Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2025/2026 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Leo tarehe 30 April 2025 ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imechangia ufanisi mkubwa katika uendeshaji wa kesi za Uhujumu Uchumi kwa kipindi kati ya Julai 2024 na Aprili 2025.
Kupitia hotuba yake, Dkt. Ndumbaro amelieleza Bunge kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kipindi cha mwaka wa Fedha 2024/2025 iliendesha kesi kubwa 177 katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ukilinganisha na Kesi 60 pekee zilizoendeshwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2023/2024.
Waziri Ndumbaro pia amebainisha kuwa katika Kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, kesi za jinai 27,523 ziliendeshwa katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, tofauti na kesi 25,037 zilizoendeshwa katika Mahakama hizo kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Ameeleza zaidi kuwa, Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kusogeza huduma kwa wananchi ngazi za Mikoa na Wilaya, ambapo katika kipindi cha mwaka 2024/2025 huduma hizo zimepelekwa kwenye mikoa yote 26 nchini pamoja na Mikoa minne ya kimashtaka hivyo kufanya idadi ya mikoa 30 inayopata huduma za Kimashtaka. Sambamba na hilo Waziri Ndumbaro amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefikisha huduma za mashtaka katika Wilaya 108 nchini.
Ameongeza kusema kuwa, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekamilisha ujenzi wa majengo yake katika mikoa ya Manyara, Shinyanga, Katavi, Rukwa, Pwani na mkoa wa Kimashtaka Ilala.







No comments:
Post a Comment