• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

ALIYEMUUA MKEWE KISHA KUMCHOMA KWA MAGUNIA YA MKAA AHUKUMIWA KUNYONGWA


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam imemhukumu mfanyabiashara Bw. Hamis Said Luwongo mwenye umri wa miaka 38 kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa aliyejulikana kwa jina la Bi. Naomi Marijani kisha kuchoma mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 26 Februari, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Hamidu Mwanga, baada ya kuridhishwa na ushahidi wa  mashahidi 14 na vielelezo 10 kutoka upande wa Mashtaka.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, jopo la Mawakili wa Serikali wawili likiongozwa na Wakili wa  Serikali Mkuu Bi. Yasinta Peter akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Bi. Ashura Mnzava, waliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa wale wanaofanya ukatili dhidi ya wanawake wanaume wote wanaowafanyia ukatili wanawake wao kwa kigezo kuwa wapo kwenye ndoa.

"Kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha ukatili na kinaleta mashaka kwa wanawake waliopo katika ndoa na wanawake wanaoingia katika ndoa, hivyo tunaomba Mahakama yako itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wanaume wanaotumia kigezo cha ndoa kufanya ukatili kwa wake zao.” Amesema Wakili Mnzava.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 44/2023, Bw. Hamis Luwongo ambaye ni mkazi wa Gezaulole, Wilayani Kigamboni, Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia ya mkewe Naomi  kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 15 Mei, 2019 nyumbani kwao, kisha akauchoma mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku ambapo inadaiwa masalia ya mwili na majivu aliyachukua akaenda kuyazika shambani na kupanda migomba juu yake kwa lengo la kuficha ushahidi.

Share:

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWANOA MAAFISA VIUNGO JUU YA NAMNA YA KUSHUGHULIKIA MAKOSA DHIDI YA BINADAMU NA MAKOSA YATAKAYOJITOKEZA KATIKA KIPINDI CHA UCHAGUZI

 Mkurugenzi wa Mashtaka  Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kushughulikia makosa dhidi ya binadamu na yatakayojitokeza katika kipindi cha Uchaguzi mkuu ili kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa Taifa na  kuhakikisha wale wote wanaovunja sheria wanashughulika nao ipasavyo kwa kufuata taratibu na sheria za makosa ya jinai.

Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akifungua Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwasababu yatawakwamua katika changamoto kadhaa zinazofanya utendaji kazi wao ukwame mahali fulani na kupelekea kutokupata matokeo wanayoyatarajia.  

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mwakitalu ameipongeza Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kwa kuanzisha na kuwaita Maafisa Viungo wanaoiwakilisha  idara hiyo katika kila mkoa kwa lengo la kuwapa mafunzo.

“Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi  inasimamia asilimia kubwa ya kesi tunazoshughulika nazo huko mikoani zikiwepo kesi za Ukatili wa Kijinsia kwa maana ya Ubakaji, Ulawiti idadi yake ni kubwa sana katika Mahakama zetu, na zilizofika mahakamani ni kidogo sana ukilinganisha na matukio yanayotokea, na yale yanayoripotiwa katika Vituo vya Polisi na hayafiki asilimia 20. 

Tunayo makosa yanayogusa mali yakiwepo wizi, unyang'anyi kwa kutumia silaha, makosa haya yote yanaangukia katika idara hiyo na pia ndio makosa mengi ambayo yanafanyika kwenye jamii zetu.” Amesema Mkurugenzi Mwakitalu.

Pia Mkurugenzi wa Mashtaka amesema kupitia mafunzo hayo wanatarajia kwenda kuongeza ubora wa uratibu katika Upelelezi na Uendeshaji wa Mashtaka

“Tunategemea kuona uboreshaji zaidi juu ya namna tunavyoshughulikia Uratibu wa Upelelezi wa Makosa haya pamoja uendeshaji wake mahakamani.”

Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka amewataka Maafisa Viungo hao kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kuyafahamu majukumu ya idara husika kwa ukamilifu ili kuleta mabadiliko juu ya namna ambavyo wanashughulikia makosa hayo yanayoangukia kwenye idara husika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kila baada ya mwezi mmoja ya namna wanavyotekeleza majukumu  katika mikoa yao.

Katika kuelekea kwenye kipindi cha Uchaguzi mkuu unaotarajia  kufanyika Mwezi Oktoba mwaka 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka amesema  kipindi hicho kinakuwa na mambo mengi, wananchi wana haki na wajibu wao kwenye shughuli za uchaguzi lakini wapo wale wanaopitiliza mipaka na kuvunja Sheria na kutenda makosa ya jinai,   hivyo maafisa viungo hao wanalo jukumu la kusimamia hilo Ili kudumisha amani nchini.

‘’Mtapitishwa kwenye makosa yanayohusiana na kipindi hicho na namna ambavyo tunaweza kuyashughulikia. Tunataka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tufanye kazi yetu kwa weledi hata katika kipindi hicho cha kampeni, kipindi cha maandalizi ya uchaguzi na hata baada ya matokeo ya uchaguzi, tuhakikishe tunatimiza wajibu wetu kwa Taifa, katika kuhakikisha wale wanaovunja sheria tunashughulika nao ipasavyo. Na pia pale ambapo tunaweza tukashauri makosa hayo yasifanyike basi hatuna budi kufanya hivyo.” Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Javelin Rugaihuruza amesema kupitia mafunzo hayo Maafisa Viungo watapitishwa kwenye mada mbalimbali kuhusiana na majukumu ya idara hiyo  ambayo wanatakiwa kufanya ili kusaidia kuweza kutekeleza majukumu yao kama idara pamoja na mambo mengine. 

Aidha, watapata nafasi ya kupitishwa kwenye Ushughulikiaji wa makosa ya Ukatili wa Kijinsia.

Kama tunavyofahamu makosa ambayo yanaongoza mahakamani ni makosa ya Ukatili wa Kijinsia, tumeona tuitumie nafasi hii kuwapitisha katika  mada hiyo ili tuweze kuona ni jinsi gani makosa hayo yanaweza kushughulikiwa na changamoto zilizopo katika makosa hayo ili kuweza kuepukana na Changamoto hizo kama sio kuzipunguza basi kuziondoa kabisa.


Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu  akifungua Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Javelin Rugaihuruza akimkaribisha Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu kufungua Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika  katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025.


Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Pendo Makondo akiwasilisha mada inayohusu Uelewa juu ya Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi na majukumu ya Maafisa Viungo kwenye Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025.


Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025

Share:

DPP AWATAKA WAAJIRIWA WAPYA KWENDA KUFANYA KAZI KWA WELEDI, UADILIFU NA UZALENDO

 

Mkurugenzi wa Mashtaka  Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka watumishi wapya walioajiriwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambao ni Mawakili wa Serikali na Makatibu Sheria kwenda kufanya kazi kwa  weledi, umakini, uadilifu na uaminifu pamoja na kuzingatia Sheria, Kanuni na Misingi ya Utumishi ya Umma ili kuifanya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kuwa Taasisi yenye  misingi bora na ya mstari wa mbele katika kusimamia haki.

“Kufanya kazi kama Wakili wa Serikali ni heshima kubwa sana hivyo naomba muilinde heshima hiyo kwani kazi yetu inahitaji umakini, weledi, uadilifu na uaminifu, tunataka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iendelee kuwa mstari wa mbele kwenye kusimamia haki za watu na hili tunalitegemea kutoka kwenu.’’

Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo tarehe 5 Februari, 2025 wakati akizungumza na watumishi waajiriwa wapya waliofika Makao Makuu, Dodoma kwa ajili ya kuchukua barua zao za kwenda kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.

Mkurugenzi Mwakitalu alisema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni ofisi ambayo imebeba haki za watu mkononi na kwamba maamuzi watakayoenda kufanya waajiriwa hao wapya ya kushtaki ama kutokushtaki ni maamuzi ambayo moja kwa moja yanagusa haki za watu, hivyo aliwaasa kuwa wanapaswa kuwa makini katika kila hatua wanayoifanya na kuhakikisha wanajiandaa vizuri kabla ya kwenda mahakamani ili kuisaidia mahakama kufanya maamuzi yaliyosahihi katika utoaji haki.

Aidha, amewataka pia waajiriwa wapya hao kutenga muda kupitia miongozo mbalimbali ambayo imewekwa katika tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambayo itawasaidia  kujifunza na kuongeza uzoefu katika utendaji kazi wao wa kila siku.

”Uzoefu mlioupata huko kabla hamjaja hapa uleteni, kama kuna kitu kinaweza kutusaidia  kuboresha utoaji wetu  huduma kwa wananchi leteni na sisi tutakuwa tayari kupokea na kufanyia kazi kama kitaleta tija kwenye kazi zetu.”, Aliongea Mkurugenzi Mwakitalu

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewapongeza waajiriwa wapya  kwa kupata nafasi ya kuingia katika Utumishi wa Umma  na pia kupata bahati ya kuungana na familia ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka hivyo na kuwataka kwenda kuzingatia yale yote watakayoelekezwa wakati wakiwa kazini.

‘’Mkizingatia yale yote mtakayoelezwa na viongozi wenu itawaletea mafanikio makubwa sana kwenye safari yenu ya utumishi na kukuwa katika taaluma yenu.’’ Alisema Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bw. Simon Ntobbi amewaasa waajiriwa wapya hao kuwa na hofu ya Mungu ili waweze kutenda haki kwa wananchi watakaokwenda kuwahudumia.

‘’ Tunashukuru kwa kupata nguvu mpya hivyo mkiwa kama Mawakili tunawategemea mkatende haki, mkawasaidie wananchi wa hali ya chini naya juu kwa kutenda haki." Aliyasema hayo Mkurugenzi wa Utawala.

Katika hatua nyingine, watumishi hao wapya walipata pia fursa ya kuelekezwa Masuala mbalimbali ikiwemo miongozo na elimu kuhusa Afya Mahali Pa Kazi na uepukaji wa vitendo vya Rushwa ambapo walijaza fomu za Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu pamoja na kujifunza kuhusu Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma, wasilisho lililotolewa na Afisa Tawala Mkuu, Ndugu Juma S. Katanga.


Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu  akizungumza na watumishi waajiriwa wapya waliofika Makao Makuu, Dodoma kwa ajili ya kuchukua barua zao za kwenda kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.



Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo akimkaribisha Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu kuzungumza na Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mara baada ya kuwasili Makao Makuu Jijini Dodoma kwa lengo la kuchukua barua zao na kwenda kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa.




Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Simon Ntobbi  akizungumza na Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mara baada ya kuwasili Makao Makuu Jijini Dodoma kwa lengo la kuchukua barua zao na kwenda kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa.

Share:

RAIS SAMIA AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo yalifanyika kitaifa katika viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma, mnamo tarehe 03 Februari, 2025. Hafla hiyo muhimu, ambayo huadhimishwa kila mwaka, imekusanya viongozi mbalimbali wa kitaifa, majaji, mawakili, maofisa wa serikali, na wadau wengine wa sekta ya sheria.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais alisisitiza umuhimu wa mfumo wa sheria imara katika maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa utawala wa sheria ni msingi wa haki, amani, na maendeleo endelevu. Aliwataka wadau wa sheria, wakiwemo mawakili na majaji, kuendelea kuwa mfano wa uadilifu na uwajibikaji katika kutoa haki kwa wakati na bila upendeleo. 

“Tunapoadhimisha siku hii ya sheria, napenda kusisitiza kuwa uwajibikaji wa vyombo vya sheria ni muhimu katika kuleta imani ya wananchi kwa serikali na taasisi za kisheria. Hatuna budi kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote kwa usawa,” alisema Rais Samia. 

Maadhimisho ya mwaka huu yalibeba kaulimbiu inayolenga kukuza ufahamu wa wananchi juu ya umuhimu wa upatikanaji wa haki kwa njia za haraka, zenye gharama nafuu na zenye kuzingatia haki za binadamu. Pia, yalihusisha shughuli mbalimbali kama maonesho ya huduma za kisheria, mijadala ya kitaalamu, na mashauriano ya bure kwa wananchi.

Aidha, Rais alitumia nafasi hiyo kupongeza juhudi za Mahakama ya Tanzania kwa maboresho ya kiteknolojia yaliyofanyika hivi karibuni, yakiwemo mfumo wa kuendesha kesi kwa njia ya mtandao (e-filing) na matumizi ya majukwaa ya kidigitali katika kupunguza mlundikano wa kesi. 

“Ni faraja kubwa kuona kwamba Mahakama yetu inaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa haki siyo tu inatendeka, bali pia inaonekana kutendeka kwa wakati unaofaa,” aliongeza Mhe. Samia. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha mifumo ya sheria na upatikanaji wa haki nchini.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Majaji, wageni waalikwa pamoja na wananchi kwa ujumla kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma tarehe 3 Februari, 2025



Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma wameshiriki Maadhimisho ya Siku ya Sheria ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma tarehe 3 Februari, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Taasisi mbalimbali walioshiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma tarehe 3 Februari, 2025

Share:

“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekuwa msaada mkubwa kwa TRA” – Mkurugenzi Shigela

 

Mkurugenzi wa Sheria kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Elisha Shigela akimwakilisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  imekuwa msaada mkubwa katika suala zima la ushughulikiaji wa mashauri yanayohusiana na ukwepaji wa kodi.

“Ukiangalia sehemu kubwa ya kodi inayokusanywa inatokana na ule ulipaji kodi wa hiari (voluntary compliance) na mara nyingi kuna watu ambao wameamua kutokulipa kodi hivyo tunaamua kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria na ndipo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inapokuja kuungana na TRA kufanya upelelezi wa kina na kugundua makosa yanayofanywa na watu husika na baada ya kukamilisha upelelezi tunawapeleka mahakamani wahusika hao na kuhakikisha kwamba tunakomesha tabia ya kutokulipa kodi”.

Mkurugenzi wa Sheria amebainisha hayo wakati alipotembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 17 Januari, 2025 akiwa ameambatana na timu yake kutoka Makao Makuu ya TRA Jijini Dar es salaam kwa lengo la  kuwashukuru wakiwa kama wadau wao katika shughuli za ukusanyaji wa kodi kwani wamekuwa msaada mkubwa sana katika masuala hayo.

Aidha, Mkurugenzi Shigela amesema wataendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na ikiwezekana kuwepo na dawati litakalowezeshwa kushughulikia makosa yanayotokana na kodi na katika hilo TRA watakuwa tayari kuandaa  programu  ambazo watawawezesha Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kupatiwa mafunzo ya pamoja.

“Ili kuweza kufanya kazi vizuri katika eneo fulani lazima uwe unalifahamu vizuri pamoja na umahiri wa kutosha, hivyo tungependa kuwahusisha katika mafunzo mbalimbali yanayofanywa na TRA ili waweze kuwa na umahiri katika kujua kodi yenyewe na kujua namna ya kuweza kushughulikia makosa yatokanayo na kodi.” Amefafanua Mkurugenzi Shigela.

Kwa upande wake Naibu Kamishna Upelelezi wa Kodi kodi Bi. Feliciana Nkane ameiomba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendeleza ushirikiano wa pamoja katika kudhibiti masuala yanayohusiana na makosa ya kodi kwa kuwapeleka watu mahakamani ili kutuma ujumbe kwa wengine ambao wanakwepa kodi ili kuweza kufahamu kwamba ukwepaji kodi ni kosa la jinai na unaweza kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Sisi sote ni Watoto wa baba mmoja na tunajenga nyumba moja hivyo tunachoomba kutoka kwenu ni ushirikiano hususani katika masuala ya Upelelezi wa makosa yanayohusiana na kodi.

Rai yangu tunahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwenu kwani ninyi ndio wataalamu zaidi katika maeneo haya na msichoke kutuongoza na kutupa miongozo mbalimbali kuhakikisha kwamba tunatengeneza kesi zilizo bora”. Amebainisha hayo Naibu Kamishna.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema ujio wa TRA  katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni muhimu sana kwasababu unawafungulia njia (platform) ya kuweza kushirikiana zaidi na pia kutafuta namna ambayo wakiamua kwenda mahakamani wanaenda wakiwa na uhakika wa kushinda mashauri kwa asilimia kubwa.

“Niwaombe kupitia platfom hii tushirikiane kuanzia tunapoliandaa jalada, tunapokusanya ushahidi na tunapokwenda mahakamani hizi timu za Wapelelezi na Waendesha Mashtaka kutoka pande zote ziwe zinashirikiana.” Amesisitiza Mkurugenzi Mwakitalu.

Mkurugenzi Mwakitalu ameishukuru pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwapatia fursa ya mafunzo kwani bila kujenga uwezo wa watendaji nafasi ya mafanikio inakuwa ndogo na hafifu. Aidha ameomba mafunzo yatakayofanyika kwa ufadhili wao,yashirikishe pia wadau wetu muhimu hasa vyombo vya upelelezi ili wanapofanya chunguzi hata za makosa mengine, wasiache pia kuchunguza makosa ya kodi yanayobainika kwa sababau tu ya kukosa maarifa ya kutosha juu ya eneo hili.





 Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu akipokea zawadi mbalimbali kutoka kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka Makao Makuu Jijini Dar es salaam wakati walipotembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 17 Januari, 2025 kwa lengo la kuwakushukuru wakiwa kama wadau wao katika shughuli za ukusanyaji kodi.



Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo akipokea zawadi ya keki kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu iliyokabidhiwa  na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka Makao Makuu Jijini Dar es salaam tarehe 17 Januari, 2025

 

 Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Sheria kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na baadhi ya Viongozi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mara baada kumaliza mazungumzo wakati walipotembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 17 Januari, 2025

Share:

Labels

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .