
NA MARRYGORETH NTANDU ...
Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi Kanda ya Dar es
salaam imemtia hatiani mshtakiwa Ayubu
Mfaume Kiboko pamoja na mke wake Pilly Mohamed Kiboko na kuhukumiwa kwenda jela
miaka 20 kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya.
Kesi hiyo Na.13/2019, imetolewa
hukumu Desemba 18, 2020 mbele
ya Mhe. Jaji Lilian Mashaka ambapo Imeelezwa Mahakamani hapo kuwa mnamo tarehe 23 Mei, 2018
mshtakiwa huyo pamoja na mke wake walikamatwa na Maafisa wa Mamlaka ya Kuzuia
na Kupambana na Dawa za Kulevya mara baada ya kufanya upekuzi wa nyumba yao
iliyopo eneo la Tegeta Nyuki Jijini Dar es salaam.
Katika upekuzi huo walifanikiwa
kupata Madawa ya kulevya aina ya Heroid
Hydrochloride yenye ujazo wa Gram 251.25
Baada ya kupatikana kwa madawa hayo washtakiwa hao
walishtakiwa kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya chini ya kifungu cha
15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Katika kuthibitisha shtaka hilo upande wa Jamhuri uliwaita
mashahidi 6 na kutoa vielelezo 16 ambapo upande wa utetezi washtakiwa
walijitetea wenyewe na kutoa vielelezo viwili.
Baada ya kupitia ushahidi huo kwa ujumla wake, mahakama
imejiridhisha kwamba Jamhuri imethibitisha shtaka bila kuacha shaka, hivyo kuwatia hatiani washtakiwa wote wawili.
Kesi hiyo imeendeshwa na Mawakili wa Serikali Faraja Nchimbi, Salim Msemo, Costantine Kakula, Candid Nasua pamoja na Tully Helela.






No comments:
Post a Comment