Picha ya Dawa za Kulevya aina ya Heroin
RAIA saba wa Iran akiwamo nahodha wa boti, Jan Miran (42) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha heroin zenye uzito wa kilo 504.36 na Methamphetamine zenye uzito wa kilo 355.
Mbali na Miran, washtakiwa wengine ni Issa Ahmad(30), Amir Kasom (35), Salim Fedhmulhammad (20), Ikbal Mohammad(22), Mustaphar Bakshi (20) na Jawid Mohammadi(19).
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao Aprili 30, 2021 na jopo la mawakili wa Serikali waandamizi, Joseph Maugo na Juma Maige mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Maria Bantulayne.
Wakili Maige amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2021.
Kabla ya kusomewa mashtaka yao, hakimu Bantulayne amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi
Akiwasomea mashtaka yao, Wakili Maugo amedai katika shtaka la kwanza washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa April 23, 2021 katika bahari ya Hindi eneo la Lindi wanadaiwa kusafirisha heroin yenye uzito wa kilo 504.36
Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa hao wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine yenye uzito wa kilo 355.0.
Hata hivyo washtakiwa hao walitafutiwa mkalimani anayejua Kiirani kutokana na wao kutokujua lugha nyingine.
Hakimu Bantulayne baada ya kusikiliza shauri hilo, aliahirisha kesi hadi Mei 14, 2021 itakapotajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
kwa upande wake kamishna wa Tume ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Gerald Kusaya, ametangaza hali ya hatari kwa watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi,
na kwamba wamejipanga kikamilifu na vita hivyo Tanzania inaenda kuishinda na kuwa na Tanzania huru bila ya dawa za kulevya.
“Tumejipanga, tutatumia weledi, umakini, nyenzo na kushirikisha wadau wote, vyombo vyetu vya usalama, kufanya kazi usiku na mchana, hatutalala na lazima tutakuwa washindi,” alisema Kusaya.
Aidha aliwataka raia wa Tanzania na wasio raia kutoa ushirikiano kwa Tume katika mapambano akisisitiza kuwa ni vita ya wote ambayo haiwezi kufika mwisho isipokuwa pale kila mmoja atakapokuwa tayari kupambana.
“Hii ni vita ya wote, nitoe rai kwa wananchi wote watoe taarifa na usiri ni jambo la muhimu kwa tume katika utekelezaji, wananchi watoe ushirikiano ili kushinda vita hii,” alisema.






No comments:
Post a Comment