumaliza ziara ya kutembelea  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iliyofanyika tarehe 19 Septemba, 2024 Jijini Dodoma.


Share:

"Zaidi ya asilimia 90 ya makosa ya jinai yanayofanyika nyuma yake kuna msukumo wa kupata kipato." Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)

 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amesema yapo makosa machache ambayo wakiamua kuyachunguza hayahusiani na kipato au fedha lakini asilimia 90 ya makosa mengi nyuma yake kuna msukumo wa kujipatia fedha.

"Tumekuwa tukipeleleza na kuendesha mashtaka kwa makosa husika tu lakini tumekuwa hatutafuti fedha ambazo zimekuwa na ushawishi mkubwa wa kufanya uhalifu huo." Mkurugenzi Mwakitalu amebainisha hayo wakati akifungua  Mafunzo kwa Wapelelezi na Wachunguzi yahusuyo Makosa ya Uhalifu wa Kifedha yaliofanyika tarehe 2 Septemba, 2024 Jijini Dar es salaam.

Sambamba na hilo DPP amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwao kwasababu yatawasaidia kudhibiti eneo hilo na kukatisha tamaa ya wahalifu wengi na kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa.

"Tulikuwa na wabobezi wachache sana katika maeneo haya ambao unaweza kuwataja kwa majina lakini kwa kutengeneza timu hii ya wabobezi 25 kwa kuanzia, tunaamini sasa tunaweza kukabiliana na uhalifu huu kwa kiasi kikubwa." Amefafanua hayo Mkurugenzi wa Mashtaka Mwakitalu. 

Aidha, DPP amewataka washiriki hao kuwekeza nguvu na akili katika mafunzo hayo ili waweze kukipata kile walichokikusudia.

"Tunawategemea kama taifa kwa kiasi kikubwa sana na tunaamini baada ya kutoka hapa tutapata kundi lingine kubwa la wakufunzi ambao wataenda kuhamisha ujuzi huu kwa watendaji wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki mahali hapa." Amebainisha hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bibiana Kileo ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuongeza utaalamu zaidi wa kuchunguza na kupeleleza juu ya makosa ya uhalifu wa kifedha.

 Naibu Mkurugenzi amefafanua kuwa washiriki wa mafunzo hayo wamegawanyika katika makundi matatu ambao kundi la kwanza na la pili ni Wapelelezi na Wachunguzi ambao wapo katika Kituo Jumuishi kinachoshughulika na Uhalifu wa Kifedha Tanzania Bara (ECC) na Zanzibar (ZECC) na kundi la tatu ni wajumbe wachache ambao hawafanyi kazi moja kwa moja na Kituo Jumuishi kinachohusika na Makosa ya Uhalifu wa kifedha (ECC).

Aidha Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amewataka washiriki wote waliopata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo kuweka umakini zaidi kwani matarajio yao makubwa katika mafunzo hayo sio tu kulenga kusaidia taasisi za Haki Jinai bali kuleta tija kwa taifa lote na kupeleka ujumbe ndani na nje ya nchi kwamba uhalifu haulipi.



Share:

Labels

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .