• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

"Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iwe ni Ofisi ya mfano katika kusimamia haki”– DPP

 Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ina  dhamira ya dhati ya kuona kuwa inakuwa mfano katika kusimamia haki kwa kujenga imani kwa wananchi na jamii nzima kwa ujumla.

“Tujenge imani kwa jamii na kwa wananchi, jambo la mwananchi likiwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka haitaji kutoa chochote bali aamini kwamba haki itatendeka, jambo hili litafanikiwa kama ninyi mnaoamua kushtaki ama kutokushtaki mtatenda kwa haki na kutokukubali kutumika iwe kwa maslahi binafsi ama ya watu wengine”.

Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akifungua Kikao kazi na Mafunzo ya Nadharia na Vitendo kwa Wakuu wa Mashtaka wa Wilaya na Waendesha Mashtaka Viongozi yanayofanyika tarehe 17 hadi 21 Desemba, 2024 Mkoani Pwani.

Amesema, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imepewa jukumu kubwa na nyeti linalogusa haki za watu kwa kuwa wao  wanahusika na kutoa maamuzi ya kushtaki na wakati mwingine maamuzi ya kutokushtaki na hayo yote yanagusa haki za watu, na kwasababu hiyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi wa hali ya juu na kwa uaminifu.

“Niwapongeze kwa kuwa mnajitahidi kutekeleza majukumu haya kwa uaminifu. Pamoja na kutekeleza majukumu hayo zipo changamoto kidogo katika utendaji wetu wa kazi ambazo zinapelekea kutotimiza wajibu wetu kwa kiwango kinachotakiwa.” Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka ameeleza kuwa timu ya Menejimenti imeweka mikakati mingi itakayowezesha kutatua changamoto hizo. Moja ya mkakati iliyowekwa ni kujenga uwezo wa watumishi kupitia mafunzo ya muda mfupi, mafunzo ya vitendo na mafunzo ya muda mrefu ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu na kuweza kuwahudumia wananchi ambao wanaangukia kwenye eneo lao husika la kimashtaka.

Amesema, mojawapo ya mikakati inayotekelezwa ni pamoja na kuwapa mafunzo Wakuu wa Mashtaka Wilaya na Waendesha Mashataka Viongozi kwa kuwa ndio nguzo muhimu kwenye utekelezaji wa majukumu hayo.

“Waendesha Mashataka Viongozi na Wakuu wa Mashtaka wa Wilaya ndio nguzo yetu, tunawategemea kwa kiasi kikubwa sana katika kuwahudumia wananchi kwenye eneo la kimashtaka. Ikiwa kama Ofisi matumaini na matarajio yetu makubwa kabisa yapo kwenu, hivyo niwaombe mfahamu na mlitambue hilo.” Amebainisha hayo Mkurugenzi Mwakitalu

Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Mashtaka amewataka washiriki hao kuhakikisha wanaweka taarifa sahihi kwenye mfumo kila siku.

“Tumetumia gharama kubwa kuuandaa mfumo huu na kuuweka kwenye mwonekano mzuri unaoeleweka kwa urahisi, ni kwasababu tunataka mfumo huu utusaidie kupata taarifa na takwimu mbalimbali zitakazo tusaidia katika kufanya maamuzi.”

Aidha, amewataka washiriki kuongeza ushirikiano na wadau wa Haki Jinai ili kupata matokeo chanya katika uendeshaji wa mashauri ya Jinai.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amesema mafunzo hayo ni ya kipekee na ya muhimu kwani yamebeba nadharia na vitendo na pia yamelenga kusaidia kuwaongezea ujuzi katika utendaji wao kazi na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kushtaki.

"Tupo hapa kwa lengo la kupata mafunzo yaliyobeba nadharia na vitendo ili  kukumbushana baadhi ya mambo ya muhimu sana kwenye uratibu na usimamizi wa upelelezi pamoja na uendeshaji wa mashtaka ambalo ndio jukumu kubwa tulilokasimiwa na Katiba ya nchi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan." Amebainisha hayo Naibu DPP

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi amewataka washiriki hao kwenda kutoa elimu kwa watumishi ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo.

“Tunataka mashauri yaweze kushughulikiwa kwa wakati na ushindi wa kesi uongezeke kwa kufuata misingi ya haki.” Amesema Mkurugenzi Ntobbi.




Share:

NAIBU MKURUGENZI WA MASHTAKA AZITAKA KAMATI ZA UJENZI WILAYANI KUSIMAMIA KIKAMILIFU NA KWA UZALENDO MIRADI YA UJENZI

 Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewataka wajumbe wa Kamati za Utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi na kamati za Ukaguzi na Mapokezi kwenda kusimamia kikamilifu miradi ya ujenzi ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kutumia vizuri mfumo wa matumizi ya rasilimali za ndani (Force Account) ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akifungua Kikao kazi na Mafunzo ya namna bora ya kutekeleza miradi ya ujenzi kwa kutumia mfumo wa matumizi ya rasilimali za ndani (Force Account) kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Mashtaka za Wilaya 24 kilichofanyika tarehe 7 Desemba, 2024 Jijini Dodoma.

Kikao hicho kimehusisha Wajumbe wa Kamati za  Ujenzi na Kamati za Ukaguzi na Mapokezi kutoka Wilaya 24, Kamati ya Uratibu wa Ujenzi Makao Makuu, Washiriki kutoka baadhi ya Divisheni na Vitengo, na Wataalamu kutoka Wakala wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Wizara ya Fedha.

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka alieleza lengo la kikao kazi hicho ni kujadiliana kwa pamoja na kupata mafunzo na miongozo ya namna bora ya   kusimamia miradi ya ujenzi wa Ofisi za  mikoa mitatu (3) na Wilaya 24 ambayo Ofisi imepanga kuanza kutekeleza katika mwaka huu wa fedha.

"Kwa Mwaka wa fedha 2024/2025, tumepanga  kujenga Ofisi za Wilaya 24 kwa kutumia Mfumo wa matumizi ya rasilimali za ndani (Force account). Ofisi ilifikia uamuzi wa kutumia njia hii ili kupunguza gharama na kuwezesha kujenga ofisi nyingi zaidi hivyo, tumekusanyika ili kupata mafunzo ya Sheria, Kanuni  na miongozo inayosimamia utaratibu wa ujenzi kwa njia hii lakini pia kufanya kikazi kazi kwa nia ya kupata uelewa wa pamoja ili kufanikisha lengo hili".

Aidha alifafanua kuwa Ofisi imedhamiria kwa dhati kutekeleza miradi ya ujenzi katika  Mikoa na Wilaya. Aliongeza kuwa ni mkakati wa Ofisi kuendelea kuanzisha ofisi mpya na wakati huo huo kuendelea kujenga majengo ya ofisi ili kufanya kazi kwenye mazingira mazuri yatakayosaidia utoaji wa huduma bora.

"Tunawategemea sana kwenda kusimamia ujenzi wa Ofisi zetu za wilaya kwa kutumia kiasi cha pesa ambacho kimetengwa. Ni jukumu ambalo tumewapa na kuwaamini sana na pia ni jukumu ambalo litahitaji moyo wa uzalendo sana, tutambue ya kuwa fedha hiyo ni fedha ya serikali, fedha ya walipa kodi, na tumeamua kutumia njia hii ili tuweze kujenga ofisi nyingi, zenye ubora na kwa gharama nafuu, alisisitiza Naibu Mkurugenzi Bibiana.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi aliwataka washiriki hao kwenda kusimamia kwa weledi mkubwa shughuli za ujenzi wa majengo ya Ofisi ya wilaya pasipo udanganyifu wa aina yoyote na wasimamie ujenzi kama wanavyosimamia mali zao binafsi kwa sababu ni fedha hizo ni mali ya  Umma.

Kwa upande mwingine wataalamu kutoka Wakala wa Ununuzi wa Umma na Wizara ya Fedha walielimisha masuala mbalimbali kuhusu mfumo wa ujenzi kwa kutumia mfumo wa matumizi ya rasilimali za ndani ambapo washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali.




Share:

"Ninyi ni watu muhimu na wathamani sana katika taasisi yetu." Naibu DPP

 Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amesema wajumbe  wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  ni watu muhimu na wathamani sana katika taasisi kwani kupitia maoni yao wanayowasilisha wanapelekea viongozi kuunga mkono juhudi za TUGHE katika kupambana na  kuhakikisha watumishi wote wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wanapata stahiki zao pasipo kubagua kada yoyote ile.

"Dhamira yetu ya dhati ni kuhakikisha tunajenga umoja wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili tuweze kutimiza wajibu wetu vizuri na kuleta matokeo chanya kwa nchi, Taasisi na wananchi, na kuona Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inatenda  haki katika kusimamia na kuendesha mashtaka Nchini"

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano wa  TUGHE Tawi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka uliofanyika tarehe 6 Desemba, 2024  Jijini Dodoma.

Sambamba na hilo Naibu  Mkurugenzi wa Mashtaka amesema matamanio ya viongozi ni kuona Ofisi yetu inatimiza jukumu lake kubwa la kikatiba chini ya Ibara 59B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano  ambalo ni kusimamia na kuendesha mashauri yote ya jinai nchini  kwa kuzingatia misingi ya haki, pasipo kuonea wala  kumpendelea mtu wa aina yoyote, pamoja na majukumu mengine ambayo wamekabidhiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, amewataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuwa na nidhamu mahala pa kazi na kuwa wazalendo katika nchi yao pamoja na taasisi, kutumia vizuri rasilimali walizopewa.

Pia amewataka wajumbe hao  mara watakaporejea katika vituo vyao vya kazi kwenda kukusanya maoni na mrejesho kutoka kwa watumishi wenzao kwa masuala ambayo wanaona yakifanyika yatasaidia zaidi katika kuboresha utendaji kazi wa taasisi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kueleza changamoto wanazokabiliana nazo.

"Tusingependa kuona kuna manun'guniko au mgawanyiko hata kidogo, nia yetu na dhamira yetu ya dhati tufanye kazi katika upendo, umoja na mshikamano ili tuweze kufikia maono ya taasisi yetu." Amefafanua hayo Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi amewataka Viongozi wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kutoa elimu kwa watumishi ambao wanasifa ya kujiunga na TUGHE lakini bado hawajajiunga na chama hicho.

"Idadi ya wanachama wa TUGHE 131 bado ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watumishi waliopo katika taasisi hii, tuendelee kuhamasishana ili kujiunga na chama chetu hiki ili tuweze kutimiza malengo." Amefafanua hayo Mkurugenzi Ntobbi

Naye Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Maulidi Kipeneku ametoa pongezi kwa uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wanachama wa TUGHE na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wao ili kukuza chama hicho.




Share:

MKURUGENZI MSAIDIZI MKEMWA AHITIMISHA KIKAO KAZI CHA MAAFISA VIUNGANISHI

 Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Udanganyifu na Utakasishaji Fedha Bw. Seth Mkemwa  amehitimisha Kikao Kazi cha Maafisa Viunganishi (Focal persons) wa Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili kilichofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Novemba, 2024 mkoani Morogoro.

"Katika hizi siku tatu kulikuwa na zoezi kubwa la kuchakata takwimu zinazohusiana na makosa ya Mazingira na Maliasili ambapo uchakataji wa takwimu hizi umekwenda sambamba na kubainisha changamoto, mafanikio na pia kuangalia namna ya kutafutia ufumbuzi changamoto husika”. Amebainisha hayo Bw. Mkemwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili Bw. Salimu Msemo amewapongeza Maafisa Viunganishi kwa juhudi na ushirikiano wa hali ya juu waliouonyesha katika kikao kazi hicho ikiwa ni zaidi ya vile ilivyotarajiwa.

Aidha amewataka washiriki hao kwenda kuwa watumishi wa mfano kwenye kila eneo linalohusisha majukumu yao ikiwa ni pamoja na kufuata miongozo na maelekezo yote yanayotolewa na viongozi pamoja na kuzingatia maazimio yote waliyokubaliana katika kikao kazi.

"Tutakuwa tunafanya ufuatiliaji wa hiki ambacho tumekubaliana kupitia maazimio ya kikao hiki pamoja na masuala mengine yanayohusu makosa ya Mazingira na Maliasili." Amefafanua hayo Kaimu Mkurugenzi Msemo.

Naye, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro Bi. Tarsila Gervas amewashukuru viongozi kwa kuwakutanisha Maafisa Viunganishi ili kuweza kujadili mustakabali mpana wa namna ya kupata taarifa zinazolisha taasisi katika masuala mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Bi. Neema Moshi ambae ni Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam, ameushukuru uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na wadau kwa kuwawezesha kushiriki kikao kazi hicho kwani  wamejifunza mengi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu makosa ya Mazingira na Maliasili na kuahidi kwenda kutekeleza yale yote waliyokubaliana kupitia kikao hicho.




Share:

KAIMU MKURUGENZI MSIGWA ASISITIZA JUU YA UMUHIMU WA UTOAJI WA TAARIFA SAHIHI.

 Kaimu Mkurugenzi Divisheni ya Makosa ya Udanganyifu na Utakasishaji Fedha Bw. Christopher Msigwa amesisitiza juu ya umuhimu wa utoaji wa taarifa zilizo sahihi ambazo zitasaidia katika suala zima la takwimu.

Kaimu Mkurugenzi Msigwa ameyasema hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Viunganishi (focal persons) wa Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili kinachofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Novemba, 2024 mkoani Morogoro.

Kikao Kazi hicho kinajumusha Maafisa Viunganishi kutoka Mikoa 30 ya Kimashtaka pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Kikosi Kazi cha Taifa cha Kupambana na Ujangili (NTAP), Kikosi Kazi cha Taifa cha Kupambana na Makosa ya Madini na Kituo cha Kupambana na Uhalifu wa Kifedha na Uhujumu Uchumi (ECC). 

Aidha Kaimu Mkurugenzi Msigwa amesema taarifa wanazozihitaji katika Kikao Kazi hicho kutoka kwa Maafisa Viunganishi hao ni muhimu sana kwao kama Idara na kwa ajili ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ujumla.

Pia  amebainisha kuwa lengo la  taarifa hizo ni pamoja na kuwasaidia katika masuala mbalimbali ikiwemo kujua aina ya mafunzo wanayopaswa kuyatoa  kama yale yanayohusu  uratibu wa upelelezi na uendeshaji wa mashtaka yenye viashiria vya mazalia ya uhalifu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili Bw. Salimu Msemo ameeleza Kikao Kazi hicho kinalenga  kuwakutanisha Maafisa Viungo wa Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili ili kuwajengea uelewa wa pamoja kwa mujibu wa sheria na miongozo.

Aidha, aliongeza kuwa, lengo jingine ni kuandaa Taarifa ya Taifa ya Takwimu zinazohusiana na Makosa ya Mazingira na Maliasili, 

"Jambo lolote la msingi haliwezi kufanyika bila kuwa na takwimu sahihi, ambapo washiriki hawa walianza kulifanyia kazi eneo hili la ukusanyaji wa taarifa kabla ya kuja kushiriki kwenye Kikao Kazi hiki." Amesema Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Msemo.



Alieleza zaidi kuwa, lengo jinginei kupata maoni kuhusiana na Mpango Mkakati wa Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili ambao upo katika hatua za awali.

Aidha, Kikao Kazi hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Divisheni ya Utaifishaji Mali, Makosa yanayovuka Mipaka na Uhalifu Mahsusi Bw. Faraja Nchimbi, Mkurugenzi Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Javelin Rugaihuruza, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Usimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi Bw. Saraji Iboru, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Rushwa Bw. Zakaria  Ndaskoi na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Udanganyifu na Utakasishaji Fedha Bw. Seth Mkemwa ambao kwa pamoja walisisitiza masuala mbalimbali yakiwemo;

1. Maafisa Viunganishi kutimiza wajibu wao na kutekeleza majukumu yao kama walivyoelekezwa ili kuleta tija katika utendaji wa Idara na Taasisi kwa ujumla;

2. ⁠Kuhakikisha wanazingatia matumizi ya mfumo wa sasa na baadaye mfumo ulioboreshwa ili kuboresha upatikanaji wa taarifa na kuimarisha upatikanaji wa matokeo chanya katika uendeshaji wa mashauri mahakamani; na

3. ⁠Kuwashirikisha Maafisa Viunganishi wa Idara nyingine na watumishi wengine kwa ujumla katika Mikoa yao masuala muhimu watakayojifunza kutoka kwenye Kikao Kazi hiki.




Share:

WATENDAJI WA SERIKALI WAJENGEWA UWEZO JUU YA MIKATABA YA HAKI ZA BINADAMU

 Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Jumuiya ya Madola na Ofisi ya Balozi Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Kanda ya Afrika Mashariki imeandaa mafunzo kwa Maafisa wa Serikali juu ya uwasilishaji wa ripoti za utekelezaji wa Mikataba ya Haki za Binadamu ambayo Serikali imeridhia ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu. 

Akizungumza leo tarehe 28 Novemba, 2024  wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu  yanayofanyika katika Hoteli ya Morena mjini Morogoro, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Mazingira na Maliasili Salimu Msemo akimwakilisha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini amesema kuwa  ni vyema Wataalamu hao kutumia mafunzo hayo ili kuongeza ujuzi katika kuandaa na kutoa taarifa muhimu juu ya Mikataba ya Haki za Binadamu na Wajibu wa Serikali nchini ya kila kifungu. 

"Kama watumishi wa Umma, nawakumbusha kuwa wasikivu ili lengo la Serikali la kuongeza  uwezo wenu katika kutekeleza majukumu yenu litimie.Tunahitaji muwasilishe taarifa ili kuweza kukamilisha ripoti ya juhudi za Serikali za kukuza na kulinda haki za watu wenye ulemavu."Alisema Salimu 

Sambamba na hilo Salimu   amesema kuwa  katika utekelezaji wa Mikataba  Serikali inatakiwa kutoa taarifa ya namna ilivyotekeleza Mikataba hiyo kwa kuchukua hatua za Kisera,Kikanuni, Kitaasisi na Kiutawala.

Kwa upande wake Mshauri wa Haki za Binadamu kutoka Ofisi ndogo za Umoja huo zilizopo  Geneva, Yashasvi Nain amesema Tanzania inatekeleza mikataba sita kati ya tisa ya msingi ya Kimataifa ya Haki za Binadamu hivyo Serikali ina wajibu wa kufuatilia na kutoa taarifa za mara kwa mara kwa vyombo husika vya mkataba kuhusu jinsi ahadi hizi za kimataifa zinavyotafsiriwa katika hatua na utekelezaji wa kitaifa na inahitaji rasilimali kubwa, pamoja na uwezo wa kibinadamu na kiufundi. 

Rai imetolewa kwa  Wizara na Taasisi zinazohusika kuendelea kutoa ushirikiano ili kuipatia Wizara ya Katiba na Sheria Sera, Sheria, Programu na takwimu kutoka Ofisi zinazohusika ili kuepuka kuwa na ripoti zisizo na ubora

Share:

Labels

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .