Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam imemhukumu
mfanyabiashara Bw. Hamis Said Luwongo mwenye umri wa miaka 38 kunyongwa hadi
kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa aliyejulikana kwa
jina la Bi. Naomi Marijani kisha kuchoma mwili wake kwa kutumia magunia mawili
ya mkaa.
Hukumu hiyo imetolewa tarehe 26 Februari, 2025 na Jaji wa
Mahakama hiyo Mhe. Hamidu Mwanga, baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi 14 na vielelezo 10 kutoka upande wa
Mashtaka.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, jopo la Mawakili wa
Serikali wawili likiongozwa na Wakili wa
Serikali Mkuu Bi. Yasinta Peter akisaidiana na Wakili wa Serikali
Mwandamizi Bi. Ashura Mnzava, waliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya
mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa wale wanaofanya ukatili dhidi ya wanawake
wanaume wote wanaowafanyia ukatili wanawake wao kwa kigezo kuwa wapo kwenye
ndoa.
"Kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha ukatili na
kinaleta mashaka kwa wanawake waliopo katika ndoa na wanawake wanaoingia katika
ndoa, hivyo tunaomba Mahakama yako itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa
wanaume wanaotumia kigezo cha ndoa kufanya ukatili kwa wake zao.” Amesema Wakili
Mnzava.
Katika kesi hiyo ya Jinai namba 44/2023, Bw. Hamis Luwongo
ambaye ni mkazi wa Gezaulole, Wilayani Kigamboni, Jijini Dar es salaam alikuwa
anakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia ya mkewe Naomi kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria
ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 15 Mei, 2019 nyumbani
kwao, kisha akauchoma mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda
la kuku ambapo inadaiwa masalia ya mwili na majivu aliyachukua akaenda kuyazika
shambani na kupanda migomba juu yake kwa lengo la kuficha ushahidi.







No comments:
Post a Comment