Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi amewataka Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa kuhakikisha wanaimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo wa haki jinai ili kuwezesha haki kupatikana kwa wakati.
Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika tarehe 20 Machi, 2025 Mkoani Morogoro.
Akizungumza na wajumbe na washiriki wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mwakitalu amesema ni vema viongozi hao wakaimarisha ushirikiano kati yao na wadau wengine wakiwemo wadau wa haki jinai ili kurahisisha utendaji kazi wao.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mwakitalu amewataka madereva wa Ofisi ya Mashtaka nchi nzima kufanya kazi zao kwa kuzingatia na kufuata Sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.
Amesema Madereva wasipozingatia sheria, kanuni na utaratibu wa usalama Barabarani wawapo barabarani wanaweza sababisha ajali ambazo zinazuilika kwani ajali husababisha hasara kubwa kwa Serikali, jamii na mtu mmoja mmoja.
‘’Kutofuatwa kwa sheria kunaweza kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo ajali, vifo, ulemavu, na kuharibika kwa mali ambayo serikali hutumia gharama kubwa kuzipata.” Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu.
Aidha amewasisitiza watumishi kuendelea kufanya kazi zao kwa bidii ili kuyafikia mafaniko yaliyolengwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kuhakikisha kuwa haki na ustawi wa jamii vinadumu daima.
Wakati huo huo Baraza hilo limetumia nafasi hiyo kuwaaga watumishi waliostaafu utumishi wa umma katika Ofisi hiyo kwa kufikisha umri wa miaka 60 baada ya kulitumikia taifa ambapo Mkurugenzi Mwakitalu amewasisistiza kwenda kuyaishi mema waliyovuna wangali watumishi.
Wastaafu hao nao wameushukuru uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kuwashika mkono wakati wote na kuahidi kuzitumia vema fedha watakazolipwa kama kiinua mgongo.










