Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Mtwara imemuhukumu Hamisi Peter Suwed @ Mkwidu (45) kunyongwa mpaka kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la Mauaji ya Jamali Saidi Mtepa.
Hukumu hiyo imetolewa tarehe 13 Machi, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Martha Mpaze baada ya kusikiliza mashahidi watano (5) kutoka upande wa jamhuri pamoja na vielelezo vitano (5) na kujiridhisha kwamba upande wa Jamhuri umethibitisha shtaka pasipo kuacha shaka.
Katika kesi hiyo ya Kikao cha Jinai Na. 28 ya mwaka 2023 Bw. Hamisi am
baye ni mkazi wa kijiji cha Mavuji, Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi alikuwa anakabiliwa na shtaka la Mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.)
Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 25 Octoba, 2022 katika kijiji cha Mavuji, Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi ambapo inadaiwa kwamba, siku ya tukio majira ya usiku mshtakiwa wakati anarudi nyumbani kwake alimkuta marehemu akiwa anaiba mboga kwenye shamba lake, Mshtakiwa alichukua jiwe na kumpiga marehemu kichwani mara mbili mara baada ya hapo Mshtakiwa aliendelea kwa kuchukua kisu na kumchinja marehemu mpaka kupelekea kifo chake, pia mtuhumiwa alichukua mwili wa marehemu na kuutupa pembezoni mwa mto karibu na shamba lake.
Kesi hii imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali watatu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Jordan Odhiambo akisaidiana na Denis Nguvu pamoja na Hilal Kabyemela.







No comments:
Post a Comment