Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amesema wajumbe wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni watu muhimu na wathamani sana katika taasisi kwani kupitia maoni yao wanayowasilisha wanapelekea viongozi kuunga mkono juhudi za TUGHE katika kupambana na kuhakikisha watumishi wote wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wanapata stahiki zao pasipo kubagua kada yoyote ile.
"Dhamira yetu ya dhati ni kuhakikisha tunajenga umoja wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili tuweze kutimiza wajibu wetu vizuri na kuleta matokeo chanya kwa nchi, Taasisi na wananchi, na kuona Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inatenda haki katika kusimamia na kuendesha mashtaka Nchini"
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka uliofanyika tarehe 6 Desemba, 2024 Jijini Dodoma.
Sambamba na hilo Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka amesema matamanio ya viongozi ni kuona Ofisi yetu inatimiza jukumu lake kubwa la kikatiba chini ya Ibara 59B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambalo ni kusimamia na kuendesha mashauri yote ya jinai nchini kwa kuzingatia misingi ya haki, pasipo kuonea wala kumpendelea mtu wa aina yoyote, pamoja na majukumu mengine ambayo wamekabidhiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amewataka watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuwa na nidhamu mahala pa kazi na kuwa wazalendo katika nchi yao pamoja na taasisi, kutumia vizuri rasilimali walizopewa.
Pia amewataka wajumbe hao mara watakaporejea katika vituo vyao vya kazi kwenda kukusanya maoni na mrejesho kutoka kwa watumishi wenzao kwa masuala ambayo wanaona yakifanyika yatasaidia zaidi katika kuboresha utendaji kazi wa taasisi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kueleza changamoto wanazokabiliana nazo.
"Tusingependa kuona kuna manun'guniko au mgawanyiko hata kidogo, nia yetu na dhamira yetu ya dhati tufanye kazi katika upendo, umoja na mshikamano ili tuweze kufikia maono ya taasisi yetu." Amefafanua hayo Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi amewataka Viongozi wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kutoa elimu kwa watumishi ambao wanasifa ya kujiunga na TUGHE lakini bado hawajajiunga na chama hicho.
"Idadi ya wanachama wa TUGHE 131 bado ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watumishi waliopo katika taasisi hii, tuendelee kuhamasishana ili kujiunga na chama chetu hiki ili tuweze kutimiza malengo." Amefafanua hayo Mkurugenzi Ntobbi
Naye Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Maulidi Kipeneku ametoa pongezi kwa uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wanachama wa TUGHE na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wao ili kukuza chama hicho.






No comments:
Post a Comment