Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakati wa ufunguzi wa Baraza la pili la Wafanyakazi wa Ofisi leo Januari 025,2024 katika hoteli ya Lenana Jijini Mwanza
Na Marrygoreth Ntandu.
Mkurugenzi wa Mashtaka
Nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka watumishi wa Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka (OTM) kufanya kazi zao kwa bidii na kuzingatia weledi wa taaluma yao
ikiwemo kufanya kazi kwa uaminifu ili kutenda haki kwa umma.
Mwakitalu ametoa rai hiyo
mapema leo Januari 25, 2024 katika ukumbi wa hoteli ya Lenana ya Jijini Mwanza wakati
akifungua mkutano wa baraza la kwanza la mwaka la wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka lililojumuisha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,Wakuu wa
Mashtaka wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi.
Bw. Mwakitalu amesema
katika kipindi cha mwaka mmoja,Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeweza kufikia
sehemu kubwa ya utekelezaji wa malengo iliyokuwa imejiwekea yakiwepo masuala ya mashauri ya jinai kuendeshwa
na kutolewa maamuzi kwa haraka na kupelekea kupungua kwa mrundikano wa kesi za
muda mrefu katika mahakama nyingi nchini.
Katika hatua nyingine
Mwakitalu ameeleza kuwa kutokana na kuimarika kwa utendaji wa watumishi wa Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka kumesaidia kupunguza mrundikano wa mahabusu katika magereza mbalimbali nchini pamoja na
kupungua kwa malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na wananchi kwa njia mbalimbali
ikiwemo barua pepe, simu na wengine kufika ofisini.
Amesema, Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka imeundwa ili kurahisisha utoaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi kwa
kuwezesha kesi nyingi kuendeshwa kwa wakati na kuhakikisha haki inatendeka kwa lengo la
kuwepo kwa haki, amani na usalama katika nchi yetu.
Aidha, Mwakitalu amesema
katika kuhakikisha watumishi wote wanafanya kazi zao kwenye mazingira salama,
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kutekeleza miradi
mbalimbali ya majengo ya ofisi za mikoa 10 ambapo mikoa miwili kati yake
imekamilika ikiwemo mkoa wa Pwani na Ilala eneo la Kinyerezi ambapo mwishoni
mwa mwezi Januari, 2024, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inatarajiwa kupokea majengo ya Ofisi kutoka mikoa ya
Shinyanga na Manyara.
Bw. Mwakitalu amesema
kuwa mpaka sasa jumla ya ofisi 92 za mashtaka zimefunguliwa katika maeneo
mbalimbali nchini ikiwemo mikoa 30 ya kimashtaka na wilaya 62 za Tanzania Bara ikiwa
ni miongoni mwa mikakati ya ofisi katika kusogeza huduma za kimashtaka karibu
na wananchi.Vile vile Mwakitalu amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka itaendelea kufungua
ofisi katika wilaya 47 zilizobaki ili kuendelea kutoa huduma bora kwa watanzania
wenye kesi mbalimbali.
Naye Katibu wa Baraza la
Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambaye ni Afisa Tawala Mkuu Bw.Juma
Katanga amesema kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kinalenga
katika kujadili na kupitia Mipango na Makisio ya Mapitio ya bajeti katika
kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai 2023 hadi Januari, 2024.
Katanga amesema wafanyakazi
wa OTM bado wanakabiliwa na baadhi ya changamoto zikiwepo uhaba wa wafanyakazi
katika maeneo mbalimbali, upungufu wa vitendea kazi katika ofisi nyingi za wilaya
zilizofunguliwa hivi karibuni huku akisema kuwa Baraza la Wafanyakazi limekuwa sehemu
ya msukumo kwa menejimenti kupunguza baadhi ya changamoto ikiwemo kununua
magari mapya, kuajiri watumishi pamoja
na kununua samani za ofisi katika Wilaya na Mikoa.
Wakati huohuo, Katanga
ameiomba Serikali kuona namna ya kuongeza bajeti katika Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka kutokana na majukumu nyeti inayoyatekeleza kwa Maendeleo ya Taifa ikiwemo kupatikana kwa nyumba za wafanyakazi
zitakazosaidia kuishi katika mazingira salama.
“Mfano Wakili wa Serikali
anaendesha kesi za Ugaidi,Ujambazi, Masuala ya pesa haramu alafu anaishi kwenye
nyumba ya kupanga pengine ni ya jambazi fikiria jinsi mazingira hayo yalivyo hatari, serikali
inapaswa kuliona hili kwa jicho la zaidi” amesema Katanga
Awali akizungumza kabla
ya ufunguzi wa mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi.Javelin Rugaihuruza amesema mkutano
wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashataka ulikusudiwa kufanyika mwishoni
mwa mwaka 2023 lakini kutokana na
sababu zilizojitokeza nje ya uwezo wa taasisi ulishindwa kufanyika na
umefanyika leo tarehe 25 mwezi Januari 2024.






No comments:
Post a Comment