• Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti

    Picha ya pamoja katika uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Serengeti, Mugumu, mkoani Mara. ( Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Edson Makallo baada ya kupokea taarifa ya magari yaliyotaifishwa kutokana na Uhujumu Uchumi na kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani jijini Dodoma.

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini

DPP AWATAKA WATUMISHI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUONGEZA BIDII KATIKA KAZI

 Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  kuongeza bidii, jitihada na ubunifu katika kazi ili Ofisi hiyo iwe ni ofisi bora na pia iwe ni ofisi ambayo wananchi wanakimbilia kupata huduma na kupata haki yao.



Mkurugenzi Mwakitalu amebainisha hayo wakati alipokutana na kuzungumza na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mara baada ya kushiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (MeiMosi) yaliyofanyika leo tarehe 1 Mei, 2025 katika viwanja vya Bombadia Mkoani Singida.

Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Mashtaka ametoa pongezi kwa watumishi hao kwa kujituma kufanya kazi vizuri na kuleta matokeo chanya katika taasisi hiyo.

"Nimepita baadhi ya mikoa na nimeona wananchi wanaamini wakija Ofisi ya Taifa ya Mashtaka watapata ufumbuzi wa matatizo yao." Ameyasema Mkurugenzi Mwakitalu

Share:

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YACHANGIA UFANISI KATIKA USIKILIZWAJI WA KESI ZA UHUJUMU UCHUMI NCHINI

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti  ya  Wizara hiyo kwa Mwaka 2025/2026 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,  Leo tarehe 30 April 2025  ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imechangia ufanisi mkubwa katika uendeshaji wa kesi za Uhujumu Uchumi kwa kipindi kati ya Julai 2024 na Aprili 2025.

Kupitia hotuba yake, Dkt.  Ndumbaro amelieleza Bunge kuwa  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  kwa kipindi cha mwaka wa Fedha  2024/2025 iliendesha kesi kubwa 177 katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi  ukilinganisha na Kesi 60 pekee zilizoendeshwa katika kipindi  kama hicho kwa mwaka 2023/2024.

Waziri Ndumbaro pia amebainisha kuwa katika Kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, kesi za jinai 27,523 ziliendeshwa katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, tofauti na kesi 25,037 zilizoendeshwa katika Mahakama hizo kwa kipindi  kama hicho kwa  mwaka wa fedha 2023/2024.

Ameeleza zaidi  kuwa, Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeendelea kusogeza huduma kwa wananchi ngazi za Mikoa na Wilaya, ambapo katika kipindi cha mwaka 2024/2025 huduma hizo zimepelekwa kwenye mikoa yote 26 nchini pamoja na  Mikoa minne ya kimashtaka hivyo kufanya idadi ya  mikoa 30 inayopata huduma za Kimashtaka. Sambamba na hilo Waziri Ndumbaro amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imefikisha huduma za mashtaka katika Wilaya 108 nchini.

Ameongeza kusema kuwa, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekamilisha ujenzi wa majengo yake katika mikoa ya Manyara, Shinyanga, Katavi, Rukwa, Pwani na mkoa wa Kimashtaka Ilala.

Share:

"Uchunguzi wa Makosa ya kifedha ni nguzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kiuchumi. Mhe." Rose Ebrahim

 Jaji Mfawidhi wa Mahamaka Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Rose Ebrahim amesema uchunguzi wa Makosa ya kifedha ni nguzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya uhalifu huu wa kiuchumi kwani wahalifu wengi wa makosa hayo wamekuwa wakiibua mbinu mbalimbali za kidigitali ikiwemo kuunda mitandao tata isiyoshikwa kirahisi na mbinu za kawaida.

“Kwenye makosa ya kifedha wahalifu wengi huwa wanatumia mbinu za kiteknolojia kutenda au kuwezesha utendekaji wa makosa hayo, hivyo Wapelelezi na Waendesha Mashtaka lazima wawe na ujuzi wa kutosha kufaa kukusanya ushahidi wa kielektoniki na kufuata sheria zilizowekwa ili kusimama vyema bila kupoteza ushahidi”.

Mhe. Jaji ameyasema hayo wakati akifungua Mafunzo ya Utatu kuhusiana na Uchunguzi wa Makosa ya Kifedha na Uchunguzi wa Kisayansi yanayofanyika tarehe 25 na 26 Aprili, 2025 Mkoani Morogoro.

Jaji Mfawidhi amesema ni muhimu  mafunzo hayo kufanyika kwa kila mamlaka ili kuweka utaratibu wa kuwa na mafunzo endelevu ya kubaini mbinu zinavyobadilika kila kukicha kwani itasaidia kupata nafasi ya kubadilishana uzoefu kwa mambo au mbinu na changamoto ambazo wengine wanakutana nazo na namna bora ya kukabiliana nazo.

Katika hatua nyingine Mhe. Jaji amesisitiza juu ya umuhimu mkubwa wa Ushahidi wa Kisayansi katika utendaji wa haki ambapo Sayansi na Teknolojia vimeshika atamu.

“Ni lazima tuwe na maarifa na mbinu za kutosha za kiupelelezi na ukusanyaji ushahidi unaojibu makosa ya kifedha ili kuisaidia mahakama kutoa maamuzi yaliyosahihi kwa upande wa mashtaka na kuweza kutaifisha mali zinazotokana na makosa husika.’’ Amefafanua Mhe. Jaji Rose.

Sambamba na hilo amewataka Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwawezesha kupata ushahidi wa uhakika na uliokamilika.

Aidha, amesema Mashtaka bila ufuatiliaji wa mali ni ushahidi nusu, ni ushindi ambao bado haujakamilika. Uhalifu wa kifedha sio tu kuwafikisha wahusika mahakamani bali ni kuhusu Urejeshaji wa mali, uwajibikaji na kutoa fundisho kwa wengine.

Mali yoyote au fedha inayoporwa kutoka kwa umma au wananchi inapaswa kurejeshwa na kila mhalifu hanabudi ya  kuadhibiwa pamoja na kupokonywa faida ya uhalifu huo.

Pia amesema mafunzo hayo yakawe chachu kwao katika kupambana na uhalifu huo wa kifedha na kutumia ushahidi wa kisayansi ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atakaethubutu kuchezea mali za taifa, kuzipora au kuzihujumu na kuachwa akafaidika kwa namna yoyote ile.

Kwa upande wake Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Morogoro Bi. Tarsila Gervas ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uwezo Wapelelezi na Waendesha Mashtaka katika masuala ya Makosa ya kifedha pamoja na makosa mengine yanayohusisha Ushahidi wa Kisayansi.

Pia amesema mafunzo hayo ni dhamira ya dhati kwa Mkoa wa Morogoro katika kuhakikisha wanafanya upelelezi na uendeshaji wa mashtaka ambao unakuwa na ufanisi mkubwa na unaolenga kukomesha uhalifu katika mkoa huo.

"Tunataka kuujenga mkoa salama ambapo wananchi wake wanaweza kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa amani pasipo kusumbuliwa wala kuwa uwoga wa vitendo vya kiuhalifu." Amefafanua Bi. Tarsila

Aidha mafunzo hayo yamehusisha taasisi mbalimbali zinazounda mnyororo wa haki jinai zikiwepo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU, TAWA, TANAPA, TFS, Jeshi la Polisi, na Uhamiaji.

Share:

DPP AWATAKA WAKUU WA MASHTAKA MIKOA KUIMARISHA UHUSIANO NA WADAU

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  amewataka Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa kuhakikisha wanaimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo wa haki jinai ili kuwezesha haki kupatikana kwa wakati.

Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika tarehe 20 Machi, 2025 Mkoani Morogoro.

Akizungumza na wajumbe na washiriki wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mwakitalu amesema ni vema viongozi hao wakaimarisha ushirikiano kati yao na wadau wengine wakiwemo wadau wa haki jinai ili kurahisisha utendaji kazi wao.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi  Mwakitalu amewataka madereva wa Ofisi ya Mashtaka nchi nzima kufanya kazi zao kwa kuzingatia na kufuata Sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.

Amesema   Madereva wasipozingatia  sheria, kanuni na utaratibu wa usalama Barabarani wawapo barabarani wanaweza sababisha ajali ambazo zinazuilika kwani  ajali husababisha hasara kubwa kwa Serikali, jamii na mtu mmoja mmoja.

‘’Kutofuatwa kwa sheria kunaweza kusababisha changamoto mbalimbali ikiwemo ajali, vifo, ulemavu, na kuharibika kwa mali ambayo serikali hutumia gharama kubwa kuzipata.” Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Aidha amewasisitiza watumishi kuendelea kufanya kazi zao kwa bidii ili kuyafikia mafaniko yaliyolengwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kuhakikisha kuwa haki na ustawi wa jamii vinadumu daima.

Wakati huo huo Baraza hilo limetumia nafasi hiyo kuwaaga watumishi waliostaafu utumishi wa umma katika Ofisi hiyo kwa kufikisha umri wa miaka 60 baada ya kulitumikia taifa ambapo Mkurugenzi Mwakitalu amewasisistiza kwenda kuyaishi mema waliyovuna wangali watumishi.

Wastaafu hao nao wameushukuru uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka  kwa kuwashika mkono wakati wote na kuahidi kuzitumia vema fedha watakazolipwa kama kiinua mgongo.








Share:

BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA MIKUMI.

Wajumbe na washiriki wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza Bw. Sylvester Mwakitalu wamepata fursa ya kutembelea mbuga ya Wanyama ya Mikumi iliyopo Mkoa wa Morogoro ikiwa ni sehemu ya programu ya mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la kujadili na kupitisha Mpango wa bajeti  ya Ofisi  ya Taifa ya Mashtaka kwa Mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika ziara hiyo wajumbe wamepata fursa ya kuona vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo vinapatikana katika hifadhi hiyo vikiwemo Wanyama kama vile Simba, Nyumbu, Twiga, Pundamilia, Tembo na wengine wengi ambapo pia wamepata nafasi ya kujifunza mazingira, jiografia na mandhari  nzuri yaliyohifadhiwa na kutunzwa kupitia Mamlaka za Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Aidha, ziara hiyo ni sehemu ya kuthamini jitihada na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutangaza utalii wa Tanzania kupitia filamu ya The Royal Tour ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii ikiwemo kuhamasisha utalii wa ndani.





Share:

DPP NA MENEJIMENTI YA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YAKUTANA MOROGORO KUJADILI MIKAKATI MIPYA YA UTENDAJI WA OFISI.

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ameendesha kikao kazi cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambacho kinafanyika Mkoani Morogroro kikilenga kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji, ikiwemo Maandalizi ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Tathmini ya utendaji kazi katika robo ya pili ya Octoba-Disemba 2024, Kupitia na kujadili rasimu ya sera ya Usalama  na Afya mahali pa kazi ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. 

Kikao hiki kimefanyika tarehe 19 Machi, 2025 Mkoani Morogroro kikihusisha Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bw. Simon Ntobbi, Wakurugenzi Wakuu wa Divisheni, Wakuu wa Vitengo na Wakurugenzi wasaidizi, ambapo kikao hicho kimelenga kuja na mstakabali mpya wa uendeshaji wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.




Share:

KIKAO CHA WELEDI BAINA YA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA NA WADAU

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Rukwa pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wamefanya kikao cha weledi pamoja na Semina kwa watumishi iliyotolewa kwa Madaktari waliopo katika mkoa huo.

Kikao hicho cha weledi kimefanyika tarehe 15 Machi, 2025 katika ukumbi wa Polisi wa Sumbawanga kwa lengo la kuongeza ujuzi na maarifa, kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wananchi kwa wakati na kufuata misingi ya haki iliyowekwa kisheria.

Katika kikao hicho mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo Elimu juu ya Uchukuaji wa Maelezo ya Onyo kwa njia ya Kimtandao, Uchoraji wa Ramani ya eneo la tukio pamoja na Ujazaji sahihi wa Polisi Fomu namba 3 (PF3), Vinasaba (DNA).

Aidha washiriki hao wameshukuru kwa kupata nafasi hiyo ya kujifunza na kubadilishana uzoefu, pia wameahidi ujuzi walioupata watautumia kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi na kuleta matokeo chanya.

Share:

AHUKUMIWA KUNYONGWA MPAKA KUFA


Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Mtwara imemuhukumu Hamisi Peter Suwed @ Mkwidu (45) kunyongwa mpaka kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la Mauaji ya Jamali Saidi Mtepa.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 13 Machi, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Martha Mpaze baada ya kusikiliza mashahidi watano (5) kutoka upande wa jamhuri pamoja na vielelezo vitano (5) na kujiridhisha kwamba upande wa Jamhuri umethibitisha shtaka pasipo kuacha shaka.

Katika kesi hiyo ya Kikao cha Jinai Na. 28 ya mwaka 2023  Bw. Hamisi am

baye ni mkazi wa kijiji cha Mavuji, Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi alikuwa anakabiliwa na shtaka la Mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.) 

Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 25 Octoba, 2022 katika kijiji cha Mavuji, Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi ambapo inadaiwa kwamba, siku ya tukio majira ya usiku mshtakiwa wakati anarudi nyumbani kwake alimkuta marehemu akiwa anaiba mboga kwenye shamba lake, Mshtakiwa alichukua jiwe na kumpiga marehemu kichwani mara mbili mara baada ya hapo Mshtakiwa aliendelea kwa kuchukua kisu na kumchinja marehemu mpaka kupelekea kifo chake, pia mtuhumiwa alichukua mwili wa marehemu na kuutupa pembezoni mwa mto karibu na shamba lake.

Kesi hii imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali watatu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Jordan Odhiambo akisaidiana na Denis Nguvu  pamoja na Hilal Kabyemela.

Share:

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA SERIKALI UJENZI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA TEMEKE

 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi wa Ofisi za Mashtaka za Mikoa na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kusogeza huduma kwa wananchi  pamoja na kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma za mashtaka ya jinai nchini jambo litakalosaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi na kulinda amani na Usalama ambayo ni dhamira ya Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kukagua maendeleo ya  Miradi ya ujenzi wa Ofisi za Mashtaka za Mikoa ya Kimashtaka Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam, tarehe 12 Machi, 2025 Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Mhe. Dkt. Joseph Mhagama alieleza kuwa Kamati hiyo imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hizo za Mikoa ya  Kimashtaka Temeke na Kinondoni ambapo miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, 2025

Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo, Waziri wa Katiba na  Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, aliipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa maono na utashi wa kutekeleza miradi hiyo ya kimkakati na kueleza imetokana na uongozi bora wa viongozi waliopo.

“Mimi ni Wakili hadi sasa, nimefanya kazi ya Uwakili kwa miaka zaidi ya 30 na nimefanya kazi na Wakurugenzi wa Mashtaka wengi, lakini nikupongeze Mkurugenzi wa Mashtaka Mwakitalu kwa mageuzi haya makubwa ambayo yanahitaji utashi mkubwa, uadilifu na kujitoa."

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alimshukuru Mhe. Rais, Kamati ya Bunge na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya mageuzi haya muhimu na kueleza kwamba miradi inayoendelea kutekeleza ni matunda ya Kamati hiyo.

Aidha, aliongeza kuwa miradi hii ni sehemu ya Miradi inayoendelea kutekelezwa katika mikoa mingine ambayo ipo katika hatua mbalimbali na kwamba kuanzia mwaka huu Ofisi ya Taifa  ya Mashtaka imeanza pia kutekeleza miradi ya Ujenzi ya Ofisi za Mashtaka za Wilaya ambapo tayari imeanza katika Wilaya 24 ikiwa ni jitihada za kusogeza huduma kwa wananchi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa pongezi kwa kutekelezwa kwa miradi katika Wilaya hizo na kuongeza kwamba itakua na tija kwa Wananchi.

" Tuna imani kuwa mradi huu ukikamilika kwa wakati utaweza kusaidia sana Watanzania, ambao wanausubiri kwa hamu kubwa sana." Amefafanua Mkuu wa Wilaya.

Aidha, Mhe. Mhagama alisema Kamati  inaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo itachochea upatikanaji wa haki kwa wananchi na kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa usimamizi mzuri wa taasisi zake katika utekekelezaji wa miradi  inayofadhiliwa na Serikali.

Sambamba na hilo alitoa rai kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kusimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa asilimia 100 kwa ufanisi ndani ya muda uliopangwa kulingana na mkataba uliopo.




Share:

MIAKA 20 JELA, VIBOKO 12 KWA KUKUTWA NA FISI HAI BARIADI

 Mahakama ya Wilaya Bariadi mkoani Simiyu imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kuchapwa viboko 12 Emmanuel John (31), maarufu kama Chief wa Kilulu, kwa kosa la kukutwa na Nyara za Serikali aina ya fisi akiwa hai na akiishi naye nyumbani kwake.

Mshtakiwa huyo, ambaye ni mganga wa kienyeji, mkazi wa kijiji cha Kilulu kilichopo kata ya Bunhamala, wilayani Bariadi, alipewa adhabu hiyo katika kesi namba 2458/2025 iliyokuwa ikimkabili kwenye mahakama hiyo.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Caroline Kiliwa, mara baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Awali, akisoma kosa la mshtakiwa, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Lupiana Mahenge, aliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa na nyara ya serikali, fisi akiwa hai, akimfuga nyumbani kwake ikiwa ni kinyume cha sheria.

Alisema kuwa mnamo tarehe 1 Januari, 2025 katika eneo la kijiji cha Kilulu, mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema ambao waliripoti kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai ndani ya nyumba yake.

Alieleza kuwa mtuhumiwa aliishi na fisi huyo kama mnyama wa kufuga kinyume na kifungu cha 86 (1) na kifungu kidogo cha (2)(C)(III) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori sura ya 283, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Alifafanua kifungu hicho kinasomeka pamoja na kifungu cha 14, jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1), na kifungu cha 60 (2) cha Sheria ya Kupambana na Uhujumu Uchumi sura ya 200, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Upande wa mashtaka, katika kuthibitisha kosa hilo, ulipeleka mashahidi sita ambao waliithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka.

Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama imsamehe kwa kuwa anategemewa na familia ya watoto wanne wakiwemo mapacha, ndipo hakimu akatoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na viboko 12 ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine.


Share:

DPP AWAELEKEZA WANAWAKE WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUTUNZA RASILIMALI ZA SERIKALI

 

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwa mstari wa mbele kutunza rasilimali walizopewa na serikali ili kuendelea kuwasaidia katika majukumu yao ya kila siku.

“Muwe ni watu wa kujali na mtunze rasilimali kidogo ambazo tumezipata kwani Serikali imewekeza fedha na rasilimali zingine na tunatarajia wanawake mtakuwa kinara katika kutuvusha kwenye hili hivyo tunataka kuona matokea ya uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.’’ 

Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo wakati aliposhiriki  chakula cha jioni pamoja na  watumishi wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka Makao Makuu Jijini Dodoma, Arusha, Mkoa wa Kilimanjaro na Manyara mara baada ya kushiriki kwenye kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 8 Machi, 2025.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ina watumishi wengi wa kike ambao ni zaidi ya asilimia 65 hivyo wanapaswa kujiamini ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kujituma.

“Utendaji kazi wetu lazima uonyeshe kwamba taasisi yetu ina wanawake wengi kwasababu nyie ni watu wa kujali. Tunataka watu waone Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inafanya vizuri kwasababu ya wanawake.’’ Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu

Pia Mkurugenzi Mwakitalu ametoa pongezi kwa wanawake hao kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kipindi chote cha  Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wakati walipotembelea banda la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Jijini Arusha.  

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewataka wanawake wa ofisi hiyo kuutumia uwezo mkubwa waliopewa na  Mwenyezi Mungu wa Ualimu,Ulezi  kuipendezesha na kuzidi kuiinua  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kazi zao kwa kuzingatia kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo inasema "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.

‘Kama Kauli mbiu ya Mwaka huu 2025 inavyosema,Tuutumie uwezo mkubwa kabisa ambao Mungu ameweka ndani yetu ili kuhakikisha taasisi yetu inaongoza  kutenda haki ndani ya nchi hii hata watakapotafuta siri ya mafanikio ya Ofisi yetu watambue kwamba ni  sababu ya mchango mkubwa pia wa wanawake  waliopo ndani ya ofisi hiyo.” Amesema Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka

Aidha, amewataka wanawake hao kuhakikisha kuwa  wanapoondoka mahali hapo waondoke wakiwa na  chachu ya kufanya kazi kwa bidii,kuwafundisha na kulea wengine na kuahidi kutokuiangusha taasisi yao.

‘’ Ipo nguvu kubwa ndani ya mwanamke ya kuratibu mambo,kufundisha na kulea.

 Ninaomba iyo nguvu pia tuiweke kwenye taasisi yetu kuwafundisha  watumishi walio chinj yetu, ili tuweze kuleta matunda na kufikia maono makubwa ya taasisi yetu.’’ Amefafanua Naibu DPP


Watumishi wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma, Arusha, Mkoa wa Manyara na Kilimanjaro wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kushiriki kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 8 Machi, 2025



Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo akipokea zawadi ya tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa wanawake Bi. Atugonza Kawamala kwa niaba ya wanawake wote wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika taasisi.


Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo akikata keki kuashiria upendo na umoja kwa watumishi wanawake wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka




Share:

ALIYEUA MWIZI AHUKUMIWA KUNYONGWA MPAKA KUFA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Iringa imemuhukumu Elia Martine Ngaile @ Rasta (54) kunyongwa mpaka kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la Mauaji ya Luca Pascal Mang’wata.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 7 Machi 2025 na Mhe. Jaji Angaza Mwipopo baada ya kusikiliza mashahidi wanne (4) wa upande wa jamhuri pamoja na vielelezo viwili (2) na kujiridhisha kwamba kesi upande wa Jamhuri imethibitishwa pasipo kuacha shaka.

Katika kesi hiyo ya Kikao cha Jinai Na. 26195 ya mwaka 2024, Bw. Elia ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ndiwili, wilaya ya Kilolo mkoa wa Iringa alikuwa anakabiliwa na shtaka la Mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.) 

Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe  21 Mei, 2024 katika kijiji cha Lundamatwe, kitongoji cha Kibati, Wilaya ya Kilolo ambapo inadaiwa mshtakiwa alikuwa akitafuta mwizi wa ng’ombe wanne (4) na alifanikiwa kumkamata marehemu na kumfungia katika kilabu cha pombe na marehemu alipotaka kukimbia alimkamata na kumkata na panga kichwani, mkononi na miguuni. Kitendo hicho kilisababisha marehemu kuvunjika miguu yote miwili na fuvu la kichwa kuwa wazi pamoja na ubongo kuonekana. Majeruhi alipelekwa hospitali kwa matibabu hatimae alifikwa na umauti akiwa anapatiwa matibabu hospitali ya Rufaa Iringa.

Kesi hii imeendeshwa na Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambao ni Muzzna Mfinanga akisaidiana akisaidiana na Majid Matitu.

Share:

AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA.

Mahakama ya Wilaya ya Momba imemuhukumu Bw. Laurent Emmanuel Sigula (18) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia kusafirisha dawa za kulevya aina bhangi yenye ujazo wa gramu 240.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 6 Machi, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu Raymond Kaswaga baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa mashtaka. 

Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 24 Aprili, 2024 katika  eneo la Migombani, Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba alipokutwa na Mtendaji wa Mtaa akimiliki misokoto 122 ya bhangi yenye gramu 240 kisha kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi na alipohojiwa alikiri bhangi hiyo kukutwa nyumbani kwake.

 Kesi hii iliendeshwa na Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka akiongozwa na Wakili Shadrack  Meli akisaidiana na Sadam Kitembe.

Share:

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 2 JELA KWA KUMUUA BABA YAKE BILA KUKUSUDIA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Sumbawanga imemuhukumu Kiumbe John Kantanga (28)  kifungo cha miaka 2 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kumuua baba yake mzazi bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 5 Machi 2025 na Hakimu Mwandamizi na mwenye Mamlaka ya Ziada Luambano baada ya kuridhika na kiri ya mshtakiwa na maelezo ya shauri.

Katika kesi hiyo ya Kikao cha Jinai Na. 16279 ya mwaka 2024,Bw. Kiumbe ambaye ni mkazi wa kijiji cha Bumanda, wilaya ya Nkasi mkoa wa Rukwa alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuua bila ya kukusudia kinyume na kifungu cha 195 na 198 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.

Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe  25 Mei, 2024 katika kijiji cha Bumanda, wilaya ya Nkasi ambapo inadaiwa mshtakiwa alimpiga shoka baba yake baada ya kutamkiwa maneno yaliyomfanya kujawa na jazba.

Kesi hii imeendeshwa na japo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Ladislaus Akaro akisaidiana na Mwanaisha Liwawa.

Share:

AHUKUMIWA KUNYOGWA MPAKA KUFA KWA KUUA.

 

Mahakama ya Hakimu Mkazi Sumbawanga yenye Mamlaka ya ziada imemhukumu  Sanyiwa Nyorobi  maarufu kwa jina la Ntemasho na kumpa adhabu ya kunyogwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la Mauaji ya mkazi wa Sumbawanga Tiga Washa.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 4 Machi, 2025 na  Hakimu Mkazi mwenye Mamlaka ya ziada Mhe. Joseph Luambano baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri.

Katika kikao cha Jinai namba 14637 cha mwaka 2024, Bw. Sanyiwa ni mkazi wa Kijiji cha Kilangawana kilichopo ndani ya Wilaya ya Sumbawanga , Mkoa Rukwa alikuwa anakabiliwa na shtaka la Mauaji  kinyume na kifungu cha 196 and 197 cha Sheria ya kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 18 Desemba,2023 katika Kijiji cha Kilangawana kilichopo ndani ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoa Rukwa ambapo inaidaiwa siku ya tukio mshtakiwa alivamia nyumbani kwa Tiga Washa ( Marehemu) na kumjeruhi kwa kumkatakata mapanga katika mwili na kupelekea kifo.

Kesi hiyo imeendeshwa na  Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Neema Erasto Nyagawa akisaidiana na Mathias Yatti Joseph.

Share:

AKUHUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA MITATU JELA KWA KOSA LA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA

 

Mahakama ya Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam imemhukumu Amosi Janus Nyitara 

 (23) kifungo cha miaka 03 jela baada ya kupatikana na dawa za  kulevya aina ya bhangi kiasi cha gramu 49.2.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 28 Februari, 2025 na  Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Vicky Mwaikambo  baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 2685/2024, Bw. Amos  ambaye ni mkazi wa Mbagala Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la kukutwa na dawa za  kulevya aina ya bhangi gramu 49.2 kinyume na kifungu cha 17(1) (b) cha Sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya , (Sura ya 95 Rejeo la mwaka 2019)

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 14 August, 2023 katika eneo la Kibonde Maji B Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam, alikutwa na madawa hayo isivyo halali.

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Sabina Ndunguru Bundala akisaidiana na Nicas Kihemba.

Share:

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 20 JELA KWA SHAMBULIO LA AIBU DHIDI YA BINTI MWENYE UMRI WA MIAKA 13


 Mahakama ya Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es salaam imemhukumu  Hilary Benard Matia (37) kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la shambulio la aibu dhidi ya  binti mwenye umri wa miaka kumi na tatu (13).

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 28 Februari, 2025 na  Hakimu wa Mahakama hiyo Mhe. Vicky Mwaikambo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 2969/2024 ya Bw. Benard  ambaye ni mkazi wa Toangoma  Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la Shambulio la aibu  (grave sexual abuse) kinyume na kifungu cha 138C(1) (a) and (2) (b) cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 01 December, 2023 katika eneo la Kongowe Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam ambapo inaidaiwa siku ya tukio mshtakiwa kwa tamaa za kimwili  alimnyonya mdomo mhanga ambaye ni mwanafunzi wake.

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Sabina Ndunguru akisaidiana na Nicas Kihemba.

Share:

AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 30 JELA KWA KOSA LA KUZINI NA MAHARIM


 Mahakama ya Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam imemhukumu Bw. Silvester Michael Chihongwe (42) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka miwili

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 28 Februari, 2025 na  Mhe. Catherine Madili baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 9568/2024, Bw. Silvester ambaye ni mkazi wa Kurasini, Shimo la Udongo Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la kuzini na Maharimu (incest) kinyume na kifungu cha 158(1) cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 22 Machi, 2024 katika eneo la Kurasin, Shimo la Udongo Wilaya ya Temeke Jijini Dar es salaam ambapo inadaiwa mama wa mtoto huyo alikwenda kuchota maji aliporudi alikuta tayari mtoto huyo amefanyiwa kitendo hicho na baba yake mzazi.

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Wakili Abdon Andrew Bundala akisaidiana na Shabani Twahil Shaban.

Share:

 

Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam imemhukumu Bw. Arafath Laurence Thadei kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya kiasi cha shilingi milioni moja pamoja na kuchapwa viboko sita wakati wa kuingia gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka Manusura mwenye umri wa miaka 15.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 27 Februari, 2025 na Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam Mhe. Janeth Mtega baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kutoka upande wa Jamhuri.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 22093/2024 Bw. Thadei ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la ubakaji kwa Manusura kinyume na kifungu cha 130(1),(2) (a) na 131 cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022)

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo katika tarehe zisizojulikana kati ya mwezi wa 12 mwaka 2023 na tarehe 4 Machi 2024 katika eneo la Tungi,Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam ambapo inaidaiwa alimuingilia kimwili binti wa miaka kumi na tano(15).

Kesi hiyo imeendeshwa na jopo la Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka likiongozwa na Bw. Sayi Gugah akisaidiana na Epiphania Mushi.

Share:

ALIYEMUUA MKEWE KISHA KUMCHOMA KWA MAGUNIA YA MKAA AHUKUMIWA KUNYONGWA


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam imemhukumu mfanyabiashara Bw. Hamis Said Luwongo mwenye umri wa miaka 38 kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa aliyejulikana kwa jina la Bi. Naomi Marijani kisha kuchoma mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.

Hukumu hiyo imetolewa tarehe 26 Februari, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Hamidu Mwanga, baada ya kuridhishwa na ushahidi wa  mashahidi 14 na vielelezo 10 kutoka upande wa Mashtaka.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, jopo la Mawakili wa Serikali wawili likiongozwa na Wakili wa  Serikali Mkuu Bi. Yasinta Peter akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Bi. Ashura Mnzava, waliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa wale wanaofanya ukatili dhidi ya wanawake wanaume wote wanaowafanyia ukatili wanawake wao kwa kigezo kuwa wapo kwenye ndoa.

"Kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha ukatili na kinaleta mashaka kwa wanawake waliopo katika ndoa na wanawake wanaoingia katika ndoa, hivyo tunaomba Mahakama yako itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wanaume wanaotumia kigezo cha ndoa kufanya ukatili kwa wake zao.” Amesema Wakili Mnzava.

Katika kesi hiyo ya Jinai namba 44/2023, Bw. Hamis Luwongo ambaye ni mkazi wa Gezaulole, Wilayani Kigamboni, Jijini Dar es salaam alikuwa anakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia ya mkewe Naomi  kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.

Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 15 Mei, 2019 nyumbani kwao, kisha akauchoma mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku ambapo inadaiwa masalia ya mwili na majivu aliyachukua akaenda kuyazika shambani na kupanda migomba juu yake kwa lengo la kuficha ushahidi.

Share:

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWANOA MAAFISA VIUNGO JUU YA NAMNA YA KUSHUGHULIKIA MAKOSA DHIDI YA BINADAMU NA MAKOSA YATAKAYOJITOKEZA KATIKA KIPINDI CHA UCHAGUZI

 Mkurugenzi wa Mashtaka  Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kushughulikia makosa dhidi ya binadamu na yatakayojitokeza katika kipindi cha Uchaguzi mkuu ili kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa Taifa na  kuhakikisha wale wote wanaovunja sheria wanashughulika nao ipasavyo kwa kufuata taratibu na sheria za makosa ya jinai.

Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akifungua Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwasababu yatawakwamua katika changamoto kadhaa zinazofanya utendaji kazi wao ukwame mahali fulani na kupelekea kutokupata matokeo wanayoyatarajia.  

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mwakitalu ameipongeza Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kwa kuanzisha na kuwaita Maafisa Viungo wanaoiwakilisha  idara hiyo katika kila mkoa kwa lengo la kuwapa mafunzo.

“Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi  inasimamia asilimia kubwa ya kesi tunazoshughulika nazo huko mikoani zikiwepo kesi za Ukatili wa Kijinsia kwa maana ya Ubakaji, Ulawiti idadi yake ni kubwa sana katika Mahakama zetu, na zilizofika mahakamani ni kidogo sana ukilinganisha na matukio yanayotokea, na yale yanayoripotiwa katika Vituo vya Polisi na hayafiki asilimia 20. 

Tunayo makosa yanayogusa mali yakiwepo wizi, unyang'anyi kwa kutumia silaha, makosa haya yote yanaangukia katika idara hiyo na pia ndio makosa mengi ambayo yanafanyika kwenye jamii zetu.” Amesema Mkurugenzi Mwakitalu.

Pia Mkurugenzi wa Mashtaka amesema kupitia mafunzo hayo wanatarajia kwenda kuongeza ubora wa uratibu katika Upelelezi na Uendeshaji wa Mashtaka

“Tunategemea kuona uboreshaji zaidi juu ya namna tunavyoshughulikia Uratibu wa Upelelezi wa Makosa haya pamoja uendeshaji wake mahakamani.”

Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka amewataka Maafisa Viungo hao kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kuyafahamu majukumu ya idara husika kwa ukamilifu ili kuleta mabadiliko juu ya namna ambavyo wanashughulikia makosa hayo yanayoangukia kwenye idara husika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kila baada ya mwezi mmoja ya namna wanavyotekeleza majukumu  katika mikoa yao.

Katika kuelekea kwenye kipindi cha Uchaguzi mkuu unaotarajia  kufanyika Mwezi Oktoba mwaka 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka amesema  kipindi hicho kinakuwa na mambo mengi, wananchi wana haki na wajibu wao kwenye shughuli za uchaguzi lakini wapo wale wanaopitiliza mipaka na kuvunja Sheria na kutenda makosa ya jinai,   hivyo maafisa viungo hao wanalo jukumu la kusimamia hilo Ili kudumisha amani nchini.

‘’Mtapitishwa kwenye makosa yanayohusiana na kipindi hicho na namna ambavyo tunaweza kuyashughulikia. Tunataka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tufanye kazi yetu kwa weledi hata katika kipindi hicho cha kampeni, kipindi cha maandalizi ya uchaguzi na hata baada ya matokeo ya uchaguzi, tuhakikishe tunatimiza wajibu wetu kwa Taifa, katika kuhakikisha wale wanaovunja sheria tunashughulika nao ipasavyo. Na pia pale ambapo tunaweza tukashauri makosa hayo yasifanyike basi hatuna budi kufanya hivyo.” Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Javelin Rugaihuruza amesema kupitia mafunzo hayo Maafisa Viungo watapitishwa kwenye mada mbalimbali kuhusiana na majukumu ya idara hiyo  ambayo wanatakiwa kufanya ili kusaidia kuweza kutekeleza majukumu yao kama idara pamoja na mambo mengine. 

Aidha, watapata nafasi ya kupitishwa kwenye Ushughulikiaji wa makosa ya Ukatili wa Kijinsia.

Kama tunavyofahamu makosa ambayo yanaongoza mahakamani ni makosa ya Ukatili wa Kijinsia, tumeona tuitumie nafasi hii kuwapitisha katika  mada hiyo ili tuweze kuona ni jinsi gani makosa hayo yanaweza kushughulikiwa na changamoto zilizopo katika makosa hayo ili kuweza kuepukana na Changamoto hizo kama sio kuzipunguza basi kuziondoa kabisa.


Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu  akifungua Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Javelin Rugaihuruza akimkaribisha Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu kufungua Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika  katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025.


Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bi. Pendo Makondo akiwasilisha mada inayohusu Uelewa juu ya Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi na majukumu ya Maafisa Viungo kwenye Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025.


Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo kwa Maafisa Viungo wa Idara ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi yanayofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma tarehe 10 hadi 12 Februari, 2025

Share:

DPP AWATAKA WAAJIRIWA WAPYA KWENDA KUFANYA KAZI KWA WELEDI, UADILIFU NA UZALENDO

 

Mkurugenzi wa Mashtaka  Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka watumishi wapya walioajiriwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambao ni Mawakili wa Serikali na Makatibu Sheria kwenda kufanya kazi kwa  weledi, umakini, uadilifu na uaminifu pamoja na kuzingatia Sheria, Kanuni na Misingi ya Utumishi ya Umma ili kuifanya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kuwa Taasisi yenye  misingi bora na ya mstari wa mbele katika kusimamia haki.

“Kufanya kazi kama Wakili wa Serikali ni heshima kubwa sana hivyo naomba muilinde heshima hiyo kwani kazi yetu inahitaji umakini, weledi, uadilifu na uaminifu, tunataka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iendelee kuwa mstari wa mbele kwenye kusimamia haki za watu na hili tunalitegemea kutoka kwenu.’’

Mkurugenzi wa Mashtaka ameyasema hayo tarehe 5 Februari, 2025 wakati akizungumza na watumishi waajiriwa wapya waliofika Makao Makuu, Dodoma kwa ajili ya kuchukua barua zao za kwenda kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.

Mkurugenzi Mwakitalu alisema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni ofisi ambayo imebeba haki za watu mkononi na kwamba maamuzi watakayoenda kufanya waajiriwa hao wapya ya kushtaki ama kutokushtaki ni maamuzi ambayo moja kwa moja yanagusa haki za watu, hivyo aliwaasa kuwa wanapaswa kuwa makini katika kila hatua wanayoifanya na kuhakikisha wanajiandaa vizuri kabla ya kwenda mahakamani ili kuisaidia mahakama kufanya maamuzi yaliyosahihi katika utoaji haki.

Aidha, amewataka pia waajiriwa wapya hao kutenga muda kupitia miongozo mbalimbali ambayo imewekwa katika tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambayo itawasaidia  kujifunza na kuongeza uzoefu katika utendaji kazi wao wa kila siku.

”Uzoefu mlioupata huko kabla hamjaja hapa uleteni, kama kuna kitu kinaweza kutusaidia  kuboresha utoaji wetu  huduma kwa wananchi leteni na sisi tutakuwa tayari kupokea na kufanyia kazi kama kitaleta tija kwenye kazi zetu.”, Aliongea Mkurugenzi Mwakitalu

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewapongeza waajiriwa wapya  kwa kupata nafasi ya kuingia katika Utumishi wa Umma  na pia kupata bahati ya kuungana na familia ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka hivyo na kuwataka kwenda kuzingatia yale yote watakayoelekezwa wakati wakiwa kazini.

‘’Mkizingatia yale yote mtakayoelezwa na viongozi wenu itawaletea mafanikio makubwa sana kwenye safari yenu ya utumishi na kukuwa katika taaluma yenu.’’ Alisema Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bw. Simon Ntobbi amewaasa waajiriwa wapya hao kuwa na hofu ya Mungu ili waweze kutenda haki kwa wananchi watakaokwenda kuwahudumia.

‘’ Tunashukuru kwa kupata nguvu mpya hivyo mkiwa kama Mawakili tunawategemea mkatende haki, mkawasaidie wananchi wa hali ya chini naya juu kwa kutenda haki." Aliyasema hayo Mkurugenzi wa Utawala.

Katika hatua nyingine, watumishi hao wapya walipata pia fursa ya kuelekezwa Masuala mbalimbali ikiwemo miongozo na elimu kuhusa Afya Mahali Pa Kazi na uepukaji wa vitendo vya Rushwa ambapo walijaza fomu za Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu pamoja na kujifunza kuhusu Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma, wasilisho lililotolewa na Afisa Tawala Mkuu, Ndugu Juma S. Katanga.


Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu  akizungumza na watumishi waajiriwa wapya waliofika Makao Makuu, Dodoma kwa ajili ya kuchukua barua zao za kwenda kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.



Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo akimkaribisha Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu kuzungumza na Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mara baada ya kuwasili Makao Makuu Jijini Dodoma kwa lengo la kuchukua barua zao na kwenda kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa.




Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Simon Ntobbi  akizungumza na Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mara baada ya kuwasili Makao Makuu Jijini Dodoma kwa lengo la kuchukua barua zao na kwenda kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa.

Share:

RAIS SAMIA AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo yalifanyika kitaifa katika viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma, mnamo tarehe 03 Februari, 2025. Hafla hiyo muhimu, ambayo huadhimishwa kila mwaka, imekusanya viongozi mbalimbali wa kitaifa, majaji, mawakili, maofisa wa serikali, na wadau wengine wa sekta ya sheria.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais alisisitiza umuhimu wa mfumo wa sheria imara katika maendeleo ya taifa, akibainisha kuwa utawala wa sheria ni msingi wa haki, amani, na maendeleo endelevu. Aliwataka wadau wa sheria, wakiwemo mawakili na majaji, kuendelea kuwa mfano wa uadilifu na uwajibikaji katika kutoa haki kwa wakati na bila upendeleo. 

“Tunapoadhimisha siku hii ya sheria, napenda kusisitiza kuwa uwajibikaji wa vyombo vya sheria ni muhimu katika kuleta imani ya wananchi kwa serikali na taasisi za kisheria. Hatuna budi kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote kwa usawa,” alisema Rais Samia. 

Maadhimisho ya mwaka huu yalibeba kaulimbiu inayolenga kukuza ufahamu wa wananchi juu ya umuhimu wa upatikanaji wa haki kwa njia za haraka, zenye gharama nafuu na zenye kuzingatia haki za binadamu. Pia, yalihusisha shughuli mbalimbali kama maonesho ya huduma za kisheria, mijadala ya kitaalamu, na mashauriano ya bure kwa wananchi.

Aidha, Rais alitumia nafasi hiyo kupongeza juhudi za Mahakama ya Tanzania kwa maboresho ya kiteknolojia yaliyofanyika hivi karibuni, yakiwemo mfumo wa kuendesha kesi kwa njia ya mtandao (e-filing) na matumizi ya majukwaa ya kidigitali katika kupunguza mlundikano wa kesi. 

“Ni faraja kubwa kuona kwamba Mahakama yetu inaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa haki siyo tu inatendeka, bali pia inaonekana kutendeka kwa wakati unaofaa,” aliongeza Mhe. Samia. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha mifumo ya sheria na upatikanaji wa haki nchini.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Majaji, wageni waalikwa pamoja na wananchi kwa ujumla kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma tarehe 3 Februari, 2025



Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na Mkoa wa Dodoma wameshiriki Maadhimisho ya Siku ya Sheria ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma tarehe 3 Februari, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Taasisi mbalimbali walioshiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma tarehe 3 Februari, 2025

Share:

Labels

Blog Archive

Recent Posts

MKURUGENZI WA MASHTAKA

MKURUGENZI WA MASHTAKA AWAONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU ASEMA NCHI INAPASWA KUWA SALAMA WAKATI WOTE Contact me .