Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka
Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa na Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya
kazi kwa umakini na kwa weledi ili kuweza kulinda haki na amani za Watanzania
hususani katika uendeshaji wa mashauri ya kijinai.
"Tunalo jukumu la kupambana na uhalifu, na sisi ndio
kiungo katika mapambano hayo, kwa hiyo tupambane vizuri ili Watanzania waweze
kuishi kwa amani, kwani pasipokuwa na amani wala usalama, hakuna maendeleo katika Taifa letu. Hivyo
tukiwa kama viongozi yatupasa kutekeleza Dira na Dhima iliyotolewa na Taasisi
yetu"
Ameyasema hayo Mkurugenzi wa Mashtaka wakati akifungua Kikao
kazi cha Wakuu wa Mashtaka Mikoa na Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka
kilichofanyika tarehe 12 hadi 13 Mei, 2022 katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mwakitalu alieleza kuwa katika siku hizi za
karibuni kumekuwa na ongezeko la wimbi la uhalifu katika nyanja zote. Hivyo
basi kuna jukumu kubwa la kulinda haki hususani zile ambazo zinaangukia kwenye
jinai.
DPP aliwapongeza
Wakuu wa Mashtaka Mikoa kwackufanya kazi nzuri ya kupunguza msongamano
wa mahabusu gerezani ijapokuwa bado changamoto hiyo ya msongamano haijaisha.
"Magereza yaliyomengi khali sio nzuri lakini kibaya
zaidi Mahabusu ni wengi kuliko wafungwa. Kwahiyo kupitia hili inabidi kujadili
kwa kina ili kuweza kupata suluhu ya kupunguza mlundikano mkubwa wa mashauri
yaliyopo mahakamani"
Aidha Mwakitalu alisema kuwa ni muhimu kupata taarifa za
kila siku kwani zitasaidia kupanga mipango ya maendeleo ya kiofisi. Na pia
aliendelea kueleza kuwa kwa upande wa eneo la Takwimu ni muhimu kuangaliwa kwa
umakini zaidi ili ziweze kuendana na uhalisia hususani katika eneo la Takwimu
za Mahakama za Mwanzo kwasababu zinalenga kesi za jinai. Hivyo basi ni muhimu
kuwa na taarifa zake ili kuona idadi ya kesi zilizosajiliwa, zilizoisha, na
kujua zimeishaje na faini kiasi gani. Hivyo ni eneo muhimu sana sana la
kuangaliwa na kupata ufumbuzi wake.
Naye pia Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande
alieleza kuwa lengo kuu la kufanya kikao kazi hicho ni
kufanya tathmini ya ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka, hivyo basi kikao
hicho kimepanga kutoka na maadhimio juu
ya namna gani ifanyike ili kukabiliana na ongezeko la uhalifu na pia
kutengeneza mikakati ya pamoja ya namna ya kukabiliana na kesi za jinai ili
kuweza kudumisha haki na amani katika Taifa la Tanzania.






No comments:
Post a Comment