• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

MKURUGENZI WA MASHTAKA ATEMBELEA GEREZA LA ISANGA

 

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu ametembelea Gereza Kuu la Isanga Jijini Dodoma kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili Maafisa wa Magereza katika kuwatunza wafungwa pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili mahabusu.

Akizungumza baada ya kutembelea Gereza Kuu la Isanga, Mkurugenzi wa Mashtaka amesema kuwa lengo la kutembele wafungwa na mahabusu ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo kwa misingi ya sharia na kanuni zake.

“kufanya haya yote ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo lakini tukipata hizi changamoto na kusikiliza tunaenda kuzifanyia kazi na kuzishughulikia. Changamoto tulizozipokea ambazo hazipo chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka tunazichukua na kuzipeleka ofisi ambazo zinahusika lengo ikiwa ni kuona Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo.”

Amesema miongoni wa changamoto ambazo amezipokea katika ziara yake ambazo mahabusu wamezieleza ni suala zima la ucheleweshwaji wa kesi na kuchelewa kwa upelelezi ambapo ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kuzishughulikia changamoto hizo kwa kuhakikisha kuwa wameshasajili Hati za Mashtaka Mahakama Kuu ambazo hivi sasa zipo katika mchakato wa kusikilizwa.

“Mahabusu wengi ambao nimewasikiliza wamesema kesi zao zimechelewa upelelezi lakini hali halisi ni kwamba kesi zao hazijachelewa upelelezi kwa kuwa tayari umekamilika na kinachosubiriwa ni utaratibu wa kesheria ambao utawezesha kesi hizo kusikilizwa na Mahakama Kuu.”

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeanza mwendelezo wa ziara zake katika Magereza mbalimbali nchini kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili Maafisa wa Magereza, wafungwa pamoja na mahabusu ili kuhakikisha Haki Jinai inasimamiwa ipasavyo kwa mujibu wa Ibara ya 59B ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.



Share:

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YAKABIDHI MSAADA KWA WATOTO WALIOPO KWENYE VIZUIZI VYA KISHERIA

 Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania  Bw. Sylvester Mwakitalu, amekabidhi  msaada wa magodoro, taulo za kike, mashuka, mafuta na sabuni kwa Mkuu wa gereza la mahabusu Segerea Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hamisi Lissu.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema msaada huo pamoja na vitu vingine umetolewa kwa ajili ya kuwahudumia watoto ambao wameshikiliwa kwenye vizuizi vya kisheria kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya.

Msaada huo uliwasilishwa baada ya kuupokea kutoka Shirika la Utangazaji (TBC) ambalo lilitoa msaada huo kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ikiwa ni mchango wa Shirika hilo katika kuisaidia jamii.


" Nashukuru wadau wote wanaoendelea kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya uhalifu na leo asubuhi nimepokea msaada wa magodoro, mashuka, taulo za kike, sabuni na mafuta kutoka Menejimenti ya Shirika la Utangazaji Nchini( TBC) kwa ajili ya kuwapelekea watoto waliopo vizuizini na waliokinzana na sheria" anasema Mkurugenzi Mwakitalu

" Tunalo kundi kubwa la watoto ambao wanakaa kwenye Magereza na wazazi wao ( wanawake) ambao wanapatikana na hatia au wameshtakiwa kwa makosa ya jinai kwa sababu moja au nyingine anakosa dhamana na kwenda gerezani wakiwa na watoto wao na hawa ndio kundi kubwa ambalo lipo Katika Magereza yetu" anasema Mwakitalu.

Akimkabidhi msaada huo kwa DPP, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Moses Chitama, amesema msaada huo unalenga kurudisha fadhila kwa jamii, hivyo alitoa wito kwa jamii na wadau mbalimbili ikiwemo Sekta binafsi na mashirika ya Umma kuiga mfano kwa TBC wa kusaidia jamii.

Chitama amesema msaada huo wenye thamani ya Shilingi milioni tano (5,000,000/=)  umetolewa na Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC) kwenda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kuupeleka gerezani kwa watoto wa wenye uhitaji maalumu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Segerea, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hamis Lissu, amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kutokana na watoto kuhitaji misaada mbalimbali ikiwemo magodoro na sabuni na vitu vingine.


" Msaada huu utaenda kutumika kama ulivyokusudiwa kwa walengwa, hivyo tunaomba wadau wengine waige mfano kama huu ulioonyeshwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Shirika la Utangazaji nchini kwa kuwajali wahitaji" amesema SSP Lissu.

Share:

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YAKABIDHI MALI ZITOKANAZO NA UHALIFU ZA SHILINGI BILIONI 4.4

 

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekabidhi Wizara ya Fedha na Mipango mali 8,188 zenye thamani ya Shilingi bilioni 4.4 zilizotokana na uhalifu 



Mali hizo zilikabidhiwa Oktoba 3, 2022 na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Bw.Sylvester Mwakitalu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba.

Mali hizo zimeshikiliwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Njombe, Morogoro, Dodoma, Kagera na Dar es Salaam. 

Akizungumza Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Chotto Sendo amesema makabidhiano hayo yanahusu nyumba 19, viwanja (9), mashamba mawili (2), vyombo vya moto (63), magari 31 na pikipiki (9).

Nyingine ni mbao (4,796), madumu (109) ya lita 20 kila moja ya mafuta ya ndege/taa, mashine moja ya kukobolea mpunga na madini bati yenye uzito wa kilo 2,104.



Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema awali baadhi ya mali walizokabidhi Serikalini siku za nyuma, zilileta changamoto kwa washtakiwa kukataa rufaa na mahakama kutengua maamuzi ya mwanzo.

Amesema hiyo ndio sababu kuu ya mali hizo kuendelea kushikiliwa na ofisi yake kwa kipindi hicho ili kutoa nafasi kwa washtakiwa kutafuta haki zao zote kabla ya kuzikabidhi kwa Serikali.



Amesema kuwa mali wanazokabidhi leo hazina kipingamizi kwasababu washtakiwa walipata nafasi ya kutafuta haki zao hadi mahakama za juu ama wengine waliridhika na uamuzi wa mahakama.

 “Kwa mujibu wa sheria zetu mhalifu hatakiwi kunufaika na mali alizopata kutokana na uhalifu. Kwasababu zikibaki kwa wahalifu zitatumika kufadhili uhalifu mwingine au zitawanufaisha wahalifu na kuonyesha jamii uhalifu unalipa,” aliyasema hayo Mkurugenzi wa Mashtaka.



Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba amesema baada ya kukabidhiwa kwa mali hizo watafanya uchambuzi kuona zinazofaa kwa ajili ya matumizi ya Serikali ambazo watazigawa kwa taasisi za umma zikaendelee kutoa huduma na zisizofaa kwa matumizi ya Serikali zitapigwa mnada.



Naye Mkurugenzi wa Mashtaka aliwataka wahalifu kuacha kutenda uhalifu kwakuwa haulipi



Share:

TCRA YAKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA KWA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi zikiwemo kompyuta Mpakato 11, kompyuta za mezani 5, Mashine ya kunakilia 1 na Mashine ya kuchapia (Printa )1.

Akikabidhi vifaa hivyo katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka leo Jijini Dodoma Mkurugenzi wa Sheria kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Modestus Ndunguru  ameitaka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuvitumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili vikalete tija na mchango mkubwa kwa Watanzania.

“Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inafarijika sana inapotoa vifaa hivi kwa Taasisi lakini faraja ni kubwa zaidi hicho kinachotolewa kinapata Thamani kubwa kutokana na mchango wa mtumiaji.Ofisi ya Mashtaka ndiyo itakayoleta thamani ya vifaa hivyo kwa Jamii, nendeni kavitumieni vifaa hivi kwa huduma nzuri ili mafao yafike kwa jamii." Amesema Modestus Ndunguru.


Aidha, Nduguru Amesema katika Kompyuta Mpakato 11 watakabidhi Kompyuta Mpakato 5 na kubakia Kompyuta Mpakato 6 ambazo zitakabidhiwa muda mfupi ujao ambapo amesema wataendelea kutoa vifaa vya TEHAMA kwa Taasisi mbalimbali nchini ili kuongeza ufanisi na urahisishaji wa kazi.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande ameihakikishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwamba vifaa hivyo vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na vitatunzwa kwa kila namna ili vikalete matokeo chanya katika kuwahudumia Watanzania.

“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kama zilivyo ofisi zingine za haki jinai zina mahitaji makubwa ya vifaa vya TEHAMA. Mikoa ya Kimashtaka Tanzania ipo 30 na inahitaji vifaa vya TEHAMA, ninaahidi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwamba vifaa hivi  vitaenda kutumika vizuri lakini pia kutokana na uhitaji mkubwa wa vifaa hivi kesho vinaenda kutumika na havitokaa stoo kwa sababu mahitaji yake ni makubwa” amesema  Bw.Joseph Pande.

Ikumbukwe kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeanzishwa kama Ofisi huru ya Umma kupitia Tangazo la Serikali na 49 la Mwaka 2018 la tarehe 13 February 2018 la kuanzisha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kutekeleza Mamlaka ya kikatiba aliyopewa Mkurugenzi wa Mashtaka ya kusimamia haki jinai kwa Mujibu wa Ibara ya 59B ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977

Share:

MAAFISA TRA NA BENKI WALIOACHIWA HURU NA MAHAKAMA YA KISUTU WATIWA HATIANI KWA KOSA LA UTAKATISHAJI FEDHA

 Mahakama ya Rufani imetoa hati ya kuwakamata na kuwaweka  rumande washtakiwa wanne, akiwamo aliyekuwa mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Idara ya wafanyabiashara wakubwa anaefahamika kwa jina la Justice Katiti.                                     

Awali, wajibu rufani walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya jinai namba 152 ya mwaka 2010 kwa mashtaka kumi, yakiwamo kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu. 

Washtakiwa hao wanadaiwa kula njama ya  kufanya uhalifu, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya Udanganyifu kiasi cha shilingi milioni 338 na utakatishaji fedha haramu.

Mahakama hiyo imewatia hatiani washtakiwa hao,  baada ya kutengua uamuzi wa hukumu iliyotolewa na Mahakama kuu Kanda ya Dar es salaam ya kuwaachia huru washtakiwa hao, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Mbali na Katiti, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya rufani ya Namba 15/2018 ni Robert Mbetwa na Gidion Otullo, waliokuwa wafanyabiashara na Godwin Paula. Na jopo la Majaji watatu wa Mahakama hiyo, wakiongozwa na Shabani Lila, Ignas Kitusi na Lilian Mashaka, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Katika uamuzi huo, jopo hilo la majaji limeamuru wajibu rufani wawekwe mahabusu huku jalada la kesi hiyo, likielezwa kurejeshwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kutoa adhabu.

Awali, jopo la Mawakili wa Serikali Waandamizi watatu  likiongozwa na Nassoro Katuga, Hellen Moshi na Tumaini Mafuru,  walidai Serikali ilikata rufaa baada ya kutoridhika na hukumu iliyotolewa Mahakama ya Kisutu na Mahakama Kuu.

Share:

USHIRIKIANO WA TAASISI TATU UMETUPA MATOKEO CHANYA - DPP


Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu ameeleza namna jinsi ambavyo Ofisi yake ilivyoshirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika kupunguza kesi mbalimbali zinazotokana masuala ya jinai. 

                                                


"Uhalifu hauwezi kuisha kwa taasisi moja kupambana peke yake, lakini tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kukabiliana na uhalifu. Na kwa taarifa tulizonazo tumefanya vizuri. Ushirikiano wa hizi Ofisi tatu umetupa matokeo chanya, kwa sasa Upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai unafanyika vizuri, mashtaka yanaendeshwa vizuri na matokeo tunayaona." Amezungumza hayo Mkurugenzi wa Mashtaka wakati akifanya mahojiano na Waandishi wa vyombo vya habari mara baada ya kufungua kikao cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambacho kimefanyika leo tarehe 11 Agosti, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gaspar Jijini Dodoma

Pia DPP aliendelea kueleza kuwa kikao hicho ni muhimu kwa maana kinalenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu  ya kipindi cha mwaka uliopita pamoja na kuweka mikakati ya utendaji wa mwaka unaofuata na pia nikwa namna gani watashirikiana kwa pamoja kukabiliana na uhalifu.

                                                          


Aidha, Mwakitalu alisema kuwa Takwimu walizonazo kwa sasa mahabusu wengi sana wamepungua kwenye magereza, na wamepungua kwasababu kesi zao zinakuwa zimefika mwisho kwa maana kuwa wamefungwa au Mahakama imewakuta hawana hatia na kuweza kuwaachia huru. Hivyo kupitia tathmini hiyo iliyofanyika na taarifa zilizopo kazi inafanyika vizuri.

Nae pia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Kamishna wa Polisi Salum Hamduni alieleza kuwa kikao hicho ni mwendelezo wa kikao cha mwaka jana ambacho walikaa na wadau katika mnyororo wa haki jinai, hususani katika taasisi hizo ambazo zinahusika na uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka. Na lengo la vikao hivyo ni kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa pamoja katika kuhakikisha wanatoa huduma ambayo wananchi waliitarajia

"Sisi tunalenga haki za watu, kwahiyo pale ambapo tunachelewa kukamilisha upelelezi maana ake tunachelewesha haki za mtu mwingine." Amezungumza hayo Mkurugenzi Hamduni.

Pia Kamishna wa Polisi Salum aliendelea kueleza kuwa lengo kuu hasa la vikao hivyo ni kuona namna ambavyo wanaweza kuongeza tija ya ufanisi katika kuharakisha shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka.             

Hivyo basi kupitia ushirikiano huo na uratibu ambao unafanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekwenda kupunguza kwa kiwango kikubwa manung'uniko ya wananchi. Pia tathmini itakayofanyika itasaidia kuona namna ambavyo wamefanya vizuri na wapi wamekwama ili kuweza kurekebisha na hatimae kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi ambao wanawahudumia

Aidha, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kamishna wa Polisi  Ramadhani Kingai ameeleza kuwa kikao hicho kina dhumuni la kuangalia ni wapi ambapo wamefikia kulingana na yale waliyoelekezana katika maazimio ya kikao kilichopita cha mwaka jana mwezi Julai. Na pia kuangalia ni wapi kuna mapungufu ili kuweza kuboresha kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora na kupunguza malalamiko katika jamii yanayohusiana na utendaji wao wa kazi ikiwepo upelelezi kuchukua muda mref                               

"Tumefanya kaguzi ili kubaini mapungufu haya, na sasa tupo kwenye kikao hiki ili kuweza kufanya tathmini ni kwa namna gani tunaweza kuyamaliza mapungufu haya." Amezungumza hayo Kamishna Kingai

Pia aliendelea kueleza kuwa suala la uchunguzi kuchukua muda mrefu kunatokana na sababu mbalimbali za kiutendaji, lakini kulingana na sasa muungano wao unapunguza hizo changamoto                                      




Share:

NAIBU KATIBU MKUU AZINDUA TAARIFA YA UKAGUZI WA VIZUIZI WANAKOSHIKILIWA WATOTO WALIOKINZANA NA SHERIA.

 Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Khatibu Kazungu amefanya uzinduzi wa Taarifa ya Ukaguzi wa Vizuizi wanakoshikiliwa Watoto waliokinzana na Sheria ambao umefanyika tarehe 18 Julai, 2022 Jijini Dodoma.

                                                    


Katika hafla ya uzinduzi huo Dkt. Khatibu ameeleza kuwa mtoto ndio taifa la leo hivyo wasipowekeza kwenye maeneo ya watoto katika kiafya, kielimu na kiakili zaidi basi taifa hili litaangamia zaidi.

"Uwekezaji katika maeneo haya ni muhimu sana kwa watoto wetu, na ni moja ya sababu ambazo zinapelekea watoto hawa 435 kukutwa katika maeneo mbalimbali ya vizuizi hapa Tanzania. Hivyo juhudi zozote zinazolenga kuhusu ustawi wa watoto hazina budi kupongezwa." Amezungumza hayo Dkt. Kazungu

Aidha Naibu Katibu Mkuu alitoa pongezi kwa niaba ya Wizara ya Katiba na Sheria kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuona umuhimu wa kukagua vizuizi hivyo kwa lengo la kulinda watoto walio kwenye mkinzano wa vyombo vya sheria. Pia alitoa pongezi kwa wadau wote  walioshirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kukamilisha zoezi hilo kwa mafanikio makubwa                                               

Pia Dkt. Kazungu aliendelea kueleza kuwa matokeo yaliyofanyika ya ukaguzi huo ni vema yatumike kama kizio cha kaguzi zitakazoendelea ili kuweza kuona kama wanasonga mbele ama hawajaweza kuimarisha haki za watoto.

"Natambua jukumu la haki jinai sio la Wizara ya Katiba na Sheria peke yake, hivyo ni imani yangu kuwa wadau wote mlio katika mnyororo huu tutashirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa yale yote yaliyomo ndani ya taarifa hii ambayo tunakwenda kuizindua leo hii na katika taarifa zitakazokuwa zinakuja kadri tutakavyosonga mbele." Ameyasema hayo Naibu Katibu Mkuu         

Nae pia Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alieleza kuwa katika ukaguzi wao walioufanya kwa kipindi hicho walikuta watoto 435 wakitunzwa kwenye Taasisi mbalimbali ambazo zimepewa majukumu kisheria. Na kati yao watoto 46 walikuwa hawajakinzana na sheria ambao wapo mahabusu kwasababu ya wazazi wao wameshikwa kwa makosa mbalimbali ambao pia ni watoto wadogo wasioweza kutenganishwa na wazazi wao. Pia walikuta watoto 260 wapo  kwenye Magereza ambapo kati yao tayari wapo hatiani kutumikia vifungo vyao na wengine kesi zao zilikuwa zikiendelea kwahiyo wapo mahabusu. Na kwa upande wa kwenye shule ya marekebisho watoto waliokuwepo ni 40, kati yao watoto 38 walikuwa ni watoto wa kiume na watoto 2 ni mabinti                                      

Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu aliendelea kueleza kuwa katika ukaguzi huo hawakuishia kuona watoto walioko kwenye Taasisi hizo bali walisonga mbele zaidi ili kuweza kufahamu sababu zinazowafanya watoto hawa kuingia kwenye ukinzani na sheria na wakaweza kubaini kuwa chanzo kikubwa ni yalikuwa ni malezi.

"Watoto wengi ambao wameingia katika changamoto hii tumebaini wanatoka katika familia ambazo zina migogoro. Na pia tumebaini kuwa watoto wengi wanaoingia kwenye shida hii ni wale ambao hawapo shule au wanaenda shule kwa kusuasua. Hii yote ni sababu ya kukosa malezi mazuri kutoka kwa wazazi na jamii." Ameyasema hayo DPP.

Pia DPP aliendelea kueleza kuwa wapo watoto ambao kwasababu mbalimbali hawapo pamoja na wazazi wao. Na jamii ina jukumu la kuhakikisha watoto hawa wanapata malezi na kupata haki zao zote za msingi.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Tumaini Kweka  alieleza kuwa Taarifa hiyo inahusu ukaguzi wa vituo na maeneo ambayo wanashikiliwa watoto waliokinzana na sheria, ambayo inahusu magereza, Mahabusu za  Polisi na inahusu shule maalum za mafunzo ya watoto pamoja na nyumba maalum ambapo watoto hao waliokinzana na sheria wanashikiliwa.                                              

Pia Mkurugenzi Kweka aliendelea kusema kuwa Taarifa hiyo inahusisha zoezi ambalo lilifanyika mwishoni mwa mwaka 2021 pamoja na mwanzoni mwa mwaka 2022 ambapo timu maalum kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilikwenda kutembelea maeneo hayo chini ya ufadhili wa UNICEF ili kuangalia ni kwa namna gani sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inatekelezwa dhidi ya watoto hao ambao wamekinzana na sheria.

Na baada ya ukaguzi huo  timu iliweza kuandaa Taarifa ikiainisha maeneo mbalimbali kuhusiana na utekelezaji wa sheria ya mtoto pamoja na matamko mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa. Na ni kwa namna gani yalikuwa yanatekelezwa katika kuhakikisha haki na ustawi wa mtoto ambae amekinzana na sheria.                                              


Share:

KIKOSI KAZI CHA ULINZI KWA WATOTO DHIDI YA BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI WA BINADAMU CHAZINDULIWA

 

Waziri Wa Katiba na  Sheria Mhe. Damas  Ndumbaro  amezindua kikosi kazi cha ulinzi kwa watoto dhidi ya biashara haramu ya Usafirishaji wa binadamu.

Kikosi kazi hicho kimeanzishwa chini ya Mradi wa kupambana na Uhalifu mkubwa wa kupangwa ( Serious Organised Crime- SOC), ambacho kitatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizindua kikosi kazi hicho, Waziri wa Katiba na Sheria, leo Julai 21, 2022 Dkt. Damas Ndumbaro, amesema athari ya uhalifu mkubwa wa kupangwa ni kubwa na inakuwa ya kushtukiza.


"Sisi, Tanzania tunayo mifano hai kuhusu madhara ya uhalifu wa aina hii, kwa mfano uripuaji wa mabomu katika ubalozi wa Marekani uliotekelezwa hapa kwetu, Kenya na Uganda kwa wakati mmoja." Amesema Dkt.  Ndumbaro na kuongeza

Amesema kutokana na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika mapambano dhidi ya ukatili na udhalilishaji  wa wanawake na watoto, wameanza kushuhudia kuibuka kwa taarifa kuhusu uhalifu wa aina hiyo katika jamii na umeonesha bayana juu ya kazi kubwa iliyopo katika kukabiliana na janga hilo.

" Kwa maelezo hayo ninajenga hoja kwamba mradi huu wa kupambana na uhalifu mkubwa wa kupangwa hasa ule wa usafirishaji haramu wa Binadamu, unyonyaji na udhalilishaji wa watoto kingono ni muhimu sana na umekuja kwa wakati unaofaa katika nchi yetu" amesema Dkt. Ndumbaro.

Kwa msingi huo, sisi sote tuliopewa dhamana ya kupambana na uhalifu mkubwa wa kupangwa kwa Makosa ya Biashara Haramu ya Binadamu, Ukatili na Udhalilishaji wa Watoto Kingono na Uhalifu Unaovuka Mipaka ya Nchi katika jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatuna budi kuitumia fursa hii ili kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kuhudumia taifa hili. Huu ni wakati wa kubuni mbinu mbali mbali zitakazoweza kubainisha hila na ghilba za wahalifu pia kubainisha changamoto zinazowakabili wapambanaji wa kazi hii na kutafuta mbinu muwafaka za kukabiliana nazo ili kufikia malengo tuliojiwekea.

Ubunifu wa mbinu mpya ni lazima utekelezwe sambamba na kuongeza uwezo wetu wa teknolojia ya mitandao ambayo baadhi ya wakati inatumika vibaya ili kuwanufaisha wahalifu wanaotaka mafanikio bila ya kufuata na kuheshimu sheria za ndani ya nchi na kimataifa.

" Kwa msingi huu sisi sote tuliopewa dhamana ya kupambana na uhalifu mkubwa wa kupangwa kwa Makosa ya Biashara Haramu ya Binadamu, Ukatili na Udhalilishaji wa Watoto Kingono na Uhalifu Unaovuka Mipaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatuna budi kuitumia fursa hii ili kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kuhudumia taifa hili." Amesema Dk Ndumbaro na kusisitiza

" Huu ni wakati wa kubuni mbinu mbali mbali zitakazoweza kubainisha hila na ghilba za wahalifu pia kubainisha changamoto zinazowakabili wapambanaji wa kazi hii na kutafuta mbinu muwafaka za kukabiliana nazo ili kufikia malengo tuliojiwekea" amesisitiza.

 

Amesema Ubunifu wa mbinu mpya ni lazima utekelezwe sambamba na kuongeza uwezo wa teknolojia ya mitandao ambayo baadhi ya wakati inatumika vibaya ili kuwanufaisha wahalifu wanaotaka mafanikio bila ya kufuata na kuheshimu sheria za ndani ya nchi na kimataifa.

Akizungumzumzia mradi huu, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania ( DPP) Bw. Slyvester Mwakitalu amesemea mradi huo ni wa miaka minne kuanzia Desemba, 2021 hadi Desemba 2025 na unatekelezwa kwa gharama ya dola za Kimarekani 6,434,320 ambapo zitatumika kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

"Mradi huu unatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza na Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Ulaya kupitia Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) likishirikiana na UNICEF pamoja na Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM)" amesema Mwakitalu.

Mwakitalu amesema mradi huo umelenga kujenga uwezo wa kiutendaji kwa taasisi za Serikali zinazohusika katika utekelezaji wa sheria za kupambana na uhalifu mkubwa wa kupangwa ambapo kwa Tanzania Bara utajikita zaidi katika makosa ya biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu na udhalilishaji (unyanyasaji) wa watoto.

"Lengo kuu la mradi huu wa SOC ni kuvijengea uwezo vyombo vya ulinzi na usalama vinavyohusika katika utekelezaji wa sheria za mapambano dhidi ya uhalifu mkubwa wa kupangwa hasa katika nyanja za upelelezi, uendeshaji wa mashtaka na ulinzi kwa wahanga na manusura" Amesema Mwakitalu.

Kwa upande wake, Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.  Doroth Gwajima amesema uzinduzi wa kikosi hicho umekuja wakati muafaka wakati Serikali ikiendelea kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.


 

 

Share:

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA AZINDUA MWONGOZO WA KIUTENDAJI WA UPELELEZI NA UENDESHAJI WA KESI ZA RUSHWA

  Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda amezindua Mwongozo wa Kiutendaji wa Upelelezi na Uendeshaji wa Kesi za Rushwa ambao umetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 18 na 24 vya Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka, Sura ya 430 nchini.

Uzinduzi huo ameufanya kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria  Dkt. Damas Ndumbaro leo Mei 31, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Geophrey Pinda ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria itashirikiana kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kuhakikisha mfumo bora wa utoaji haki kwa wananchi unazidi kuimarika na kuleta ufanisi.

"Mahakama ya Tanzania imefanya mabadiliko makubwa sana, lakini haiwezi kuperfom kama nyie hamna vitendea kazi vya kusaidia kesi zao kwenda, kwa hiyo tumekubalina kwenye Mpango wa Serikali tunakuja na mageuzi makubwa na ya idara zote zinazosaidia katika huduma za utoaji haki." Ameyasema hayo Mizengo Pinda

Pia ameongeza kuwa, dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwa na mfumo mzuri wa utoaji haki kwa wananchi hivyo ushirikiano wa dhati wa Wizara hizo ni muhimu sana ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao pamoja na kuendesha shughuli za maendeleo kwa ufanisi.


Nae pia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw.  Sylivester Mwakitalu amewapongeza wadau wa maendelo ikiwemo Serikali ya Uingereza na Umoja wa Ulaya ambao wameshiriki kikamilifu kufanikisha juhudi mbalimbali za Serikali katika kupambana na vitendo vya rushwa.

DPP alieleza kuwa, upelelezi wa makosa ya rushwa unahitaji umakini wa hali ya juu kutokana na makosa hayo kufanywa na watu wenye weledi, hivyo upelelezi wake unahitaji umakini na umahiri ndiyo maana Ofisi ya Taifa ya Mashitaka kwa kushirikiana na wadau waliona ni vyema wakatengeneza mwongozo huo ambao utawasaidia Wapelelezi na Waendesha Mashtaka wanapoendesha kesi hizo ili kuleta usawa.


"Kwa kipindi ambacho tuliwapatia madaraka Waendesha Mashtaka wa Mikoa na Wilaya tuligundua ziko changamoto za hapa na pale hati za Mashtaka za mahali pamoja zinatofautiana na hati za Mashtaka za sehemu  nyingine, na namna uchunguzi unavyopita sehemu moja na sehemu nyingine kwa hiyo tukaona kwa kushirikiana pamoja tutengeneze mwongozo ambao utawaongoza waendesha Mashtaka na Wapelelezi ili waweze kufanya kazi hiyo kwa weledi, lakini tupate tija na pia tupate matokeo chanya." Ameyasema hayo DPP Mwakitalu

Mkurugenzi Mwakitalu alieleza kuwa Mwongozo uliozinduliwa  hautosaidia  kubadilisha dira, bali taratibu zilizopo ni nyongeza ya kile ambacho tayari kipo na  kitasaidia Watumishi wote ambao watashiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.

DPP aliendelea kueleza kuwa mwongozo  utawawezesha Wapelelezi na Waendesha Mashtaka kushughulikia kesi za rushwa kwa urahisi na tija, na mara baada ya kuzinduliwa utasambazwa na kuhakikisha kwamba watendaji wote wanaupata na pale itakapolazimika kufanya mafunzo ili kurahisisha wauelewe na wautumie kikamilifu basi itafanyika hivyo.

"Mwongozo huu ni nyenzo muhimu sana kwetu kwani  utatusaidia kupata matokeo chanya katika kupambana na rushwa." Ameyasema hayo DPP Mwakitalu.

Aidha, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Joseph Pande  amesema kuwa, mwongozo huo utasaidia kwa kiwango kikubwa ikiwemo kuongeza mahusiano kuanzia tukio linapotokea mpaka kesi itakapomalizika mahakamani.

Nae pia Mkurugenzi wa Divisheni ya Makosa ya Udanganyifu, Utakatishaji Fedha na Rushwa kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Oswald Tibabyekomya ameeleza  kuwa, Mwongozo wa Kiutendaji wa Upelelezi na Uendeshaji wa Kesi za Rushwa (Standard Operating Procedures for Investigation and Prosecution of Corruption and Related Offences), umetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 18 na 24 vya Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka, Sura ya 430 (The National Prosecutions Service Act, Cap 430).

Vifungu ambavyo amesema, vinampa Mkurugenzi wa Mashtaka mamlaka ya kutengeneza miongozo kwa ajili ya kuratibu upelelezi na kusimamia mashtaka.

"Lengo la Mwongozo huu ni kuweka mfumo unaofanana wa kupeleleza na kuendesha mashtaka kwa kuelekeza masuala muhimu ya kuzingatia na kutengeneza nyenzo kama vile mpango wa uchunguzi (Investigation Plan), Uendeshaji Mashtaka ( Prosecution Plan) na Uchambuzi wa Viini vya Makosa ya Rushwa (Elements Worksheet) ambavyo vitasaidia kuweka utaratibu unaofanana katika kushughulikia kesi hizi." Amefafanua hayo Mkurugenzi Oswald



Pia Mkurugenzi Tibabyekomya aliendelea kueleza kuwa, mambo muhimu yanayosisitizwa katika mwongozo ni Kushauriana na Kuratibu Kesi Kubwa za Rushwa Mapema ( Early Case Consultation and Coordination).

"Katika eneo hili Mwongozo unawataka Wachunguzi baada ya kujiridhisha kuwa kosa limetendeka, kutoa taarifa kwa Viongozi wa Mashtaka kwenye Ofisi za Taifa za Mashtaka ngazi ya Wilaya na Mikoa au kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ili waweze kuteua Mwendesha Mashtaka kuratibu upelelezi huo.

Na Mwendesha Mashtaka atakayeteuliwa atashirikiana na wachunguzi kwenye hatua zote muhimu za upelelezi kwa ajili ya kuhakikisha ushahidi wenye ubora unakusanywa ili kuwezesha kuwa na matokeo mazuri mahakamani." Amezungumza hayo Bw. Oswald.

Pia ameeleza kuwa ili kuhakikisha kunakuwepo na uratibu mzuri, mwongozo unataka wachunguzi na Waendesha Mashtaka kufanya vikao vya pamoja kabla na baada ya kukamata watuhumiwa (pre-arrest conference, post arrest conference) au wakati wowote linapotokea jambo la dharura (emergency conference) kwa ajili ya kujadili mwenendo na masuala muhimu ya upelelezi.

Katika, mwongozo huo, Mkurugenzi Tibabyekomya anasema, wakati wa ukusanyaji ushahidi mwongozo unafafanua utaratibu wa kufuata wakati wa ukamataji, upekuzi na ukusanyaji wa ushahidi wa aina mbalimbali kama vile uchukuaji wa maelezo ya mashahidi, maelezo ya washtakiwa ushahidi wa kitaalam ili kuhakuikisha ushahidi unakusanywa kwa kuzingatia sheria.

Kwa kuzingatia kuwa, makosa ya rushwa ni makosa ambayo yanatendeka kwa ajili ya kupata fedha au mali, amesema mwongozo unawataka wachunguzi kufanya uchunguzi wa mali mapema wanapoanza uchunguzi wa makosa ya rushwa ili waweze kubaini mali hizo na kuchukua hatua stahilifu mapema

Ili kuhakikisha maamuzi yanatolewa baada ya kuelewa vizuri ushahidi, Mwongozo unasisitiza kufanya vikao vya majadiliano kati ya Wachunguzi na Waendesha Mashtaka wakati jalada linapowasilishwa Ofisi za Taifa za Mashtaka au baada ya kuwa jalada limepitiwa na waendesha mashtaka katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Vikao hivi vinaweza kuombwa na Wachunguzi au kuitishwa na Waendesha Mashtaka wanapoona kuna jambo linalohitaji majadiliano

Baada ya upelelezi kukamilika na kesi kufunguliwa mahakamani Mwongozo unawataka wachunguzi na waendesha mashtaka kufanya maandalizi vizuri kabla ya kesi kuanza kusikilizwa kwa kufanya vikao kabla ya kesi kuanza (pre-trial conference) kati ya wachunguzi na waendesha mashtaka. Mwongozo pia umetengeza nyenzo (templates) kama vile nyenzo za kutumia kuwatayarisha na kuwaongaza mashahidi mahakamani na nyenzo ya kutumia kutoa vilelezo mahakamani kwa ajili ya kuahakikisha maandalizi mazuri yanafanyika.


Mwongozo pia umetengeneza nyaraka ya uchambuzi wa makosa yote yaliyopo katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo inachambua viini vya makosa hayo na kutoa mifano ya hati za mashtaka. Lengo la kutengeneza nyenzo hii ni kuhakikisha wachunguzi na waendesha mashtaka wanaelewa vizuri viini vya makosa ili viwasaidie wakati wa upelelezi, maandalizi ya hati za mashtaka na wakati wa uendeshaji wa kesi mahakamani.

Kwa upande wao wawakilishi wa mabalozi, Bw.Simon Charter kwa niaba ya Balozi wa Uingereza nchini Tanzania na Simon Van Broek kwa niaba ya Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania wamesema kuwa, wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupambana na vitendo vya rushwa.

Sambamba na shughuli mbalimbali za maendeleo Ili iweze kutekeleza kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Share:

WAENDESHA MASHTAKA NA WAPELELEZI WAJENGEWA UWEZO

 Serikali imeendelea kuwekeza katika kuwajengea  uwezo  Waendesha Mashtaka na Wapelelezi ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya kimazingira  na mbinu za kutenda makosa mbalimbali ya jinai yakiwepo ya Wanyamapori na Misitu.

Akifungua mafunzo ya Upelelezi na Uendeshaji wa kesi za Wanyamapori na Misitu kwa Wakuu wa Upelelezi na Waendesha Mashtaka nchini yanayofanyika mjini Moshi kuanzia tarehe 25 Mei, 2022, Kamishna Wambura alitoa rai kwa washiriki wa mafunzo kuhakikisha wanajiongezea maarifa yatakayowasaidia kutekeleza majukumu yao ya kila siku.



Akimkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alisema kuwa  Wapelelezi na Waendesha Mashtaka ni wadau muhimu sana katika mnyororo wa  Haki Jinai.

Aliendelea kueleza kuwa baada ya mafunzo anatarajia kuona mabadiliko makubwa katika utendaji wa kazi.

Aidha Mwakitalu alieleza kuwa ufanisi katika kesi unaanza toka matukio ya uhalifu yanapoanza na mnyororo wa ushirikiano huanzia hapo ambapo mnyororo ukikatika mahali matokeo tarajiwa sio rahisi kupatikana.

'' Changamoto za kiutendaji zinaanzia kwenye kufanya ukusanyaji ushahidi na utunzaji wa vielelezo hivyo mafunzo yanayotolewa yanalenga kutatua changamoto katika ngazi zote.

Aliyasema hayo Mkurugenzi wa Mashtaka Mwakitalu.



Naye pia  Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande akizungumza katika mafunzo hayo  alisema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefanya operesheni maalum ya kusoma mafaili ambapo ni zaidi ya mafaili  elfu moja mia saba na kufungua kesi elfu moja mia tatu na pia kesi zipatazo mia nne zimefutwa.

Naibu Mkurugenzi aliendelea kueleza kuwa ifikapo tarehe 16 Juni 2022,  kesi zaidi ya Mia Mbili hamsini zitakuwa zimesomwa.

"Kesi hizi 250 zitasomwa ndani ya mwezi mmoja na zitasaidia kupunguza sana malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wananchi." 

Alisema Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Joseph Pande



Share:

DPP AHUTUBIA MKUTANO WA NNE WA KIMATAIFA WA WAENDESHA MASHTAKA NCHINI KENYA

 

Rais wa Umoja wa Waendesha Mashtaka kanda ya Afrika Mashariki ( East Africa Association of Prosecutors), ambae pia ni Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania Bw. Sylvester Mwakitalu akihutubia Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Waendesha Mashtaka wa Afrika na Ukanda wa Bahari ya Hindi unaofanyika Mombasa, nchini Kenya.

Mkutano huo unalenga kujadili ,masuala mbalimbali ikiwemo Mikakati ya pamoja ya kupambana na Uhalifu unaoibuka pamoja na Makosa ya Kupangwa yanayovuka Mipaka.

Share:

DPP ASISITIZA UMAKINI NA WELEDI KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA KIOFISI

 


Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa na Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya kazi kwa umakini na kwa weledi ili kuweza kulinda haki na amani za Watanzania hususani katika uendeshaji wa mashauri ya kijinai.

"Tunalo jukumu la kupambana na uhalifu, na sisi ndio kiungo katika mapambano hayo, kwa hiyo tupambane vizuri ili Watanzania waweze kuishi kwa amani, kwani pasipokuwa na amani wala usalama,  hakuna maendeleo katika Taifa letu. Hivyo tukiwa kama viongozi yatupasa kutekeleza Dira na Dhima iliyotolewa na Taasisi yetu"



Ameyasema hayo Mkurugenzi wa Mashtaka wakati akifungua Kikao kazi cha Wakuu wa Mashtaka Mikoa na Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kilichofanyika tarehe 12 hadi 13 Mei, 2022 katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mwakitalu alieleza kuwa katika siku hizi za karibuni kumekuwa na ongezeko la wimbi la uhalifu katika nyanja zote. Hivyo basi kuna jukumu kubwa la kulinda haki hususani zile ambazo zinaangukia kwenye jinai.



DPP aliwapongeza  Wakuu wa Mashtaka Mikoa kwackufanya kazi nzuri ya kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani ijapokuwa bado changamoto hiyo ya msongamano haijaisha.

"Magereza yaliyomengi khali sio nzuri lakini kibaya zaidi Mahabusu ni wengi kuliko wafungwa. Kwahiyo kupitia hili inabidi kujadili kwa kina ili kuweza kupata suluhu ya kupunguza mlundikano mkubwa wa mashauri yaliyopo mahakamani"

Aidha Mwakitalu alisema kuwa ni muhimu kupata taarifa za kila siku kwani zitasaidia kupanga mipango ya maendeleo ya kiofisi. Na pia aliendelea kueleza kuwa kwa upande wa eneo la Takwimu ni muhimu kuangaliwa kwa umakini zaidi ili ziweze kuendana na uhalisia hususani katika eneo la Takwimu za Mahakama za Mwanzo kwasababu zinalenga kesi za jinai. Hivyo basi ni muhimu kuwa na taarifa zake ili kuona idadi ya kesi zilizosajiliwa, zilizoisha, na kujua zimeishaje na faini kiasi gani. Hivyo ni eneo muhimu sana sana la kuangaliwa na kupata ufumbuzi wake.



Naye pia Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande alieleza  kuwa  lengo kuu la kufanya kikao kazi hicho ni kufanya tathmini ya ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, hivyo basi  kikao hicho kimepanga kutoka na  maadhimio juu ya namna gani ifanyike ili kukabiliana na ongezeko la uhalifu na pia kutengeneza mikakati ya pamoja ya namna ya kukabiliana na kesi za jinai ili kuweza kudumisha haki na amani katika Taifa la Tanzania.



Share:

KAILIMA ATAKA KUTATULIWA KWA CHANGAMOTO YA UPELELEZI KUCHELEWA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ramadhani Kailima ameitaka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kushughulikia mambo muhimu sita ili kuboresha utendaji kazi na kutatua changamoto za uratibu wa Upelelezi.



Akizungumza katika hafla ya Ufunguzi wa mafunzo juu ya Makosa ya Mtandao, Uchunguzi na mbinu za Mashtaka Naibu Katibu Mkuu Kailima ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka Waendesha Mashtaka wa Serikali kutumia Mamlaka waliyopewa kisheria kutatua changamoto mbalimbali za kiutendaji. 

Katika hotuba yake Bw. Kailima    aliyataja mambo sita ambayo angependa yashughulikiwe.

Jambo la kwanza alilohitaji lishughulikiwe ni kuwepo kwa changamoto ya upelelezi kuchukua muda mrefu hivyo alitaka eneo hili lifanyiwe kazi kwa kuhakikisha upelelezi unaratibiwa vizuri na kwa haraka.

Eneo la pili Bw. Kailima aliomba Waendesha  Mashtaka kushirikiana na Jeshi la Polisi ili  kutatua changamoto za ucheleweshaji mafaili.

Tatu alitaka Waendesha Mashtaka kukataa rushwa wanapotekeleza majukumu yao kwakuwa rushwa ni adui wa haki.

Nne aliwashauri kutimiza wajibu wao ipasavyo kwakuwa majukumu yao yanaakisi utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Mashtaka.

"Ukitembea, ukiongea, ukifanya kazi uonekane kama DPP kwakuwa huna namna ya kutenganisha majukumu yako na DPP". Alisema Naibu Katibu Mkuu Kailima.

Jambo la tano Naibu Katibu Mkuu Kailima alisisitiza umuhimu wa kuwa waadilifu kwa kuhakikisha kila jambo wanalolitenda kulifanya kwa uadilifu mkubwa.

Na jambo la sita aliwataka Waendesha Mashtaka kuendelea kutunza siri za Serikali.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu aliwataka Mawakili wa Serikali kuyatumia mafunzo hayo kikamilifu na kuboresha utendaji wao wa kazi.

Alisema ukuaji wa teknolojia huja na mambo mema lakini pia huambatana na changamoto hivyo mafunzo yaliyotolewa yatawaongezea weledi wa kupambana na uhalifu.


Bw. Mwakitalu alisema baadaye ofisi itawapima kutokana na utendaji wao wa kazi baada ya mafunzo.

Naye Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Veronica Matikila  alisema Makosa ya Mtandao yanaangukia katika Makosa ya kupangwa ambapo alieleza kuwa mafunzo wanayopatiwa Waendesha Mashtaka wa Serikali yanalenga kuwajengea ufahamu wa namna bora ya kuratibu upelelezi wa Makosa ya Mtandao na Makosa yanayoendana na hayo.


Naye Wakili wa Serikali Bi. Prosista Minja kutoka Songwe kwa niaba ya Washiriki wengine alimshukuru mgeni rasmi kwa kuwafungulia mafunzo na alishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuwaandalia mafunzo ambapo aliahidi kwa niaba ya wenzake kuyatumia mafunzo kuboresha utendaji kazi.

Share:

Labels

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .